
MAHAKAMA Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, leo tarehe 15 Oktoba 2025, imeendelea kusikiliza kesi Na. 19605/2025, Jamhuri dhidi ya Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambapo Lissu, ameendelea kumuuliza maswalia dodoso shahidi wa pili wa serikali John Kaaya, ofisa wa polisi anayefanya doria mtandaoni ili kubaini uhalifu, endelea nayo kama ifuatavyo…
Kabla ya shauri hilo halijaanza kusikilizwa wakili wa serikali, Renatus Mkude, ametoa taarifa ya msiba wa msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanya.
“Tumekuwa na utaratibu wa kwenda kushiriki matukio kama haya na tulipanga kuhudhuria kwenye msiba huo kwa vile ni jambo la kibinadamu ilikuwa na rai yetu itakapofika saa tano twende tukamuage huyu ndugu yetu ili tuendelee kesho tena. Ni hayo tu,” alidai Mkude.
Lissu: Mimi sina pingamizi lolote na ikiwapendeza wakienda kwenye huo msiba wanipelekee salamu zangu za rambirambi kwa wafiwa.
Wakati huohuo, Lissu akaeleza mahakamani hapo namna wageni wake waliotoka Ujerumani na Marekani walivyofutiwa visa zao za kuwepo nchini na kurejeshwa kwao.
“Lakini pia niwaeleze kuhusu watu waliokuwa wanazuiwa kuingia mahakamani, nimesema sana jambo hili.
“Kasoro juzi Jumatatu sikulizungumzia kwa sababu niliambiwa wangeruhusiwa siku hiyo lakini walikuja wakazuiliwa hapo getini,” amedai Lissu.
Lissu amedai kuwa amesikia kuwa wageni wake wamefukuzwa nchini “Kwa taarifa nilizonazo walichukuliwa na maafisa wa uhamiaji na baadae wakafukuzwa nchini ili wasiweze kuingia mahakamani kushuhudia kesi hii.”
“Sasa waheshimiwa majaji hii ni mara ya tatu kwa watu wanaotaka kuja kuhudhuria mahakama hii kufukuzwa nchini.
“Walianza na Ujumbe uliotoka Kenya ukiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu wa Kenya, Willy Munyoki Mutunga,” Lissu amedai
Lissu akaikumbusha mahakama hiyo wageni wake wengine waliowahi kukamatwa na kutupwa katika mipaka ya nchini zao “Wakafuata Boniface Mwangi na Agatha Atuhire walikamatwa na kuteswa na kupelekwa mipakani na kutupwa.
“Na sasa hili limetokea kwa raia wa Ujerumani na Marekani walioingia nchini kihalali kuja kutaka kuona kinaendelea nini. Hii ni kesi kubwa kuliko zote ndivyo inasema Katiba yetu ni kesi inayo draw Regional and International attention,” amedai Lissu.
Hata hivyo Lissu amedai mahakamani hapo kuwa tayari suala la wanachama wa chama hicho tarehe 24 Aprili kupigwa nje ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, limetua kwenye Mahakama ya Haki ya Umoja wa Mataifa “Haya yaliyofanyika Kisutu tayari yapo kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa yapo katika mahakama za haki za binadamu na watu Afrika.”
“Kwa hiyo haya sio mambo madogo kabisa. Mahakama inapoingiliwa inasababisha sintofahamu kwenye mfumo wetu wote wa haki jinai ndani ya Taifa letu,” amedai Lissu.
“Mwaka 1958 kulikuwa na kesi kubwa katika mahakama ya Wilaya Dar es Salaam Kivukoni ambayo ni Regina Vs Julius Nyerere na wenzake wawili mmoja wapo Robert na mwingine Rashid baldell,” amedai.
Lissu ameieleza mahakama hiyo kuwa hata mahakama za wakoloni hazikuwahi kuwazuia wananchi wasihudhurie kesi za viongozi wao “Wakoloni wa kingereza did not dare kuzuia watu kwenda kushuhudia kesi ya kiongozi wao na wanaofahamu historia ya nchi hii Mwalimu alitetewa na Wakili kutoka Uingereza. Wakoloni hawakukataza pia hawakupiga watu wasiingie mahakamani.
“Kesi ya Jommo Kenyata pia ilikuwa kubwa ambayo ilifanyika katikati ya Vita vya Maumau, Waingereza did not dare kuzuia watu kwenda kusikiliza the trial of Jomo Kenyata ilifuatiliwa.
“Mwaka 1956 mpaka 1961 tulikuwa na kesi ya Uhaini Afrika Kusini imeelezwa kwenye Long Walk to Freedom, Kesi ya Nelson Mandela hakuna mtu aliyepigwa wala kuzuiwa kwenda mahakamani, hakuna watu walioteswa ili wasiingie Mahakamani.
“Sasa nchi hii baada ya miaka 64 ya uhuru serikali yetu na vyombo vya Ulinzi na Usalama inazuia watu wasiingie Mahakamani kwenye nchi ambayo sheria zinasema mahakama ni ya wazi.
“Tunafanya mambo ya hovyo kuliko wazungu waliotutawala sisi hapa Tanganyika, walioitawala Kenya na wale wa Afrika Kusini sasa mimi niko Gerezani na Mahakama imeshindwa kufanya lolote.
“Sasa ili isije kuja kusemwa baada ya mimi na nyie majaji kutoweka hapa Duniani kuwa nilikuwa kwenye dhambi ya watu ambao walinyamaza kimya mambo haya kutokea. Nimesema kutimiza wajibu wangu na sitaki dhambi ya kunyamazia uovu au maovu, naomba kumalizia hapo,” amedai Lissu.
Baada ya maelezo hayo ya Lissu majaji waliruhusu shauri hilo kuendelea.
Lissu: Ni kweli au sio kweli hiyo video ya Tarehe 3 Aprili ilichapishwa kwenye Jambo Tv na mitandao mingine na walichapisha Jambo Tv wenyewe?
Kaaya: Aliyechapisha sifahamu.
Lissu: Ni kweli Mkutano wangu wa tarehe 3 Aprili ulirushwa mubashara na Jambo Tv?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Na ni kweli au sio kweli mimi sina uhusiano wowote na Jambo TV?
Kaaya: Mimi sikufanya upelelezi wa kuhusu wahusika wa Jambo TV ni akina nani.
Lissu: Ile Flash Disk ‘XIOXIA’ yenye rangi nyeupe unaikumbuka ulisema.
Kaaya: Ndio nakumbuka.
Lissu: Je uliandika aina hiyo ya Flash na rangi yake kwenye maelezo yako Polisi?
Kaaya: Sikuandika.
Lissu: Umezungumza sana kuhusu video na kuwaonyesha wakubwa zako na kuipakua na kuweka kwenye flash disk umezungumza sana sasa waeleze majaji kama umewasilisha hiyo flash disk au hiyo video mahakamani hapa.
Kaaya: Bado sijaiwasilisha.
Lissu: Ni sahihi nikisema hakuna mtu aliyeiona isipokuwa wewe hiyo video, majaji hawajaona, mawakili hawajaona na mimi sijaona?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu au hufahamu hiyo video vilevile haikuwasilishwa wala kuonyeshwa kwenye committal Kisutu?
Kaaya: Sifahamu.
Lissu: Sasa shahidi unakumbuka kwenye ushahidi wako ulieleza jinsi ulivyoona hiyi video na kutoa taarifa kwa mkuu wa kitengo?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Waeleze majaji kama kwenye maelezo yako polisi au hapa mahakamani ulimtaja huyo mkuu wako wa kitengo kwa jina?
Kaaya: Sikumtaja.
Lissu: Unakumbuka nilikuuliza maswali mengi juu ya kesi mbalimbali zilizofunguliwa na watu tofauti tofauti kuhusu masuala ya katiba na mabadiliko yake.
Kaaya: Nakumbuka.
Lissu: Waelelze majaji kama unafahamu au hufahamu kwamba tarehe 13 Juni 2023 Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Wananchi ilitoa uamuzi kwamba Serikali ya Tanzania ibadilishe sheria ya uchaguzi ili kuhakikisha sheria za uchaguzi zinakuwa za haki kwenye kesi ya Bob Chacha Wangwe.
Ni kesi ya Bob Chacha Wangwe akiwa na Legal and Human Right Center wakiwashitaki AG, Tume ya Uchaguzi.
Lissu: Sasa kuzuia uchaguzi ni uhaini mnasema hivyo kwenye ushahidi wako ulieleza kuzuia uchaguzi bila kufuata utaratibu wa kisheria kama vile kupata amri ya mahakama ni kuitisha serikali?
Kaaya: Nakumbuka.
Lissu: Utaratibu huo wa namna ya kuzuia uchaguzi upo katika sheria gani?
Kaaya: Sifahamu.
Lissu: Katiba unaifahamu shahidi?
Kaaya: Ndio naifahamu.
Lissu: Waeleze majaji kama upo utaratibu wa kuzuia uchaguzi mkuu?
Kaaya: Haupo. Haujaanishwa kwenye Katiba.
Lissu: Kwahiyo utaratibu haupo?
Kaaya: Zipo sheria zingine lakini.
Lissu: Hivi unaelewa swali langu au unatuchelewesha kwenda kwenye mazishi?
Kaaya: Haupo
Lissu: Je ni kweli uchaguzi mkuu wa Tanzania unaendeshwa na inayoitwa Tume Huru ya Uchaguzi?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Je ni kweli katiba inasema tume ni chombo huru na haitakiwi kuingiliwa na mamlaka au mtu yeyote?
Kaaya: Sikumbuki.
Lissu: Anamsomea katiba hapa ibara ya 74(11) – Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu masharti ya katiba hii , Tume ya uchaguzi haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya serikali au maoni ya chama chochote cha siasa . Kwamba tume haitakiwi kupokea maelekezo yoyote kutoka serikalini wala chombo chochote cha serikali.
Kaaya: Ni sahihi.
Lissu: Sasa waeleze majaji kuwa serikali haihusiki chochote na uchaguzi na uchaguzi uko chini ya Tume huru?
Kaaya: Hapo ni kweli serikali haihusiki ni tume ndio inahusika.
Lissu: Sasa naambiwa nilitengeneza nia ya kuhamasisha wananchi wazuie uchaguzi mkuu unalifahamu hilo?
Kaaya: Inategemea.
Lissu: Inategemea nini wewe polisi mimi nakwambia kuhusu mashitaka yangu. Hiyo hati umeisoma, unajua nashitakiwa na nini?
Kaaya: Mimi sijaisoma hiyo Hati ya Mashitaka.
Lissu: Kwahiyo hujui mashitaka yanasema nini, Kama hujaisoma huwezi kuijua.
Kaaya: Kimya.
Lissu: Haya umegoma kujibu. Mimi nakuacha tuendelee.
Lissu: Kwenye maneno ninayotuhumiwa nayo sijaitaja kabisa serikali?
Kaaya: Umeitaja kwa namna fulani hujataja kwa uwazi.
Lissu: Hiyo namna fulani ndio wamekufundisha akina Kingai ambao nao pia sio mawakili wamekudanganya umekalili na unakimbia na haya mambo ya uongo unaona unavoteseka hapa sasa nakusomea maneno yaliyopo kwenye hati ya mashitaka .
“Walisema msimamo huu unaashiria uasi ni kweli kwasababau tunasema tutazuia uchaguzi hii ndio namna ya kupata mabadiliko. Tutaenda kukinukisha sana. Hayo ndio maneno nashitakiwa nayo sasa katika hayo maneno kuna neno serikali?
Kaaya: Hapo neno Serikali lipo kwa maana ukitafsiri.
Lissu: Nakuuliza kuhusu maneno niliyosema mimi nimetaja serikali?
Kaaya: Kwenye maneno hujataja ila lipo.
Job Mrema: Anasema tuna pingamizi tunaona shahidi ameshajibu hili Swali.
Jaji: Hebu tuendelee sioni pingamizi hapo.
Lissu: Kwenye hayo maneno ninayosadikika kuyasema kama nimetaja Tume huru ya Uchaguzi?
Kaaya: Hujataja Tume Huru ya Uchaguzi.
Lissu: Hii habari ya kutishia serikali sasa ulisema umesoma Criminal Law? Ni kweli?
Kaaya: Ni kweli nimesoma Criminal Law.
Lissu: Je umesoma Penal Code? Kanuni ya adhabu umeisoma. Wewe si umesoma LL.B?
Kaaya: Nimesoma.
Lissu: Kifungu cha 39(2)(d) cha Penal Code sasa waeleze kwenye kifungu hicho neno kutishia kama limefafanuliwa?
Kaaya: Sikumbuki.
Lissu: Neno lililotumika ni intimidation. Je waeleze kama hilo neno limefafanuliwa? Nikupe sheria usome ili unataka kuropoka.
Kaaya: Sikumbuki.
Lissu: Nikikwambia hilo neno halijajatafsiriwa kokote kwenye Penal Code utasemaje?
Kaaya: Sikumbuki.
Lissu: Je kwenye hati ya mashitaka hilo neno kutishia serikali limefafanuliwa?
Kaaya: Sikumbuki.
Lissu: Hata kwenye hati ya mashitaka hicho kinachoitwa kutishia serikali halijafafanuliwa utasemaje?
Kaaya: Sina uhakika.
Lissu: Sasa naomba apatiwe maelezo yake exhibit D1 sasa tuyapitie shahidi na usinisumbue.
Lissu: Je maneno yafuatayo ni ya kihaini yapo kwenye ukurasa wa 2 wa maelezo yako. Umesema mambo ya majaji kuwa ma CCM na wanataka vyeo. Umeyaona hayo maneno?
Kaaya: Ndio nayaona.
Lissu: Sasa Je hayo maneno ni uhaini?
Kaaya: Hapana sio ya uhaini.
Lissu: Pia ulisema maneno mengine ambayo mimi nimeyasema kwamba nilisema wapinzani walienguliwa kwa amri ya Rais. Je hayo nayo ni Uhaini?
Kaaya: Inategemea. Wapelelezi wanajua.
Lissu: Nakuuliza wewe hayo ni uhaini? kama kuna mtu mwingine anajua wewe umekuja kufanya nini hapa?
Kaaya: Mimi ni mpelelezi lakini sijapeleleza hilo mimi.
Lissu: Na mimi nataka kuchaguliwa kwenye kacheo fulani na nyie mnataka kuchaguliwa pia sasa mnafikiri tunafanyaje kwa mazingira haya. Je hayo pia ni uhaini.
Kaaya: Sasa hadi nichunguze ndio nitajua.
Lissu: Ulichunguza?
Kaaya: Mimi sio Mpelelezi. Sikuchunguza hili.
Lissu: Unajua Uchaguzi wa Serikali za mitaa unaendeshwa na TAMISEMI?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Ni kweli kwamba uchaguzi huo unaendeshwa kwa kanuni za uchaguzi huo zinazotungwa na Waziri?
Kaaya: Sifanyi kazi huko kwahiyo sifahamu.
Lissu: Huyo Waziri ni mteule wa Rais?
Kaaya: Mimi sijui.
Lissu: Kwahiyo wewe hufahamu mtu anayeteua mawaziri nchi hii wewe humfahamu?
Kaaya: Mawaziri wanateuliwa na Rais.
Lissu: Kwahiyo Mohamed Mchengerwa ni mteule wa Rais Samia. Huyo ni Waziri wa TAMISEMI?
Kaaya: Ni kweli.
Lissu: Je ni kweli au sio kweli ni Waziri ambae anatoa tangazo la uchaguzi na ratiba yake ya huo uchaguzi wa serikali za mitaa?
Kaaya: Sina Uhakika.
Lissu: Ni kweli au sio kweli wasimamizi wakuu wa uchaguzi huo ambao ni returning officer ni wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali?
Kaaya: Sijui.
Lissu: Ni kweli au sio kweli wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya ni wateule wa Rais?
Kaaya: Sifahamu.
Lissu: Askari polisi mwenye cheo cha Inspector hafahamu wakurugenzi wanateuliwa na nani?
Lissu: Ni kweli kwamba watumishi wote wa serikali za mitaa wanaohusika na uchaguzi wa serikali za mitaa wanafanya kazi kwa niaba ya Rais au maelekezo ya Rais?
Kaaya: Sina uhakika.
Lissu: Ni kweli uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 kwa maelfu walienguliwa na kuzuiwa kugombea?
Kaaya: Sina uhakika.
Lissu: Ni kweli au si kweli baada ya kuenguliwa kelele ikawa kubwa hadi Dk. Nchimbi Katibu Mkuu wa CCM alielekeza warudishwe?
Kaaya: Sina Uhakika.
Lissu: Ni kweli baada ya kelele zote hizo Waziri wa Tamisemi Mchengerwa aliomba muda uongezwe na kubadili ratiba ya Uchaguzi?
Renatus Mkude: Mheshimiwa Jaji imefika saa tano kamili naomba turuhusiwe kwenda msibani na tutafikisha salamu za rambirambi pia za mshitakiwa.
Jaji Ndunguru: Shahidi tukutane kesho saa tatu asubuhi. Tunaahirisha shauri hili.
ZINAZOFANANA
Raila Odinga afariki dunia
OMO aahidi kupitia upya mfumo wa mafao ya wastaafu serikalini
TEC yaukana waraka wa uchaguzi