Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi Chadema, Brenda Rupia
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza orodha ya majina ya watu 52 wakiwemo viongozi wa chama hicho, wafuasi na wanachama wake, walioripotiwa kutekwa katika kipindi cha mwezi mmoja. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho, iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, kati ya tarehe 1 Oktoba hadi tarehe 25 Oktoba mwaka huu, zaidi ya watu 52 wamechukuliwa na jeshi la polisi, huku wengine wakidaiwa kuchukuliwa na watu wasiofahamika.
MwanaHALISI Online, limeshindwa kumpata msemaji wa jeshi la polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), David Misime, kuzungumzia madaia hayo. Tunaendelea kumtafuta.
Lakini taarifa ya Chadema inasisitiza kuwa matukio hayo ya utekaji yametokea katika maeneo mbalimbali nchini ndani ya siku 25 zilizopita.
“Katika kipindi hicho, jumla ya watu 52 wametekwa, wengi wao wakiwa viongozi na wanachama wa Chadema, pamoja na wanachama wa vyama vingine vya siasa na wananchi wa kawaida,” imeeleza taarifa ya chama hicho.
Chadema kimeyaeleza matukio hayo kuwa yamezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii kuhusu hali ya usalama na uhuru wa raia.
Kimeongeza, “…hali hiyo inahitaji hatua za haraka za Serikali. “Tunatoa wito kwa vyombo husika kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usalama wa raia wote bila kujali vyama au itikadi za kisiasa.”
Katika kuhakikisha usalama wa raia, chama hicho, kimewataka wananchi kujilinda na kuwa makini katika kipindi hiki kigumu ambacho matukio ya utekaji yamekithiri.”
Taarifa ya Chadema, imekuja siku moja baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kuvikumbusha vyombo vya dola, umuhimu wa kuyasaka “magenge ya watekaji nchini.”
Alisema, “wajibu wa vyombo vya dola, ni kulinda rai ana kulinda viongozi waliopo kwa mujibu wa Katiba. Siyo sahihi kwa vyombo hivyo, kunyamazia matendo haya kana kwamba hawahusiki nayo.”
Kwa mujibu wa Gwajima, kuna ushahidi wa kutosha wa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo, uliotolewa na baadhi ya waliopatwa na mkasa huo.
Miongoni mwao, ni Edgar Mwakalebela, maarufu kwa jina la Sativa, aliyetekwa tarehe 23 Juni mwaka jana na kutelekezwa kwenye msitu huko Katavi, mkoani Rukwa.
Gwajima anasema, hata waliomteka Humphrey Polepole, wanafahamika kwa kuwa baadhi ya watekaji husimulia waliyotenda baada ya kukamilisha kazi yao.
Kwa muda sasa, taifa la Tanzania limeshuhudia matukio makubwa ya utekaji yanayoibua taharuki na maswali makubwa kuhusu usalama wa wananchi.
Vitendo hivi vinaendelea kuathiri taswira ya taifa na kuacha raia wakiishi kwa hofu ya usalama wao binafsi.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na usalama, wanatupia lawama vyombo vya dola, kushindwa kukabiliana na na wimbi hili zaidi ya kukanusha kila wakati.
Aidha, wadau wa haki za binadamu na wanaharakati wamesisitiza kuwa ukimya wa viongozi wakuu kuhusu hali hiyo, unazidisha kuongeza wasiwasi nchini.
“Wananchi wanataka uwajibikaji, uwazi na mipango madhubuti ya kusitisha vitendo hivi vinavyoendelea kujitokeza,” ameeleza Juma Bakari, mkazi wa Kinondoni, aliyezungumza na gazeti hili jana.
Anasema, “usalama wa kila raia, bila kujali nafasi yake katika jamii, unapaswa kulindwa kwa ufanisi.”
Anaongeza, “Hatua madhubuti zinahitajika sasa ili kuliimarisha taifa na kulinda hadhi ya Tanzania kama nchi yenye amani na haki.”
Akihutubia Bunge la Jamhuri, tarehe 27 Juni 2025, Rais Samia Suluhu Hassan, aliliagiza jeshi la Polisi nchini, kuchunguza matukio ya utekaji.
ZINAZOFANANA
Mamlaka za ulinzi chukueni hatua kuzuia njama za kuhujumu uchaguzi
Gwajima acharuka tena, akemea utekaji
Chadema yataka Heche achiwe huru