November 8, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Watu 172 kortini kwa kufanya vurugu, unyang’anyi siku ya Uchaguzi

 

WATU 172 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza na kusomewa mashtaka kadhaa yakiwemo ya kuharibu mali, kuchoma moto na unyang’anyi wa kutumia silaha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya tarehe 29 na 30 Oktoba mwaka huu.

Washitakiwa hao wamefikishwa mahakamani leo tarehe 7 Novemba 2025 chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi na kusomewa mashitaka yanayowakabili kwa nyakati tofauti na kwa makundi kulingana na maeneo wanakodaiwa kutenda makosa hayo.

Akisoma shtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Raula Shehagilo, Kiongozi wa Jopo la Waendesha Mashtaka wa Serikali, Jaines Kihwelo akisaidiana na Heleni Mabula na Sara Heperias amesema shtaka linalokabili kundi la kwanza linadaiwa kutenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287(a) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023, kosa wanalodaiwa kulitenda tarehe 30 Oktoba mwaka huu.

Aidha, mwendesha mashtaka huyo wa Serikali amesema kwa nyakati tofauti watuhumiwa hao wakishirikiana na watu wengine ambao bado hawajakamatwa, wanashtakiwa kwa kosa la kuharibu mali kwa makusudi kinyume na kifungu cha 326 (1) cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marekebisho mwaka 2023, kufanya fujo kinyume na kifungu cha 74(1) na cha (2) 76 na 37 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.

Kosa lingine linalowakabili washtakiwa hao ni kuharibu mali, kosa wanalodaiwa kulitenda kinyume na kifungu cha 326(1) cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023, kuchoma moto mali kinyume na kifungu cha 319 (a)(b) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023, kufanya maandamano bila kibali kinyume na kifungu cha74 (1)(2) 76 na 37 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.

Washtakiwa wote wamekana kutenda makosa hayo. Pia wamekosa dhamana kutokana na sehemu ya makosa yanayowakabili kutodhaminika na waheshimiwa mahakimu kwa nyakati tofauti wameelekeza washtakiwa hao kurudishwa rumande hadi kesi hiyo itakapoitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa, tarehe 17,19 na 20 Novemba mwaka huu.

About The Author

error: Content is protected !!