Cyprian Musiba
MWANAHARAKATI huru, Cyprian Majura Musiba, ambaye miezi michache iliyopita alijiunga na chama cha ACT Wazalendo na kuwania ubunge wa jimbo la Mwibara, ametangaza kuachana na siasa. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).
Alihamia ACT-Wazalendo akitokea Chama cha Mapinduzi (CCM) alipokatwa katika kinyang’anyiro hich.
Katika ujumbe wake alioandika leo, tarehe 5 Novemba, 2025 kupitia mitandao ya kijamii, amewataka Watanzania kutafakari upya kuhusu hatima ya taifa lao na kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Musiba amesema taifa linapaswa kurejea katika misingi ya utu, upendo na kuvumiliana iliyowekwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Ndugu zangu Watanzania, ni muda wa kutafakari utamaduni huu mpya katika nchi yetu. Amani, umoja na mshikamano ndiyo tunu ya taifa letu. Kwa heshima na nidhamu kubwa ninawaomba wananchi wenzangu kutafakari hatima ya nchi yetu iliyoasisiwa na Baba wa Taifa,” ameandika Musiba.
Ameeleza kuwa, licha ya maumivu na huzuni kutokana na matukio ya vifo na uharibifu wa mali vilivyotokana na uchaguzi mkuu uliofanyika siku chacje zilizopita ni muhimu taifa lisiwe na visasi bali litafakari njia ya kurejesha umoja na amani.
“Najua tuna maumivu makali mno, lakini pamoja na maumivu hayo ya kupoteza wapendwa wetu na vijana wetu, nawaomba tutafakari hatima ya nchi na vizazi vyetu vijavyo. Turejee kwenye misingi yetu ya utu, upendo, amani na mshikamano,” ameongeza.
Musiba ameeleza pia kuwa amefikia uamuzi wa kujiondoa katika masuala yote ya kisiasa, ikiwemo uanachama wa chama chake cha awali na vyama vingine vyote nchini.
ZINAZOFANANA
Watahiniwa 937,581 wafaulu elimu ya msingi
Mwabukusi alaani Heche kutuhumiwa kwa ugaidi
Rais Samia amuapisha Mwanasheria Mkuu