
MAKAMU mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche, amemtembelea mwanasiasa mkongwe nchini, Mabere Marando. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Akiwa nyumbani kwa Marando, makamu huyo mwenyekiti, alimhakishia mwanasiasa huyo, kuwa bado Chadema kiko imara na ana uhakika wa kushinda mapambano inayopitia.
“Tuko vizuri na tutashinda mapambano haya,” alisema Heche na kuongeza, “Tumekumisi sana Mzee Marando na tunazidi kukuombea.”
Mabere Nyaucho Marando, ni mmoja wa waasisi wa mageuzi nchini. Amewahi kuwa mwenyekiti wa kwanza wa NCCR- Mageuzi na katibu mkuu wa chama hicho.
Kutokana na kuyumbishwa kwa NCCR-Mageuzi, kulikochangiwa na mgogoro uliofukuta kati ya Mrema na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, Marando aliondoka kwenye chama alichokiasisi na kujiunga na Chadema.
Akiwa Chadema, aliweza kushika nafasi mbalimbali, ikiwamo Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani; Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na wakili mwandamizi wa chama hicho.
Katika mazungumzo yake na makamu mwenyekiti Heche, Marando amesema, pamoja na kwamba hajashiriki siasa za majukwaani, lakini anafuatilia yanayojiri nchini na kumtaka kiongozi huyo, kutosaliti mageuzi aliyoanzisha yeye na wenzake.
Aidha, mbunge huyo wa zamani wa Rorya, mkoani Mara, alitumia ziara ya Heche, kumtakia kheri mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini, akisema hana mashaka kuwa Lissu atavuka kihunzi hicho.
“Nawatakia kila la kheri na nashukuru kwa kuja kuniona,” ameeleza Marando, katika mazungumzo yake na Heche.
Katika ziara hiyo, Heche aliambatana na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia na Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Ntele Benjamin.
ZINAZOFANANA
Mgombea udiwani Kinyerezi ajinadi kuwa mtu wa vitendo zaidi
Lissu aanza kumbana shahidi wa pili, ataendelea J’tatu
Uhamiaji yawang’ang’ania wageni wa Lissu