October 9, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Maswali ya majibu ya shahidi wa pili wa kesi ya Lissu

Tundu Lissu akiwa mahakamani

 

MAHAKAMA Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam, imeendelea na usikilizaji wa shauri Na. 19605/2025 ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambapo leo shahidi wa pili ofisa wa polisi Insepekta John Kaaya (45) ambaye anafanya kazi kwenye dawati la doria ya mtandaoni ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Leo tarehe 9 Oktoba 2025, Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema mbele ya jopo la majaji watatu walioongozwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Jaji Dunstan Ndunguru, akishirikiana na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde, ameanza kumuongoza shahidi huyo.

Mrema: Ufahamu kuna amri ya mahakama kuu iliotolewa ya kulinda mashahidi haitakiwi kutaja majina ya baadhi ya mashahidi pia uongee kwa sauti.

Mrema: Eleza mahakama hii umeajiriwa lini?

Kaaya: Nimeajiriwa 2006 baada ya kuhitimu mafunzo ya ukuruta nilioanza mwezi Agosti 2005 na kuhitimu Februari 2006

Mrema: Eleza mahakama mafunzo ulipata wapi?

Kaaya: Nilipata chuo cha polisi Zanzibar.

Mrema: Eleza katika mafunzo hayo ulijifunza nini?

Kaaya: Nilijifunza mbinu mbalimbali za kivita, sheria mbalimbal mathalani sheria ya ushahidi, criminal procedure, kazi za polisi, investigation skills na First aid.

Mrema: Baada ya kumaliza mafunzo haya ulipata nini?

Kaaya: Nilitunukiwa certificate of competence.

Mrema: Baada ya kumaliza mafunzo hayo ilikuwaje?

Kaaya: Nilipangwa makao makuu ofisi ya upelelezi.

Mrema: Unaposema makao makuu unamanisha nini?

Kaaya: Makao makuu ya polisi Mkurugenzi wa upelelezi.

Mrema: Ilipofika 2020 ilitokea nini?

Kaaya: Nilihamishiwa kitengo cha Cybercrime( uhalifu wa mtandaoni), dawati la doria mtandaoni.

Mrema: Eleza mahakama hii ulikuwa unafanya nini?

Kaaya: Kupeleleza makosa ya jinai, kukamata watuhumiwa, kufikisha watuhumiwa mahakamani pamoja na kutoa ushahidi.

Mrema: Shahidi unaeleza Mahakama ulihamishwa kwenye kitengo cha makosa ya mtandao hebu eleza kiko chini ya nani?

Kaaya: Kitengo cha dawati la doria mtandaon kiko chini ya DCI

Mrema: Eleza ofisi ya DCI ilikuwa wapi?

Kaaya: Kwanzia mwaka 2006 ofisi ya DCI ilikuwa jengo la Polisi Makao Makuu Dar baadae Serikali kuhamia Dodoma na ofisi zikahamia huko.

Mrema: Wewe kwa sasa majukumu yako unatekeleza ukiwa wapi?

Kaaya: Ililokuwa polisi Makao Makuu Dar es Salaam.

Mrema: Shahidi umejitambulisha kama inspekta John kaaya eleza cheo hicho ulikipata lini?

Kaaya: Cheo hicho nilipewa mwaka 2025 mwezi wa 6, nilipewa kutokana na utendaji kazi mzuri kazini.

Mrema: Nani alikupa hicho cheo?

Kaaya: Nilipatiwa na Jeshi la polisi muajiri wangu.

Mrema: Mbali na Mafunzo nje ya Kipolisi yapo mengine?

Kaaya: Nimejifunza pia Forensic Cyber Crime in Modern Investigation niliyapatia Chuo cha Polisi Dar es salaam.Pia nimeweza kujifunza Cyber Crime Management, digital forensic, Basic Computer Skills in Cyber Crime Investigation, pamoja na Cyber Ivestigation Skills. Haya yote nilihitimu 2020 na nikapata Cheti.

Mrema: Je kuna mafunzo mengine mbali na hayo?

Kaaya: Ndio, Sisco Certified Support Technician in Cyber Security. Mafunzo haya nilisoma chuo cha JR institute of Information Technology kilichopo Kisutu Dar es salaam na ilikuwa mwaka 2024.

Mrema: Mambo muhimu uliyojifunza kupitia course hiyo?

Kaaya: Ulinzi wa Data nilijifunza, Networking, Computer hacking aahhh sio hiyo ni Ethical Hacking. Mafunzo ni ya miezi mitatu yalikuwa na haya yalikuwa mwaka 2024 ambapo nilipata cheti pamoja na ujuzi pia.

Mrema: Je kuna mafunzo mengine tena?

Kaaya: Pia nilisoma Computer Hacking Forensic Investigation. (CHFI) Nilijipatia katika mafunzo ya Unique Academy pale Upanga Dar es salaam na yalikuwa ni mafunzo ya miezi miwili. Mambo niliyojifunza ni upelelezi wa kisayansi katika mifumo mbalimbali ya Computer.

Mrema: Ulisema unafanya kazi wapi hivi?

Kaaya: Kitengo cha upelelezi wa makosa ya mtandao ‘online patrol desk’ na sasa majukumu yangu ni kufanya doria katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Mrema: Doria mtandaoni ni nini?

Kaaya: Ni kwamba tunaperuzi mitandaoni kwa ajili ya kung’amua makosa mbalimbali ya kijinai yanayofanywa na watumiaji wa mitandao hiyo na mitandao yenyewe ni instagram, tiktok, X na kadhalika.

Mrema: Hiyo Doria inafanyikaje?

Kaaya: Doria tunafanya kwa kuperuzi katika mitandao hiyo niliyosema baada ya kung’amua kama kuna kosa la jinai nawasilisha kwa wakubwa wangu kama kuna kosa basi hatua stahiki zinachukuliwa.

Mrema: Mitandao inatumikaje na watu?

Kaaya: Ni lazima wawe na account yaani kujisajili kuweka taarifa zako katika uwanja wa mtandao husika na ukishaandika basi taarifa hizo zitaonekana kwa watumiaji wengine wa mitandao hiyo.

Mrema: Unaposema taarifa unamaanisha nini?

Kaaya: Namaanisha Username binafsi na jina utakalotaka wajue watumiaji wengine, Password na email address.

Mrema: Je unajua utaratibu wa kusajili mtandao wa YouTube?

Kaaya: Ndio mtumiaji unapaswa kuwa umeandaa taarifa zako binafsi kama Username, email address pamoja na passwords utakayoitumia baada ya hapo utaingia uwanja wa YouTube na kuandika taarifa hizo kadri zitakavyokuwa zinahitajika. Ukishakamilisha watakupa terms and condition na baadae watakupa channel URL.

Mrema: Hiyo Channel URL ni nini?

Kaaya: Yaani uniform resource locater ni unique ID yaani utambuzi wako binafsi ambayo inakuwezesha kuendelea kutumia mtandao huo wa YOUTUBE ama hiyo Account yako.

Mrema: Hiyo unique ID unamanisha nini?

Kaaya: Maana yake ni utambuzi wa mtumiaji wa mtandao wa YOUTUBE ambao haufanani na mtu mwingine.

Mrema: Ili mtu aingie anapaswa kufanya nini kwenye huo mtandao?

Kaaya: Utaingia kwenye ukurasa wa YouTube kwa kutumia username yako na password uliyokwisha umeandaa baada ya hapo utakuwa unaweza kuona maudhui mbalimbali yaliyochapishwa na watumiaji mbalimbali wa mtandao huo.

“lingine muhimu kuhusu mtandao wa YOUTUBE unaweza kuweka maudhui na baadae ukafuta na unaweza kutumia kuona maudhui ya watu wengine waliyoyaweka”.

Mrema: Live stream ni nini shahidi nasikia uliitaja?

Kaaya: Live streaming ni kitendo cha kurusha ama kuchapisha tukio katika mtandao wakati tukio hilo likiwa linatendeka moja kwa moja.

Mrema: Huwa unafanya maandalizi gani unapoingia kazini kabla hujafanya majukumu yako?

Kaaya: Huwa ninaandaa vitendea kazi vyangu ambavyo ni Computer maalumu ya jeshi la polisi, police notebook na Internet access. Kingine huwa naandaa umeme ni muhimu nihakikishe umeme upo.

Mrema: Taratibu binafsi zingine ni zipi huwa mnachukua?

Kaaya: Huwa nahakikisha chumba kinakuwa salama kwa maana mtu ambae hahusiki asiingie.

Mrema: Baada ya kuandaa hivyo vyote huwa unafanya nini?

Kaaya: Nawasha Kompyuta kwa kutumia username yangu binafsi na password na baada ya kuingia nafanya ukaguzi wa Kompyuta kama inafanya kazi na pia natumia anti virus ku scan kama virus wapo na pia nakagua Internet access ili kuniwezesha kufanya kazi.

Mrema: Je, hiyo Computer unayizungumza ni ya namna gani na ina vitu gan?

Kaaya: Hii ni software na ina program maalumu zinazotuwezesha kufanya doria mtandaoni.

Mrema: Hizo programu maalumu zinaweza kufanya mambo gani?

Kaaya: Zinatusaidia kwa ajili ya ku monitor mitandao mbalimbali niliyoitaja. Zinatuwezesha kupakua maudhui yenye ujinai. Doria mtandaoni huwa tunafanya kwa muda wa saa 24 za siku na pale katika dawati tunaingia kwa zamu.

Mrema: Shahidi tuambie tarehe 4 Aprili 2025 ulikuwa shift zamu gani gani?

Kaaya: Majira ya saa 12 asubuhi nilikuwa zamu kazini.

Mrema: Ieleze Mahakama tarehe hiyo jambo gani lilitokea kuhusu hii kesi?

Kaaya: Waheshimiwa majaji mnamo tarehe 4 Aprili 2025, niliingia zamu saa 12 asubuhi baada ya kufika ofisini niliandaa vitendea kazi vyangu kama kawaida.

Kaaya: Niliweza kuwasha Kompyuta mali ya jeshi la Polisi kwa kutumia username na password baada ya kuwaka nikaweza kuikagua na kugundua iko katika hali nzuri ya kufanya kazi.

Mrema: Ukawa unafanya nini?

Kaaya: Nikawa naperuzi na niliingia YouTube. Nilivyoingia YouTube nilibaini machapisho mbalimbali ya video. Mojawapo ya Chapisho ni katika ukurasa uliosajiliwa kwa majina ya JAMBO TV na niliona picha iliyokuwa imeambatana na maneno ‘Tundu Lissu uso kwa uso na watia nia majimboni . No reforms No election njia panda’.

“Baada ya kuona picha mjongeo hiyo niliweza kuchezesha picha mjongeo hiyo ili niweze kuona maudhui yaliyochapishwa”

Mrema: Lengo la kuchezesha lilikuwa ni nini?

Kaaya: Ili nione maudhui yaliyopo humo ni nini?

Mrema: Sasa ili iweje ukishaona hayo maudhui?

Kaaya: Lengo ni kubaini kilichozungumzwa.

Mrema: Kwanini uliingia sasa?

Kaaya: Nilishangaa kuona video ile ina watazamaji wengi elfu na 39 nikaona ngoja na mimi niingie kuona kuna nini na watazamaji 300 niliona wamecomment.

Mrema: Sasa shahidi unaweza kueleza mahakama majukumu yako ni yapi?

Kaaya: Majukumu yangu ni kuperuzi kwenye mitandao ya kijamii kubaini makosa yanayofanywa.

Mrema: Sasa ieleze mahakama hiyo sjju ya tarehe 4 Aprili uliingia kule kufanya nini?

Wakati huo huo Lissu amesimama na kudai kuwa swali hilo lilishajibiwa alisema aliingia kuwa video ile ilikuwa imetizamwa na watu wengi na waliocomment nikashawishika ni maudhui gani yamechapishwa humo.

Mrema: Baada ya kuingia ulibaini nini humo ndani shahidi?

Kaaya: Niliweza kubaini baadhi ya matamshi yenye viashiria vya jinai.

Mrema: Viashiria hivyo ni vipi?

Kaaya: Aliposema kuwa kwa kuwa hatuna access na hizo server za tume na mapolisi ndo hao mnawaona na vibegi vya kura feki.

Mrema: Haya mambo ya vibegi feki yalishakataliwa na mahakama siku ya juzi hauwezi kuletwa leo tena unahusiana na kesi iliyopo kisutu.

Wakati huo huo Mrema akawasilisha pingamizi dhidi ya pingamizi la Lissu kuhusu kuzungumza suala la polisi kubeba vibegi vya kura kwenye kesi ya uhaini

Mrema ameitaja kesi ya Mukisa Biscuits inayoeleza kuwa pingamizi lazima liwe na sheria iliyotajwa.

Naye Lissu akijibu hoja hizo akadai kuwa tayari mahakama imeshasonga mbele tangu shahidi wa kwanza alitoa ushahidi wake (ASP George Bagyemu).

“Nafikiri Mrema alikuwa anaongea jambo ambalo halifahamu.Unaleta kesi ya Mukisa ambayo yenyewe inahusu mapingamizi ya mamlaka ya mahakama,” alidai Lissu.

Akitoa uamuzi mdogo kwenye shauri hilo Jaji Kiwonde amesema kuwa tayari mahakama hiyo ilishaamua kwa shahidi wa awali
“Shahidi alisema habari za vibegi vya kura feki na mshitakiwa alipinga hapa. Baada ya sisi kutafakari swali la msingi tulijiuliza kama mahakama hii ilishatoa amri ya kuzuia maudhui yaliyoonwa yasitolewe ushahidi. Mahakama siku ya Jumatatu ilisema masuala yanayohusu vibegi vya polisi na utendaji kazi wa mahakama ya Tanzania. Hicho ndio tulichokizuia siku ya Jumatatu,” alisema Jaji Kiwonde

Jaji Kiwonde, alimruhusu shahidi huyo kuendelea na ushahidi wake

Mrema: Sasa shahidi endelea

Kaaya: Lissu alisema hawa mapolisi mnawaona wana vibegi vya kura

Maneno mengine alisema kwa kuwa majaji nao ni watu wa Rais na wao ni MACCM. Wanataka wapandishwe vyeo kwenda kwenye mahakama za rufani kuteuliwa kwenye commissions na kwenye tume ndiko kuna hela. Hayo maneno niliona akisema mshitakiwa. Akaeleza tena kwahiyo mahakamani hakuendeki.

Kaaya: Maneno mengine lissu alisema “mkutano wetu unasema No Reforms No Election, Wamesema Kitu kimoja sahihi hapa kwamba tunapanga kufanya uasi, ni kweli tunaashiria uasi.Tutakinukisha vibaya sana, tutakinukisha sana sana.

Mrema: Ulivyomaliza kusikiliza Video ulibaini nini?

Kaaya: Nilibaini matamshi yale yana viashiria vya jinai.

Mrema: Shida gani?

Kaaya: Maneno yavibegi niliona yanapotosha umma.

Jaji Kiwonde: Sasa mnaona huko mnaanza kuelekea tena kwenye vibegi.

Lissu: Mheshimiwa jaji huu ushahidi aachwe aendelee kuutoa tu maana nilipinga mkasema ni sahihi aendelee sasa nafikiri asikatazwe acha aseme tu.

Jaji Ndunguru: Basi aendelee hakuna shida.

Mrema: Ieleze Mahakama Shahidi ulikuwa unaelezea viashiria vya makosa kwenye maneno hayo.

Kaaya: Waheshimiwa Majaji pamoja na hayo matamshi niliyosema, pale aliposema kuwa mahakamani hakuendeki kwasababu majaji ni watu wa rais na ni MaCCM niliona taarifa hiyo ina viashiria vya jinai.

“Shahidi kusema kanuni za utumishi wa umma zinakataa watumishi kuwa wafuasi wa vyama vya siasa”.

Kaaya: Pia aliposema mahakamani hakuendeki ila mahakama ni chombo cha kutoa haki na kutoa maamuzi ya mambo mbalimbali yanayobishaniwa. Hivyo anavyojulisha umma kwamba hakuendeki ni kutoa taarifa ya uongo kwa umma na kuitishia serikali .

Mrema: Baada ya kuitizama hiyo video nini kingine ulikisikia.

Kaaya: Lissu alisema Tutaenda kuzuia uchaguzi, tutazuia uchaguzi kwasababu wanasema tunahamasisha uasi na tutaenda kuuvuruga sana sana. Kwa matamshi hayo niliyosema waheshimiwa majaji niliona kuna viashiria vya jinai.

“Uchaguzi huandaliwa kwa mujibu wa katiba na sheria hivyo kuzuia uchaguzi kwa kuhamasisha uasi bila kufuata utaratibu ni kosa.

“Haya yote aliyafanya lengo lake ni kuitisha serikali ambayo ndio msimamizi mkuu wa Sheria na kulinda amani,”alidai Kaaya.

Kaaya: Baada ya kuona hayo maudhui nilichukua Police notebook yangu na ku note maudhui hayo niliyosema na nilinote link ambayo hayo maudhui yanahusika. Hapa namaanisha ni ukurasa wa Jambo TV pamoja na mtoa maudhui Lissu.

Mrema: Kila muda unasema Tundu Lissu unamfahamu yuko wapi?

Kaaya: Anasema namfahamu na yupo hapa mahakamani.

Mrema: Yuko wapi?

Kaaya: Yule pale (anaashiria kwa kuonesha kwa mkono kizimbani aliko Lissu).

Kaaya: Baada ya kuona hayo nilimjulisha mkuu wangu wa kazi ambae ni mkuu wa kitengo cha doria mtandaoni.

Mrema: Hiki kitengo kipo ofisi gani?

Kaaya: Kipo ofisi ya DCI (Mkuu wa Upelelezi wa makossa ya jinai).

Mrema: Hiyo picha mjongeo alimaliza kuitizama muda gani?

Kaaya: Nilimaliza kuitazama kwenye majira ya saa nne asubuhi siku ya tarehe 4, Aprili 2025.

Mrema: Taarifa kwa mkuu wako wa kazi ulitoa saa ngapi?

Kaaya: Nilipomaliza kuitizama ndio nilitoa taarifa kwa mkuu wangu wa kazi.

Mrema: Ulivyotoa taarifa ulipata matokeo gani?

Kaaya: Nilielekezwa kwenda polisi kanda maalumu Dar es salaam kwa ajili ya kwenda kumjulisha Afande SSP George, Juu ya maudhui yale.

Mrema: Utekelezaji wa majukumu yako ikawaje?

Kaaya: Nilisimama kutekeleza majukumu mengine nilienda kuonana na Afande George ambae kwa siku ile alikuwa ni Naibu Kamanda wa Upelelezi Kanda ya Dar es salaam na ilikuwa siku hiyo hiyo ya Tarehe 4 Aprili 2025.

Mrema: Ikawaje?

Kaaya: Nilivyofika nikamkuta Afande George na kumjulisha dhumuni la ujio wangu kwake.Nilimwambia nimeelekezwa na mkuu wa kitengo cha makosa ya mtandao kuwa nije kukupa taarifa ya nilichokiona huko mtandaoani.

Baada ya kumjulisha alinielekeza, nimuonyeshe picha mjongeo zile na nilimuonyesha kupitia simu janja yake kwa kuingia kwenye ukurasa wa Jambo TV.

Mrema: Ikawaje tena?

Kaaya: Basi nilichezesha picha mjongea ile kwa kumuonyesha baadhi ya vipande nilivyobaini vina viashiria vya jinai.

Hapa nazungumzia ile video ya tundu lissu uso kwa uso na watia nia majimboni No Reforms, No Election.

Mrema: Nini kikafuata?

Kaaya: Afande George alichukua police notebook yake na kujaza taarifa kuhusiana na picha mjongeo ile na baada ya kuchukua baadhi ya taarifa muhimu, aliniamuru kurudi eneo langu la kazi kuendelea na majukumu mengine.

Mrema: Tarehe 7 Aprili 2025 nini kilitokea?

Kaaya: Nakumbuka nilikuwa zamu kazini. Wakati naendelea na majukumu ya kila siku. Alinipigia afande SSP George majira ya asubuhi akinielekeza niende ofisini kwake.

Mrema:  Ulivyofika ofisini ikawaje?

Kaaya: Alinikumbusha kuhusu ile taarifa niliyompelekea aliniamuru nirudi ofisini ninapofanyia kazi za doria mtandaoni na kupakua video ile katika ukurasa wa Jambo TV niipakue na baadae nimpelekee. Nilivyopokea amri ile nilirudi ofisini kuifanyia kazi.

Nilipofika ofisini niliandaa vitendea kazi vyangu kama vile computer na notebook. Nilikagua utendaji kazi wa computer yangu na nilichukua police notebook yangu na kuchukua ile link na kuinakili kwenye program maalumu kwa ajili ya kupakua yale maudhui.

Mrema: Halafu ikawaje?

Kaaya: Niliandaa Flash mpya aina ya XIOXIA yenye ukubwa wa GB 8 niliiweka kwenye computer na kuifanyia virus scanning na baadae nikaifanyia formating ili kuondoa data yoyote iliyomo mle kwenye flash. Ndipo nikaichukua ile video na kuihifadhi katika flash hiyo.

Mrema: Wakati unaipakua hiyo video ilikuwa na muonekano gani?

Kaaya: Ilikuwa na watazamaji elfu 52 na waliocomment mia tatu.Kingine nilibaini ile video ilichapishwa tarehe 3 Aprili 2025, kwenye ukurasa wa Jambo TV.

Mrema: Kuhusu maudhui yake ulifanya nini?

Kaaya: Niliweza kuisecure flash ile kwa ku encrypt na password (kuilinda). Nilichukua pia PF 145 ambayo ni Exhibit label na niliilabel kile kielelezo na kukipa alama DM.

Mrema: Baada ya kufanya labelling uliendelea na hatua gani nyingine?

Kaaya: Niliondoka ofisini na kuonana na afande ASP GEORGE na kwamba nimeshapakua na kuyahifadhi. Hiyo ilikuwa ni tarehe 07 Aprili majira ya saa 9 mchana baada ya kufika ofisini kwa George nilionana nae na kumjulisha kwamba maelezo aliyonipa nimekamilisha.

Baada ya kumjulisha afande George alichukua diary yake na kunijulisha kuwa ameshafungua kesi ambayo ina Reference No. DSMZ/CID/PE.101/2025

Pia aliniambia niorodheshe hiyo kesi namba kwenye kile kielelezo ambacho niko nacho yaani flash aliniambia niandike maelezo yangu nimpatie.

Mrema: Nini kikafuata?

Kaaya: Aliniambia nikipeleke kielelezo kwa ACP Malugala mtunza vielelezo. Nilijaza namba ya jalada kwenye kielelezo. Nilichukua kielelezo DM na kukipelekea kwa ACP Malugala.

Mrema: Tarehe. 8 Aprili 4 kilitokea nini sasa?

Kaaya: Nilikuwa zamu kazini na nikiwa naendelea na majukumu yangu. Alinipigia afande ASP George akiniamuru niende Ofisini kwake, nilisitisha shughuli zangu na kwenda kuonana na Afande George.

Mrema: Nini kiliendeleaa ulipofika?

Kaaya: Nilimkuta yupo na Mpelelezi. Alinikumbusha kuhusu tukio la Tarehe 7 Aprili 2025 kuhusu uwasilishaji wa kielelezo kwake. Aliniambia nimpatie yule mpelelezi password katika kielelezo DM.

Nilichukua Police notebook yangu kwa ajili ya kujikumbusha password yangu na kuinakili kwenye notebook ya mpelelezi niliyoamuriwa nimpatie.

Mrema: Je hiyo video ya tarehe 4 Aprili 2025, utaitambuaje ukiiona?

Kaaya: Hiyo video naweza kuitambua kwa maudhui yanayotamkwa, mzungumzaji amevaa kombati ya Kaki, nyuma ya mzungumzaji kuna rangi za Bendera ya Taifa pia itakuwa kwenye flash disk.

Mrema: Kwani Maudhui yaliyokuwepo kwenye hiyo video ni yapi?

Mrema: Hiyo Flash utaitambuaje pia?

Kaaya: Nitaitambua ina GB 8 na ina rangi nyeupe.

Mrema: Waheshimiwa Majaji ni hayo tu kwa shahidi huyu.

Shahidi huyo amehitimisha kuwasilisha ushahidi wake ambapo majaji wanamuuliza Lissu kama analolote la kusema.

Lissu: Mheshimiwa Jaji huyu shahidi asiende hivi hivi naomba mnipatie nusu saa nianze nae leo leo au hata kama mkiniruhusu niendelee nae hadi saa mbili usiku niko tayari.

“Jambo lingine off record jana niliwaahidi nitawaleteeni kitabu nilichoandika miaka mitano iliyopita kinaitwa “Remaining in the Shadow” kuhusu mambo ya Uchaguzi,” alidai Lissu.

Nimebeba copy tatu (nakala tatu) hapa naomba niwape na Mawakili wa Serikali nakala moja nao wakasome ili wajue mambo mengi wasidhani mimi ni mtu wa mchezo mchezo na waache kutumika tu.

Majaji pia nawapatieni nakala moja.

Jaji Ndunguru: Sasa unatupatia nakala moja tunasomaje si bora ungetoa nakala mbili?

Lissu: Waheshimiwa majaji nikiwapa mbili mtagombana sana maana mko watatu.

Watu wanacheka.

Jaji Ndunguru: Sasa wewe ugomvi wetu haukuhusu, tupe hizo nakala mbili sisi tutajua cha kufanya.

Lissu: Basi nyie vijana anawanyooshea Wakili Paul Kisabo na Deodatus Mahinyila kuwa hakikisheni kesho mnaongeza nakala zingine nne zije hapa.

Wakati huo huo Jaji Nduguru akaahirisha shauri hilo na kueleza kuwa litaendelea kesho tarehe 9 Oktoba 2025 saa tatu asubuhi. .

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online, MwanaHALISI Digital kwa taarifa kuhusu mwenendo wa kesi hii.

About The Author

error: Content is protected !!