November 8, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Chadema yalaani kukamatwa viongozi wake

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi Chadema, Brenda Rupia

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelaani hatua ya vyombo vya dola kuwasaka na kuwakamata viongozi wake. Kinasema, kitendo hicho, kinalenga kukivuruga na kuvuruga uendeshaji na shughuli zake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama kikuu cha upinzani nchini, Brenda Rupia, ameeleza kuwa chama chake, hakihusiki na kilichotokea siku ya uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba mwaka huu.

Brenda ambaye ametajwa kwenye orodha ya wanasiasa wa upinzani wanaosakwa na jeshi polisi kwa tuhuma za kuchochea maandamano yaliyoishia kwa ghasia na vifo, amelituhumu jeshi hilo, kutumika kisiasa.

Kwa mujibu wake, zaidi ya nusu ya viongozi wa chama hicho wako mikononi mwa polisi au wanatafutwa, jambo analosema, “linaashiria jitihada za makusudi za kuua sauti ya upinzani nchini.”

Kauli ya Brenda imekuja siku moja, baada ya jeshi la polisi, kutoa orodha ya watu kadhaa inayodai inawatafuta kuwahoji, kuhusiana na madai ya kuchochea vurugu siku ya uchaguzi.

Brenda anasema, “…kuna mkakati wa makusudi wa kutaka kuihusisha Chadema na maandamano hayo. Hilo halikubaliki. Aliyeitisha maandamano anafahamika. Tusitupiwe tuhuma zisizotuhusu.”

Anaongeza, “Maandamano yale yangekuwa ya Chadema, tungeyatolea taarifa. Tungeyaitisha kwa kueleza wapi yanaanzia na wapi yataishia. Na siku zote, huwa hatufanyi vitu sirini. Tunafanya vitu vyetu hadharani,” amefafanua kiongozi huyo.

Tayari mamia ya watu wamefikishwa mahakamani jana Ijumaa, katika mikoa mbalimbali nchini, na kufunguliwa mashtaka yanayotokana na maandamano ya uchaguzi ya Jumatano iliyopita.

Jijini Dar es Salaam, taarifa zinasema, watu 240 walipandishwa kizimbani na kufunguliwa mashitaka ya uhaini.

Katika maandamano hayo, watu kadhaa wameripotiwa kupoteza Maisha. Waandamanaji walikuwa wakilamikia uonevu, ikiwamo matendo ya utekaji na utesaji.

Nako jijini Mwanza, watu 172 walipandishwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kuchoma moto na uharibifu wa mali, huku watu wengine 11 wakishitakiwa mkoani Kigoma.

Mjini Dodoma watu 25 walifunguliwa mashtaka ya uhaini na uharibifu wa mali.

Katika mkoa wa Kaskazini mwa Tanzania – Arusha – watu kadhaa wamefunguliwa mashitaka hayo, akiwamo mwandishi wa habari wa kituo cha Millard Ayo, Godfrey Thomas.

Maandamano yaliyoanzia Dar es Salaam, yalisambaa katika maeneo mengine, ikiwemo majiji ya Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma.

Karibu maeneo yote yaliyofanyika maandamani, kumefanyika uharibifu mkubwa, ikiwamo watu kadhaa kuripotiwa kufariki dunia.

Lakini baadhi ya familia zilizopoteza wapendwa wao kwenye maandamano hayo, wanalalamika kuzuiliwa kuzika ndugu zao, huku wengi wao, wakidai miili ya wapendwa wao, imeondolewa hospitalini.

About The Author

error: Content is protected !!