October 24, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Utekaji umewaamsha wasomi wa UDASA

 

WANAWAZUONI wa UDASA – Jumuiya ya wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – wamelaani kushamiri kwa matukio ya watu kupotea au kudaiwa kutekwa, kikisema hali hiyo inatishia uhuru wa kujieleza na misingi ya haki za binadamu nchini. Anaripoti Shamsa Jumbe, Dar es Salaam … (endelea).

Tamko la kusikitishwa kwa jumuiya hiyo, iliyotolewa leo tarehe 23 Oktoba, inaeleza kuwa matukio ya aina hiyo, yamezua hofu miongoni mwa wananchi na kuathiri taswira ya taifa katika jamii ya kimataifa.

Katika taarifa yake kwa umma, jumuiya hiyo imeitaka serikali na vyombo vya usalama kuchunguza kwa uwazi na kwa haraka visa vyote vya aina hiyo ili kutoa majibu ya kweli kwa umma.

Tamko hilo limerejea ripoti ya shirika la haki za binadamu (LHRC), kuhusu tishio la kile kinachoitwa, “Watu wasiojulijkana,” limelitupia lawama jeshi la polisi nchini kwa ama kushindwa kudhibiti au kunyamazia matendo hayo.

Mara kadhaa jeshi la polisi nchini Tanzania, limedai linaendelea kufuatilia wanaodaiwa kutekwa, na linakanusha kuhusika na wapo wengine waliodaiwa kutekwa kubainika kujiteka.

“UDASA wasomi tuliosomeshwa kwa kodi za Watanzania, tunaowajibu wa kufanya tafakuri ya kina kuhusu kinachoendelea nchini na kutoa mapendekezo stahiki. Katika kutekeleza wajibu wetu huu, tunaangazia mambo mawili:

“Kutoheshimu haki za Watanzania na uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.”

Kuhusu kutoheshimu haki za Watanzania, UDASA wanasema, “Ibara ya 8 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kuwa, Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii. Kwamba, wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na serikali inapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa wananchi.”

Kwamba, “Lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi na serikali itawajibika kwa wananchi.”

Nayo Ibara ya 9 ya Katiba, UDASA inasema, inazitaka mamlaka za nchi, kuzingatia utu na kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa.

Inasema, mamlaka zinatakiwa kuhakikisha kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa.

Wasomi hao wanasema, “heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata kanuni za tangazo la dunia kuhusu haki za binadamu.”

Katika kusisitiza hoja yake, UDASA merejea tena ripoti ya LHRC waliobainisha kati ya mwaka 2021 mpaka 2024 watu 87 wametekwa na kupotezwa.

Aidha, UDASA imewataka viongozi wa serikali, vyama vya siasa na wadau wengine kulinda haki ya kujieleza bila woga wa vitisho au madhara, ikisisitiza kuwa uhuru huo ni nguzo muhimu katika maendeleo ya demokrasia.

Katika tamko hilo, Jumuiya hiyo imeeleza umuhimu wa kujenga mazingira salama kwa wahadhiri, wanafunzi na wanaharakati kushiriki mijadala ya kitaaluma na kijamii bila kuonewa au kudhibitiwa.

UDASA imesema bila uhuru huo, misingi ya utawala bora inaweza kudhoofika.

Chama hicho kimehimiza serikali kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha vyombo vya dola vinawajibika ipasavyo na kwamba kila raia anatendewa haki bila upendeleo.

About The Author

error: Content is protected !!