October 12, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Ilala wafanya dua kumuombea Samia, Tanzania

 

ZIKIWA zimesalia takribani wiki mbili kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu, baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu ambao ni wakazi wa Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, wamefanya dua maalumu ya kuliombea taifa amani na utulivu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Pia wamemuombea Rais Samia Suluhu Hassan, afya jema, busara na hekima ili alivushe taifa katika uchaguzi huo ambao ni wa saba tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe mwaka 1992.

Dua hiyo ilifanyika jana Jumamosi, tarehe 11 Oktoba, nyumbani kwa Issa Kivina (Mr Cap) ambapo mgombea ubunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu, alihudhuria na kuwasihi wananchi wajiepushe na vurugu kwenye kampeni zinazoendelea na katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 29 Oktoba mwaka huu.

Zungu amewataka wananchi kupuuza kauli za watu wanaotaka kuchochea vurugu ili uchaguzi uvurugike au usifanyike kama ratiba inavyopangwa.

“Dk. Samia alishasema hali ya utulivu ipo na itaendelea kuwepo. Vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kulinda amani hiyo, hivyo Watanzania mjitokeze kwa wingi Oktoba 29 mkapige kura kwa Dk. Samia, wabunge na madiwani wote wa CCM kote nchini,” alisema Zungu.

Zungu alisisitiza kuwa amani ni nguzo muhimu ya maendeleo, hivyo wananchi hawapaswi kuruhusu watu wachache kuvuruga utulivu uliopo kwa misingi ya kisiasa.

Kwa upande wake, Kivina aliyeratibu dua hiyo, alisema wamemuomba Mwenyezi Mungu amuepushe Rais Samia na mabalaa pamoja na watu wasio na nia njema kwa taifa wenye lengo la kuvuruga amani na utulivu uliopo.

“Dua hii siyo ya kisiasa bali ni ya kiimani. Tumeomba Mungu amlinde Mama Samia, ampe afya njema, busara. Tumemkabidhi mikononi mwa Mungu kwa imani kwamba Tanzania itaendelea kuwa na amani chini ya uongozi wake,” alisema Cape.

Akionyesha ishara ya mapenzi na heshima yake kwa Rais Samia, Mr Cape alichinja ngamia ikiwa ni sadaka maalumu, akisema kitendo hicho kinaashiria upendo, utiifu na imani yake kubwa kwa kiongozi huyo aliyeonyesha uongozi wa hekima na huruma kwa Watanzania wote.

“Ngamia huyu nimemtoa kama sadaka yangu binafsi kwa ajili ya dua hii. Ni alama ya mapenzi na shukrani zangu kwa Mama Samia ambaye ametuletea matumaini mapya. Mungu amzidishie baraka na amani katika kila hatua,” alisema.

Naye Mwanahawa Juma, mkazi wa Ilala Boma, alitoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi.

“Sio kwamba Mama hashindi, hapana. Tunahitaji kura nyingi zaidi. Hivyo wamama tuamke mapema Oktoba 29 tukapige tiki tatu za maana,” alisema kwa tabasamu.

About The Author

error: Content is protected !!