October 19, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Heche hajaenda Kenya – Chadema

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekana taarifa kuwa makamu mwenyekiti wake, Tanzania Bara, John Heche, amevuka mpaka na kuingia nchini Kenya. Anaripoti Saed Kubenea…(endelea).

Katika barua yake iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa Orange Democratic Movement (ODM), Heche amesema, ameshindwa kuhudhuria mazishi ya kiongozi mkuu wa chama hicho, Raila Odinga, kutokana na kuzuiwa na Idara ya Uhamiaji.

Amesema, viongozi wa chama chake, waliandaa msafara wa viongozi wake wakuu, kuhudhuria “mazishi muhimu ya mwanasiasa mkongwe nchini Kenya,” lakini kwa masikitiko makubwa hawataweza kufanya hivyo.

Amesema: “Tulipanga kuja kuungana nanyi ODM, pamoja na wananchi wengine wa Kenya kwa ujumla, kutoa heshima zetu za mwisho kwa mwanademokrasia huyu mkuu katika eneo hili la Afrika Mashariki.”

Anaongeza: “Hata hivyo, juhudi zetu zimegonga mwamba baada ya kuzuiwa kwenye mpaka wa Isibania One Stop, wilayani Tarime, mkoani Mara. Katika tukio hilo, hati yangu ya kusafiria imechukuliwa na hivyo, kushindwa kuendelea na safari kama ilivyopangwa.”

Anasema, sababu za Chadema kutaka kuhudhuria mazishi hayo, haikulenga kuwa na urafiki na marehemu Raila Odinga na mtu wa karibu na chama chetu, bali alikuwa mshauri wa Chadema na mambo mengine ya kisiasa.

Heche anasema, Odinga na chama chake, wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kupigania haki za watu katika eneo la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, msimamo ambao anasema, unafuatwa pia na Chadema.

Heche anasema, “Marehemu Raila Odinga, atabaki kuwa muhimili na mfano wetu wa kuigwa katika mapambano ya haki, usawa na demokrasia ndani ya Afrika.

“Tunatambua mchango wake kusimamia uwajibaki wa serikali na kuimarisha taasisi zake na kutetea haki na maslahi ya raia.”

Anaongeza, “Kwa niaba ya viongozi wa Chadema, wanachama na wafuasi, tunatuma salaam zetu za pole na rambirambi kwenu, familia yake, wanachi wote wa Kenya na wanachama wote wa ODM.

“Tunasimama nanyi katika kipindi hiki kigumu cha kuombeleza. Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema peponi na awajalie ninyi nguvu, faraja na umoja, katika kipindi hiki kigumu.”

Salaamu za rambirambi za Heche kwa Serikali ya Kenya, familia ya marehemu Odinga na wanachama wa ODM kwa ujumla, imekuja muda mfupi baada ya Idara ya Uhamiaji ya Tanzania, kudai kuwa kiongozi huyo, alivuka mpaka wa Tanzania kuelekea nchini Kenya, bila kufuata taratibu.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanasema, hatua ya Idara ya Uhamiaji kujitokeza mapema na kudai kuwa Heche alivuka mpaka na kuingia nchi jirani, bila kufanyia utafiti taarifa, inathibitisha madai ya wananchi kuwa baadhi ya vyombo vya usalama nchini, vinafanya kazi kwa mihemko ya kisiasa.

About The Author

error: Content is protected !!