
Peter Kibatala
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, imekataa na kutupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na upande wa Jamhuri katika kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi na Cuba, Humphrey Polepole, dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na wengine. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Kesi hiyo, ambayo imefunguliwa kwa hati ya “dharura sana” na Wakili wa familia ya Polepole, Peter Kibatala, ilikumbwa na pingamizi kutoka kwa upande wa Jamhuri uliotaka kuwahoji kwa maswali ya dodoso (cross examination) mashahidi wawili wa upande wa mleta maombi — Peter Kibatala na Godfrey Polepole — waliowasilisha viapo Mahakamani.
Jamhuri ilidai kuwa maswali hayo yangeisaidia Mahakama kupata picha kamili kuhusu mazingira ya kutoweka kwa Humphrey Polepole, ikisisitiza kuwa viapo vya mashahidi hao vilihitaji kuchunguzwa kwa undani zaidi. Hata hivyo, Wakili Kibatala alipinga vikali ombi hilo, akiiomba Mahakama kuliondoa kwa hoja kuwa halina msingi wa kisheria.
Katika uamuzi wake uliotolewa leo, Alhamisi tarehe 16 Oktoba 2025, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Salma Maghimbi, ametupilia mbali pingamizi hilo la Jamhuri. Uamuzi huo unafungua njia kwa Mahakama kuendelea na usikilizwaji wa kesi ya msingi kuhusu kutoweka kwa Humphrey Polepole.
ZINAZOFANANA
JWTZ latoa tamko kuelekea Uchaguzi Mkuu
Isingewezekana Mpina kupata haki – Shahidi wa serikali kesi ya Lissu
Ndege iliyobeba mwili wa Raila Odinga ndiyo inayofuatiliwa zaidi duniani