
Steven Wassira
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira amewataka Watanzania wakatae woga na wajitokeze kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).
Wassira amesema kuwa nchi iko salama na dola ya CCM iko pale kwa kuwa hakuna mtu yeyote atakayechezea chochote.
Kiongozi huyo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na viongozi wa CCM Wilaya ya Geita, akiwa katika ziara ya kumnadi na kumwombea kura mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, wagombea ubunge na udiwani.
Amewasisitiza viongozi wa chama hicho kuhakikisha Watanzania hawanunui woga wanaouziwa na mitandao ya kijamii juu ya upigaji wa kura utakaofanyika wiki ijayo.
Wassira amesema wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kupiga kura na wakifanya hivyo dunia itajua kwamba uchaguzi umefanyika Tanzania na wananchi wamepiga kura.
“Wanaosema hapana waende wakapige kura na wanaosema ndio nao waende halafu tuhesabu (kura) watashika kichwa waseme hatukujua kama mambo yangekuwa hivi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Wassira, amewaagiza viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya shina kuhakikisha wananchi wanatoka kwenye nyumba zao na kwenda kupiga kura kumchagua rais, diwani na mbunge.
Amebainisha kuwa msukumo zaidi uwekwe katika maeneo ambayo wagombea chama hicho wamekosa wapinzani wa kuchuana nao kwa kuwa huko wana CCM wanaweza kubweteka kwa kudhania wameshapita bila kupigiwa kura.
“Mamlaka ya nchi yapo mikononi mwa watu na tungependa watu wengi sana wapige kura na kwa sababu ya mazingira ya uchaguzi wa mwaka huu, kwa mfano ukija hapa mjini (Geita) yupo ndugu yangu Waja (Mgombea ubunge Jimbo la Geita Mjini) hana mpinzani sasa katika mazingira hayo watu wanaweza kudhani Waja ameshapita kumbe bado.
“Kwa hiyo twende kwa wanachama, twende kwa wananchi, mabalozi ndio nguvu ya chama chetu na chama chetu ni chama cha wanachama na wanachama wanaongozwa kuanzia nyumba kumikumi.
“Tunawaomba wakuu wa mashina siku ya kupiga kura muwatambue wapigakura wote, sio wanachama tu, wapigakura wote washaurini tu hata wanaotukataa waende (kupiga kura) ili na zao zihesabiwe,” amesema
ZINAZOFANANA
Lissu aibwaga tena serikali
Lissu aweka pingamizi lingine, mahakama kutoa uamuzi kesho.
Lissu aibwaga tena serikali, Heche akamatwa