October 8, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Yaliyojiri mahakamani kesi ya Lissu neno kwa neno

 

TUNDU Lissu – Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo tarehe 8 Oktoba 2025 akiwa anamuuliza maswali ya Dodoso shahidi wa awali wa ambaye ni ASP George Bagyemu – Naibu Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Kama ifuatavyo:-

Lissu: shahidi kuna mambo nataka tumalize haraka haraka katika maelezo yako ya juzi ulisema ulishika madaraka pia ndani ya hii miaka yako 22 ya upolisi ulikuwa Deputy RCO wa Rufiji 2008.

Bagyemu: Ni kweli kabisa.

Lissu: Ulikuwa Rufiji lini?

Bagyemu: Nilikuwa kuanzia tarehe 01 julai 2018 hadi Tarehe. 17 julai 2019.

Lissu: waeleze majaji kama Rufiji ni mkoa wa kipolisi au wilaya ya kipolisi?

Bagyemu: Rufiji ni Mkoa wa kipolisi wenye wilaya nne.

Lissu: Ni nani alikuwa RPC wako?

Bagyemu: SACP Onesmo Lyanga.

Lissu: Nani alikuwa RCO?

Bagyemu: Alikuwa anaitwa ACP Faustine Mafwele na mwingine SSP Richard Mchomvu.

Lissu: Mafwele huyu huyu?

Bagyemu: Kimya

Lissu: Nilikwambia jana uwe unajibu maswali yangu usiwe na kiherehere.

Lissu: Je kipindi kile ukiwa Deputy RCO mkuranga, kibiti, kulikuwa na mauaji mengi?

Bagyemu: Ni kipindi hicho hicho kweli nilikuwa Deputy RCO.

Lissu: Je unakumbuka idadi ya waliouawa?

Bagyemu: Sikumbuki idadi yao.

Lissu: Je unaweza kueleza sababu ya mauaji hayo mengi?

Bagyemu: Kulikuwa na makosa mengi ya kigaidi ndo maana yalikuwepo.

Lissu: Na wewe ulikuwa Deputy RCO na hujui idadi ya watu wengi waliokufa?

Bagyemu: Ungenipa muda ningekuja na idadi hiyo halisi.

Lissu: Wakati unaoneshwa ile video ulikuwa na police notebook?

Bagyemu: Yes nilikuwa nayo na hiyo notebook niliitumia kurekodi yale muhimu.

Lissu: Naomba ueleze kama uliwasilisha hiyo Police notebook?

Bagyemu: Sikuiwasilisha.

Lissu: Ulizungumza kwa kiasi kidogo juu ya mashahidi waliopatiwa ulinzi wa mahakama?

Bagyemu: Ndio ni sahihi.

Lissu: Waeleze majaji kama ulihusika kuwahoji hao mashahidi wa siri?

Bagyemu: Sikuhusika kabisa kuwahoji.

Lissu: Ieleze Mahakama kama unawafahamu hao mashahidi wa siri?

Bagyemu: Siwafahamu kwa majina.

Lissu: Waeleze majaji kama uliona maombi yaliyopelekwa mahakama kuu kuwaombea ulinzi?

Bagyemu: Sikuyaona kabisa.

Lissu: uliona hati ya viapo ya Amini Mahamba na Mossie Kahima ?
George: Sikuona kabisa.

Lissu: Je unajua chochote kuhusu kilichofanya katika jambo hilo la mashahidi wa siri?

Bagyemu: Mimi ninachojua waliopatiwa ulinzi huo ni raia tu.

Lissu: Sasa tuzungumze kuhusiana na uhaini.

Ulisema kwamba nilielekeza uchunguzi wa uhaini kwasababu Lissu alisema atahamasisha uasi?

Bagyemu: Ni kweli kabisa.

Lissu: Sasa kuna mahali kokote umetafsiri neno uasi?

Bagyemu: Kuzuia uchaguzi, vitisho kwa serikali basi sikusema neno moja moja. kwahiyo sikutoa tafsiri ya neno uasi.

Lissu: Je katika hati ya mashtaka ninayoshtakiwa nayo kuna ufafanuzi wa neno tutahamasisha uasi?

Bagyemu: Huo ufafanuzi upo.

Lissu: Sasa tuambie upo wapi, Hapo kwenye hati ya mashitaka, nakusomea hati ya mashitaka ilivyosema Neno uasi limetajwa mara mbili. Je kuna mahali kokote imeandikwa?

Bagyemu: Uasi ilitafsiriwa.

Lissu: Una akili timamu wewe afisa wa polisi?

Bagyemu: Nina akili timamu ndio maana ni afisa wa Polisi.

Lissu: unaweza kuwa afisa wa polisi nchi hii na ukawa huna akili timamu
Lissu: Sasa uasi maana yake nini, Naomba nimsomee tafsiri kutoka kamusi kuu ya kiswahili toleo la 3 ni kitendo cha kuwaondoa madarakani na pia nakusomea Kamusi ya Baraza la Kiswahili la Zanzibar inasema tendo la kuvunja sheria, kanuni au amri.

“Kamusi ya kiswahili sanifu imetolewa na Chuo kikuu cha Dar es Salaam na hii inasema tolea la 2002 inasema uasi hali ya uvunjaji wa kanuni, sheria au amri,”.

Sasa swali je wewe unafahamu maana tofauti ya hizi zilizopo kwenye kamusi?

Bagyemu: hizo tafsiri zipo vizuri nakubali.

Lissu: Je kuna sheria inayohusu mikutano ya hadhara?

Bagyemu: Ipo hiyo sheria.

Lissu: Je mtu akivunja sheria ya mikutano ya hadhara atakuwa amefanya uasi, Je mtu akifanya mkutano wa hadhara bila kibali? Bila kutoa taarifa polisi

Bagyemu: Haliwi kosa la uhaini.

Lissu: Mtu akifanya maandamano bila kutoa taarifa polisi ni kosa la uhaini?

Bagyemu: Sio kosa la uhaini.

Lissu: Hilo neno uasi ni kuvunja sheria?

Bagyemu: Ni kuvunja sheria za Uchaguzi.

Lissu: Safi umekuja vizuri. Twende kwenye Sheria za Uchaguzi. Ninayo hapa Sheria ya Uchaguzi wa Rais wabunge na madiwani ya mwaka 2024 .Sheria na. 1. Nataka nimuelekeze shahidi sura ya 7 inayozungumzia makosa na adhabu yani makosa ya Uchaguzi. Sasa wambie majaji kosa la kwanza ni kosa gani?

Bagyemu: Makosa yanayohusu uandikishaji wa wapiga kura.

Lissu: Hili ni kosa la uhaini nitakuuliza yote ili nikienda kunyongwa niseme hakuna swali niliacha kuuliza, kosa la pili ni nini, Kutumia wadhifa kushawishi wasiombe kuteuliwa.

Bagyemu: Anasoma

Lissu: Sasa katika yote uliyosoma kwenye sheria hiyo kuna kosa la kuzuia uchaguzi Mkuu?

Bagyemu: Lipo kwenye makosa mengineyo.

Lissu: Hebu yaseme.

Bagyemu: makosa mengineyo maana yake ni kusema uongo na adhabu yake ni kulipa faini elfu 50.

Lissu: Kwahiyo katika orodha ya makosa yote ya uchaguzi hakuna kosa la kuzuia Uchaguzi ni kweli?

Bagyemu: Kwa niliyoyasoma hakuna hilo kosa lakini sehemu nyingine linaweza kuwepo.

Lissu: Hayo mengine baki nayo mwenyewe mimi nimekupa sheria. ” Mtu hawezi kwenda kunyongwa bila mapambano hilo nakuahidi. Sasa twende,”.

Lissu: Atakinukisha vibaya sana tena sana. Ulisema hivyo?

Bagyemu: Ni sahihi.

Lissu: Kwenye maelezo yako uliyanukuu hayo maneno “Wanasema msimamo huu unaashiria uasi, tutakwenda kukinukisha sana sana” Je katika maelezo yako yote ulifafanua maana ya maneno ‘tutakinukisha vibaya sana au tutakinukisha sana ‘

Bagyemu: Sikutafsiri neno moja moja.

Lissu: Unafikiri ni rahisi kunyonga mtu. Haya maneno kwenye hati ya mashitaka kuna mahali hayo maneno tutakinukisha yametafsiriwa?

Bagyemu: Kwa neno moja moja hayajatafsiriwa.

Lissu: Sasa twende kwenye Kiswahili sanifu tukaone maana ya neno kukinukisha .Tuangalie sasa maana ya neno ‘kukinukisha , ni sahihi neno kukinukisha linatokana na neno nuka au nukia?

Bagyemu: Ni sahihi .

Lissu: Kamusi inasema tokwa na harufu mbaya au vunda na nukia ni toa harufu nzuri. Kamusi nyingine ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam inasema nuka ni toa harufu mbaya kwasababu ya kuoza. Nukia toa harufu nzuri kama vile marashi. Sasa kama tulisema tutakinukisha sanasana maana yake kinuke vibaya kitoe harufu mbaya sana si kweli?

Bagyemu: Kwa unayosoma kwenye kamusi ni kweli kabisa.

Lissu: Na vilevile kukinukisha kinukie ni kukifanya kitoe harufu nzuri sana?

Bagyemu: Kwa vile ulisema vibaya basi ni kinuke sio kunukia.

Lissu: Je na kukinukisha sana sana ni inaweza kuwa kinukie vizuri sana?

Bagyemu: Hiyo haiwezekani.

Lissu: Ulisema kwenye ushahidi wako kwamba Tar. 09/04 ulipigiwa simu na DCP Ramadhani Ng’anzi kuwa alikuwa amekamatwa Mbinga na angesafirishwa usiku huo huo?

Bagyemu: Ni kweli kabisa.

Lissu: Sasa waeleze majaji kama amri ya kunikamata mimi ilitoka kwako au kwingineko?

Bagyemu: Ilitoka kwingineko.

Lissu: Yalitokea Dodoma kwa akina Kingai?

Bagyemu:Hilo sijui.

Lissu: Kwahiyo ni kweli mawasiliano yako na Kingai yalikuwa yanapitia kwa Ng’anzi?

Bagyemu: Mimi sijui kama ilitokea huko.

Lissu: Sasa turudi kwenye PGO. Ni kweli au si kweli askari polisi wanaatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuelewa kanuni kwamba Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayotumia kanuni ya utawala wa sheria?

Bagyemu: Ni kweli kabisa.

Lissu: Order 1(2)C yapo kwenye PGO hayo niliyosema yapo huko kwenye PGO?

Bagyemu: Ni sahihi yapo.

Lissu: Askari polisi wote wanatakiwa kwa muda wote wanatakiwa kuheshimu haki za binadamu na uhuru uliowekwa na katiba?

Bagyemu: Sahihi kabisa.

Lissu: O.1(3) ya PGO ndio hayo yapo?

Bagyemu: Ni sahihi kabisa.

Lissu: Je haki ya kutoa maoni ni pamoja na mambo mnayoyasimamaia kama haki za msingi kwa binadamu?

Bagyemu: Ni sahihi kabisa.

Lissu: Haki mnayoitakiwa kuiheshimu muda wote ni kuhakikisha kila mtu kuishi kwa uhuru bila kosa lolote?

Bagyemu: Ni kweli pia.

Lissu: Haki ya kutoa mawazo yake hadharani na kujiunga na vyama vya siasa au mashirika?

Bagyemu: Ni sahihi kabisa.

Lissu: Haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu kwa mujibu wa ibara ya 27?

Bagyemu: Ni sahihi kabisa.

Lissu: Sasa ni kweli au si kweli PGO inaposema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia ya vyama vingi?

Bagyemu: Ni kweli kabisa.

Lissu: Sasa kama ni nchi ya mfumo wa vyama vingi ni sahihi Inategemea nini au utaratibu wa Polisi?

Bagyemu: Inategemea sheria.

Lissu: Ni haki kuunda Chama na kupinga serikali?

Bagyemu: Ni kweli kabisa.

Lissu: Ni halali kwa mtu yeyote kupinga Chama kinachotawala?

Bagyemu: Itategemea kitu gani kwa njia halali inaruhusiwa.

Lissu: Kuitisha mikutano ya hadhara au mikutano ya ndani si ni sahihi?

Bagyemu: Ni sahihi kabisa, kutaka kuwa na mkutano ni shida vitisho.

Lissu: Sasa waeleeze Majaji katika maelezo yako kuna mahali kokote ambapo ulieleza kwamba hawa watu wana haki ya kukutana na kusema mambo yao?

Bagyemu: Hilo sikuandika.

Lissu: Kuna mahali kokote ulisema Tundu Lissu na Chadema wana haki ya kutaka mabadiliko ya Katiba?

Bagyemu: Sikusema kwenye maelezo yangu

lissu: Ulisema pia kuwa majaji ni watu wa Rais na ni maccm kwahiyo mahakamani hakuendeki?

Bagyemu: Ni sahihi.

Lissu: Kwa ufahamu wako Rais ndie anateua majaji wa Mahakama kuu?

Bagyemu: Ndio sahihi.

Lissu: Kwa ufahamu je majaji wa Mahakama ya Rufani?

Bagyemu: Anateua pia.

Lissu: Jaji Mkuu Je?

Bagyemu: Anateua pia.

Lissu: Je ndie anateua Jaji Kiongozi?

Bagyemu: Ni sahihi pia.

Lissu: Anateua Wasajili wa Mahakama kuu na mahakama ya rufani?

Bagyemu: Ni kweli.

Lissu: Kwa ufahamu wako Rais ndie anayeteua Mwanasheria Mkuu wa Serikali?

Bagyemu: Ni sahihi hadi DPP anateua Rais.

Lissu: Mwanasheria Mkuu wa Serikali akiteuliwa anaakuwa Mbunge ni kweli?

Bagyemu: Ni kweli kabisa.

Lissu: Mbunge yeyote wa nchi hii ni lazima awe mwanachama wa Chama cha siasa?

Bagyemu: Ni kweli kabisa.

Lissu: Sasa waeleze majaji kama unamfahamu Jaji Eliezer Feleshi Mbuki?

Bagyemu: Namfahamu ndio.

Lissu: Kama Eliezer Feleshi Mbuki alikuwa Mwanasheria mkuu wa serikali na Mbunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Bagyemu: Ni kweli.

Lissu: Kwahiyo alikuwa mwanachama wa CCM?

Bagyemu: Hilo sina uhakika.

Lissu: Je unamfahamu Jaji Frederick Werema marehemu?

Bagyemu: Namfahamu.

Lissu: Na yeye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali?

Bagyemu: Ndio

Lissu: Je na yeye alikuwa mwanachama wa CCM?

Bagyemu:Hapana

Lissu: Je Werema na yeye alikuwa mwanachama wa CCM?

Bagyemu:Hapana

Lissu: Aina ya Wabunge ni waliochaguliwa, viti maalumu, walioteuliwa.

Sifa za mtu kuwa mbunge. Anasoma ya kwanza raia na yapili mwanachama wa chama cha siasa na asipokuwa mwanachama wa Chama cha siasa huwezi kuwa mbunge.

Je Frederick Werema alikuwa mwanachama wa CCM au hakuwa?

Bagyemu: Huyo Hakuwa.

Lissu: Unamfahamu Jaji Mkuu George Mcheche Masaju?

Bagyemu: Huyo nimesoma nae.

Lissu: Alikuwa mwanasheria mkuu wa Serikali?

Bagyemu: Ndio

Lissu: Alikuwa mwanachama wa CCM?

Bagyemu: Hilo sio kweli.

Lissu: Je unafahamu wakati wa urais wa Mkapa, Masaju alikuwa mshauri wake wa sheria ikulu?

Bagyemu: Ni sahihi kabisa.

Lissu: Wambie majaji kuwa aliteuliwa kuwa naibu mwanasheria mkuu na baadae kuwa mwanasheria mkuu wa serikali?

Bagyemu: Ni sahihi kabisa.

Lissu: Na sasa Samia kamteua kuwa Jaji mkuu?

Bagyemu: Ni sahihi kabisa.

Lissu: Ni sahihi alikuwa Jaji wa Mahakama ya rufaa na anafanya kazi Ikulu?

Bagyemu: Ni sahaihi alikuwa anafanya ikulu.

Lissu: Unafahamu Samia anahamisha wamasai ngorongoro kwenda Muheza?

Bagyemu: Hilo sijui kabisa.

Wakati huo wakili wa serikali mkuu Nassoro Katuga amesimama na kudai kuwa maswali ya ngorongoro hayahusiani na shauri hilo “Mahakama inaweza kuzuia maswali kwa mujibu wa kifungu cha 167 cha sheria ya ushahidi. Anasema sasa naomba huyu mtu azuiwe huko anakotaka kwenda japo anaruhusiwa kuuliza chochote swala la Ngorongoro na masuala ya Rais hayahusiani kabisa. Ametuhamishia Ngorongoro”

Lissu: Waheshimiwa Majaji mimi nataka kumuonyesha ni kwa namna gani huyu Jaji Mkuu Masaju ni mtu wa Rais hawa wanafikiri Rais ni semi God (mungu mtu) huyu mtu ni Rais sio Mung kabisa tunaweza kumtaja kabisa.

“Wao walisema Majaji ni watu wa Rais hayo maneno nimesema mimi sasa wavumilie mimi niulize maswali tafadhali,” alidai Lissu.

Wakati huo huo Jaji anayeongoza jopo hilo Jaji Dunstan Ndunguru amesema kuwa mahakama hiyo haitaingilia mchakato huo “Hebu tuendelee basi”.

Bagyemu: Sijui kama kuna suala la kuhamisha wamasai kule ngorongoro.

Lissu: Na unajua kama Masaju aliongoza timu ya washauri kumshauri Rais hadi kuhamisha wamasai na baadae ndio ameteuliwa kuwa Jaji Mkuu?

Bagyemu: Hilo sijui.

Lissu: Je unafahamu 1964 hadi 1994 watu ilikuwa ni lazima wawe wanachama wa CCM?

Bagyemu: Ni sahihi kabisa.

Lissu: Je unafahamu kipindi hicho chote ukitaka kuingia chuo cha kwanza wanauliza kadi ya CCM?

Bagyemu: Sijui hilo .

Lissu: Ukitaka kuwa mtumishi wa umma katika kipindi hicho lazima uwe MwanaCCM katika kipindi hicho?

Bagyemu: Sijui kabisa.

Lissu: Hufahamu kwasababu hamjui historia ya nchi hii. Waeleze majaji Jaji Elizer Feleshi, Ferdinand Wambari, Jaji Masaju, Amir Mruru, Leila Mgonya, Mustapha Ismail Kambona, Sam Rumanyika hao wote ni wanaCCM kwasababu nilienda nao JKT?

Bagyemu: Mimi sifahamu

Lissu: JKT yenu ilikuwa ni oparesheni Chama yani ni Oparesheni Programu CCM.

Bagyemu: Hapana

Lissu: Je hao wote niliowataja sema kama waliwahi kutangaza popote kuacha kuwa maCCM?

Bagyemu: Sijawahi kusikia.

Lissu: Mimi mwenzao nilitangaza kuacha kuwa mwanaccm nikawa Chadema je hao walitangaza lini?

Bagyemu: Sijui.

Lissu: Je unamfahamu Agustino Ramadhani alikuwa Jaji Mkuu?

Bagyemu: Ndio nafahamu.

Lissu: Sasa alivyomaliza ujaji akaenda kuchukua fomu ya urais CCM je alijiunga lini CCM? Alijiunga zamani sana kabla ya mfumo wa vyama vingi. Je aliacha lini kuwa mwanaccm?

Bagyemu: Sijui kabisa.

Lissu: Jaji Mwambegele unamfahamu yule wa tume ya Uchaguzi?

Bagyemu: Namfahamu.

Lissu: Je aliteuliwa na Rais kuwa Mwenyekiti wa Tume?

Bagyemu: Ni sahihi kabisa.

Lissu: Jaji Themistocles Kaijage, Jaji lubuva hao wote walikuwa wenyeviti wa tume ya Uchaguzi?

Bagyemu: Ni kweli kabisa.

Lissu: Na waliteuliwa na Rais?

Bagyemu: Ni sahihi.

Lissu: Je kuhusu Jaji Nyalali na Jaji Kisanga aliteuliwa na Rais kuwa wenyeviti wa tume za Rais?

Bagyemu: Ni kweli.

Lissu: Wanalipwa hela za serikali na umma wakateuliwa hao wote majaji nilowataja?

Bagyemu: Sijui kwakweli.

Lissu: Mohamed Chande Othamn amekuwa akiteuliwa kuwa Mwneyekiti wa Kikosi Kazi cha haki jinai?

Bagyemu: Ni sahihi.

Lissu: Sasa nikisema Majaji wanapenda kuteuliwa kwenye tume nakosea wapi?

Bagyemu: Huna unalokosea.

Lissu: Nakosea nini nikisema wanapenda kupandishwa vyeo hao majaji ni dhambi hiyo?

Bagyemu: Sio dhambi.

Lissu: Unasema nilisema kuwa mahakamani hakuendeki majaji hawatendi Haki?

Bagyemu: Ni haki ulisema.

Lissu: Sasa ngoja nikusomee Tume ya Warioba ilisema nini kuhusu utendaji wa Majaji. Ukurasa wa 85 wa utafiti wa tume. Inasema hivi. “jaji bila kulazimishwa anaweza kuwa na tamaa kuwa jaji mkuu mkuu au apewe cheo kingine ”

“Ukurasa wa 90 Jaji mkuu Nyalali aliwahi kusema tatizo la mahakama kuu ni rushwa. Tume ya Warioba ilisema majaji “Ingawa Mahakama kuu hufanya maamuzi isiyozingatia maamuzi ya kimsingi ila ni mahakama ya rufani isiyotenda maamuzi yakiufundi yanayoweza kutenda haki ya kimsingi”

Lissu: Sasa je mimi nikisema mahahkamani hakuendeki linakuwaje kosa la uhaini?

Bagyemu: Hilo sio kosa na hujakosea hapa. Hilo lipo Kisutu.

Lissu: Mlisema kuwa maneno yangu yalikuwa Jambo TV YouTube, Clouds na Mwanzo TV kwa mujibu wa Kahaya?

Bagyemu: Ni sahihi tulisema hivyo.

Lissu: Sasa kwanini wewe na wenzako mliamua kwenda Jambo TV peke yake?

Bagyemu: Tulienda kote.

Lissu: Je kwenye maelezo yako uliandika hilo?

Bagyemu: Sikuandika.

Lissu: Sasa kama mlienda huko kote Jambo TV na kwingine kote kwanini hujaandika?

Bagyemu: Niliandika kabla sijaenda ila watu walienda.

Lissu: Sasa tuambie shahidi gani alienda huko kwingine?

Bagyemu: Simjui aliyeenda.

Lissu: Sasa je ulikuwa objective kwenye police action zako?

Bagyemu: Nilikuwa sahihi.

Lissu: Ni kweli P alisema tulikuwa tunazingumzia matatizo ya uchaguzi?

Bagyemu: Ni sahihi P alisema.

Lissu: Sasa je kuzungumzia hayo matatizo ya uchaguzi ni makosa ya uhaini?

Bagyemu: Yeye alielewa hivyo.

Lissu: Kwahiyo ni uhaini?

Bagyemu: Sio Uhaini.

Lissu: Haya maneno ulikuwa unayafahamu ulipoletewa Tarehe 07 Aprili?

Bagyemu: Ndio sahihi.

Lissu: Na tarehe 8 Aprili ndio uliamua kufungua makosa ya uhaini?

Bagyemu: Ni kweli kwa maelekezo yangu nilielekeza kufungua uhaini.

Lissu: Hadi tarehe 8 Aprili unahamishia jalada kwa Mahamba ulikuwa umemjulisha DPP kuhusu uhaini?

Bagyemu: Ndio nilikuwa sijamwambia DPP.

Lissu: Mpaka unamfungua tarehe 8 Aprili si DPP wala maafisa wake aliyekuwa na taarifa yoyote kwamba kuna uchunguzi?

Bagyemu: Mimi sikumjulisha ila Mahamba asingekuja ningemjulisha.

Lissu: Sikiliza wewe polisi acha kiherehere.

Baada ya mapumziko ya saa moja Lissu ameendelea alipoishia kama ifuatavyo:-

Lissu: Kesi ya Uhaini kwa haiba yake ni kesi ya usalama wa taifa ni kweli au si kweli?

Bagyemu: Ni kweli kabisa.

Lissu: Mamlaka nyingine yenye mamlaka ya kuhusika na usalama wa taifa ni TISS?

Bagyemu: Ni sahihi.

Lissu: Sasa waeleze majaji kama uliwahi mjulisha RSO?

Bagyemu: Sijawahi , RSO ni mkuu wa usalama Dar es salaam.

Lissu: Je ulimwambia Mkurugenzi Mkuu wa usalama wa Taifa?

Bagyemu: Sijawahi kabisa.

Lissu: Je unafahamu kama kiongozi mwingine wa Polisi aliwahi kutoa taarifa kwa idara ya Polisi?

Bagyemu: Sijui kabisa.

Lissu: Je hii ni kesi ambayo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa umma?

Bagyemu: Ni sahihi ilikuwa hivyo.

Lissu: Na hii ni kesi inayomuhusu mtu muhimu kisiasa?

Bagyemu: Si kweli umuhimu huo siuoni.

Lissu: Huyu mshitakiwa ni Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani nchi hii?

Bagyemu: Si kweli.

Lissu: Je unafahamu ni Makamu Mwenyekiti na Mjumbe wa Kamati ya halmashauri kuu ya IDU international Democratic Union?

Bagyemu: Ndio nasikia kwako.

Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama unafahamu au hufahamu amekuwa makamu mwenyekiti wa Chadema 2019 hadi 2025?

Bagyemu: Hilo ni sahihi kabisa.

Lissu: Je unafahamu mshitakiwa kwenye kesi hii aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Chadema 2011 hadi 2017 na alishambuliwa kwa risasi?

Bagyemu: Hilo nalifahamu ila kuhusu risasi sijui.

Lissu: Sawa afisa wa polisi mkubwa kama wewe hujui kama nilishambuliwa na risasi. Je mshitakiwa huyu amekuwa Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na haki za Binadamu wa Chadema tangu 2004 hadi 2010.

“Kama unafahamu kwamba mshitakiwa huyu aliwahi kuwa Mbunge wa Kuchaguliwa kati ya 2010 hadi 2019 alipovuliwa ubunge?”

Bagyemu: la kuwa Mbunge nafahamu ila la kuvuliwa sifahamu.

Lissu: Mwanasheria mkuu kivuli 2010 hadi 2017 nilipopigwa risasi?

Bagyemu: Hilo ni sahihi ila kwenye risasi sina uhakika nalo.

Lissu: Je unafahamu mshitakiwa huyu alishambuliwa na risasi tarehe 7 Septemba 2017?

Bagyemu: Nafahamu lakini sijui kuhusu wasiojulikana.

Lissu: Je unafahamu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani mwezi Septemba mwaka 2017?

Bagyemu: Sikumbuki.

Lissu: Je nikukumbushe?

Bagyemu: Naomba unikumbushe.

Lissu: Alikuwa ni Mwigulu.

Lissu: Sasa baada ya kushambuliwa nilisafirishwa kwenda Nairobi?

Bagyemu: Ni sahihi ila muda sijui ilikuwa saa ngapi.

Lissu: Je unafahamu au hufahamu kwa wakati huo uwanja wa Ndege wa Dodoma ulikuwa hauruhusu ndege kutua baada ya saa 12 jioni?

Bagyemu: Hilo nafahamu kabisa.

Lissu: Eleza kwa vile kulikuwa na hilo zuio ilibidi ruhusa maalumu itolewe na mamlaka ya ndege Tanzania?

Bagyemu: Hilo sijui.

Lissu: Je unafahamu Waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba ndie aliyetoa maelekezo?

Bagyemu: Hilo sijui.

Lissu: Waeleze kama unajua kama Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alikuja kunitembelea Nairobi?

Bagyemu: Nafahamu alikuja ndio.

Lissu: Rais Mwinyi na mkewe pia walikuja. Hilo je?

Bagyemu: Hao sifahamu kama waliokuja.

Lissu: Je unafahamu Warioba, Jaji Chande Othman nao walikuja kunitembelea.

Bagyemu: Kimya

Lissu: Sasa nakuuliza tena je hii ni kesi yenye umuhimu mkubwa wa kisiasa na umma?

Bagyemu: Sio, kwasababu sio kesi ya kisiasa.

Lissu: Je mshitakiwa huyu ni mtu muhimu kisiasa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Bagyemu: Sio mtu muhimu.

Lissu: Je unafahamu kwamba mshitakiwa huyu ni Wakili toka mwaka 2003?

Bagyemu: Hilo natambua.

Lissu: Unafahamu aliwahi kuchaguliwa kuwa Rais wa TLS 2017?

Bagyemu: Nalitambua hilo.

Lissu: Unajua kama cheo hicho hupewi pewi bali wanakuchagua na kukupa nafasi hiyo kwasababu ya sifa?

Bagyemu: Ni kweli nafahamu.

Lissu: Je mshitakiwa huyu amekuwa mpiganiaji wa mabadiliko ya kisiasa toka akiwa Jeshini?

George: Sifahamu hilo.

Lissu: Je unafahamu ili nchi yetu aingie kwenye mfumo wa Vyama vya siasa ilibidi aunde tume?

Bagyemu: Ni sahihi.

Lissu: Waeleze majaji kama mshitakiwa huyu alitoa ushuhuda mbele ya tume ya Nyalali kwenye jopo lililokuwa likiogozwa na Jaji Augustino Ramadhani kuhusu masuala ya mabadiliko ya katiba mpya?

Bagyemu: Nafahamu tume ilikuwepo hiyo.

Lissu: Je unafahamu mshitakiwa huyu alikuwa mgombea ubunge jimbo la singida kusini mwaka 1995?

Bagyemu: Nafahamu ila hakushinda huo mwaka.

Lissu: Unafahamu baada ya pendekezo la Nyalali serikali ya CCM ilikataa tume huru na katiba mpya?

Bagyemu: Hilo sifahamu.

Lissu: Je unafahamu mwaka 1998 waliunda tume nyingine ya Katiba iliyoongozwa na Robert Kisanga?

Bagyemu: Hilo nalifahamu.

Lissu: Kama unafahamu tume ya Jaji Kisanga nayo ilipendekeza katiba mpya na mfumo mpya wa uchaguzi nayo ilikataliwa na eerikali ya Mkapa?

Bagyemu: Nafahamu hilo.

Lissu: Je unawafahamu waliokuwa wajumbe wa tume ya mabadiliko ya Katiba iliyoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete?

Bagyemu: Nawafahamu ndio mtu kama vile Paul Makonda.

Lissu: Amemwambia una akili wewe. Huyo hakuwa mjumbe wa tume. Huyo alikuwa Bungeni. Wajumbe ni kama Polepole ambae sasa tunaambiwa ameuwawa.

Lissu: Sasa nakuuliza huu usomi umeupata wapi?

Bagyemu: Nisingekuwa kamishina wa jeshi la Polisi sio kila mmoja anapata hii nafasi.

Lissu: Anamwambia mimi najua sio kila anayepata anastahili kuwa kamishna wa Polisi kama wewe vile.

“Unajua kama mshitakiwa huyu ndie aliyeongoza wakati wa bunge la mabadiliko ya katiba ndie alikuwa Mnadhimu wa Kambi ya upinzani na aliongoza hoja zote za kisheria upande wa upinzani kuhusu Katiba?”

Bagyemu: Nafahamu hilo, ulikuwa ndie kiongozi wa Upinzani.

Lissu: Unafahamu mshitakiwa huyu ndie aliyeandika hoja zote za kikatiba pale bungeni za kikatiba za kambi ya upinzani?

Bagyemu: Hilo sijui.

Lissu: Je unafahamu mshitakiwa huyu ana ufahamu kuhusu masuala ya sheria za Uchaguzi?

Bagyemu: Hilo silifahamu.

Lissu: Je unafahamu pia mshitakiwa huyu kama Wakili amekuwa Wakili kwenye kesi za Uchaguzi nyingi kuliko wakili mwingine yeyote nchi hii?

Bagyemu: Nafahamu ni Wakili ila kuwa wakili kuliko wote kufanya kesi nyingi za uchaguzi sifahamu.

Lissu: Je unafahamu kama mshitakiwa huyu ameandika Kitabu kuhusu matatizo ya kikatiba Tanzania, Kenya na Uganda?

Bagyemu: Sijapata kukisoma bado hicho.

Lissu: Waeleze majaji kwamba baada ya Uchaguzi Mkuu 2020 akiwa uhamishoni alianza kufanya utafiti wa matatizo ya uchaguzi kuanzia 2021 hadi 2025 alipokamatwa?

Bagyemu: Hilo Sijui.

Lissu: Je kama isingekuwa kukamatwa na kuwekwa mahabusu angeshachapisha kitabu chake cha The Architecture of Free and fair Election?

Bagyemu: Hilo sijui

Lissu: Je unafahamu mshitakiwa huyu amepata tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwasababu ya kupigania haki za binadamu?

Bagyemu: Hilo sifahamu.

Lissu: Je unafahamu au hufahamu mwezi wa tano mwaka 2011 mshitakiwa huyu alipata tuzo ya kuwa fellow wa Bridgeport united state of America?

Bagyemu: Hilo mimi sifahamu.

Lissu: Unafahamu Chuo Kikuu cha BridgePort walitoa tuzo hiyo wakisema kwa kutambua utendaji uliotukuka kupigania haki za binadamu?

Bagyemu: Hilo sifahamu pia.

Lissu: Je unafahamu siku chache kabla sijachaguliwa kuwa Rais wa TLS nilikamatwa Dodoma na kusafirishwa kuja Dar es salaam siku nne na nilipotoka nikaenda Arusha kuchaguliwa kuwa Rais wa TLS?

Bagyemu: Sifahamu hilo

Lissu: Unajua nilipotangaza ndege ya Bombadier ilipokamatwa na walinikamata walisema wanaenda kunipima mkojo ili wanisingizie madawa?

Bagyemu: Hilo sifahamu.

Lissu: Katika kipindi cha Magufuli nilikamatwa mara nane na kushitakiwa mara 6 hapo Kisutu?

Bagyemu: Sifahamu ila nashangaa kwanini ni wewe tu?

Lissu: hujui Mbowe alishtakiwa na nini? Hawa akina Heche hujui kesi walizowahi kuwa nazo?

Bagyemu: Aah! Nimekumbuka, nafahamu basi.

Lissu: Tarehe 11 Agosti 2024, unafahamu kuwa nilikamatwa jijini Mbeya nikiwa nimeenda Mbeya kusheherekea siku ya Vijana?

Bagyemu: Nakumbuka mliletwa hadi Central na tukawapeleka majumbani.

Lissu: Acha kiherehere sijakuuliza hayo ya nyumbani wewe George.

Lissu: Unafahamu nilikamatwa na kupelekwa Vwawa na kesho yake nililetwa kwenye kituo cha Polisi Central Dar?

Bagyemu: Mimi niliona umekuja Central Dar es salaam.

Lissu: Na unafahamu nilivyofika Central hamkunishitaki kwa lolote mliniambia nirudi nyumbani tu?

Bagyemu: Hiyo sahihi.

Lissu: Mwaka jana umesema nilikamatwa Magomeni?

Bagyemu: Ndio nimesema hivyo.

Lissu: Wewe ulikuwa Depeuty ZCO wakati nakamatwa hapo Magomeni?

Bagyemu: Ndio nilikuwa na cheo hicho.

Lissu: Nikisema mimi sikuwahi kukamatwa na Polisi magomeni?

Bagyemu: Sijui ulikamatiwa magomeni.

Lissu: Nikikwambia sijawahi kupelekwa Oysterbay toka nizaliwe utasema nasema uongo?

Bagyemu: Ndio utakuwa unasema uongo.

Lissu: Sasa mimi nakwambia nilikamatwa nyumbani Tegeta na kupelekwa Mbweni kituo cha polisi ukiwa chini ya kiapo unadhani unafaa kuwa askari wa jeshi la polisi?

Bagyemu: Ndio ninafaa hivyo hivyo.

Lissu: Shahidi nikikwambia tarehe 9 Aprili 2025 , nimekamatwa ili tu niwe gerezani mpaka uchaguzi upite na ili huyu utu na kazi asiwe na mpinzani wa maana?

Bagyemu: Sio kweli

Lissu: Je baada ya mimi kukamatwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima walitangaza Chadema hairuhusiwi kuweka mgombea?

Bagyemu: Hilo sikumbuki.

Lissu: Na ni kweli au si kweli ndani ya mwezi huo huo mmoja niliposhitakiwa kwa uhaini msajili wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi amesimamisha Ruzuku kwa chama cha Chadema ni kweli au sio kweli?

Bagyemu: Sikumbuki

Lissu: Msajili wa Vyama vya siasa, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, IGP na DCI, DPP hawa wote ni wateule wa Rais?

Bagyemu: Hawa wote ni kweli.

Lissu: Ndani ya mwezi huo huo mmoja jaji wa Mahakama hii akaamuru shughuli za siasa zote za Chadema zisimame?

Bagyemu: Ni Kweli.

Lissu: Na huyo jaji alikuwa mjumbe wa Tume Zanzibar na ni mteule wa Rais?

Bagyemu: Ni kweli.

Lissu: Sasa tuambie huyu Mwenyekiti wa Chadema amefunguliwa mashitaka ya uhaini na wateule wa Rais?

Bagyemu: Sio kweli.

Baada ya swali hilo Lissu aliwaeleza majaji kuwa ameshamalizana na shahidi huyo . shauri hilo litaendelea kesho saa tatu asubuhi ambapo upande wa serikali utampitisha wenye maswali aliyoulizwa ili kusawazisha.

About The Author

error: Content is protected !!