
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, ‘OMO’ amewataka wazee wa Zanzibar kutambua wajibu wao wa kihistoria wa kusimama mstari wa mbele katika mapambano ya kuleta mabadiliko kupitia uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba. Anaripoti Mwandishi wetu, Pemba … (endelea).
Akizungumza katika mkutano wa ndani na wazee wa Jimbo la Mtambile, uliofanyika katika ukumbi wa Judo Shehia ya Chole Kengeja, Othman aliweka wazi kwamba wazee si tu nguzo ya familia, bali pia ni taa ya jamii inayopaswa kuongoza kizazi kipya kuelekea mustakabali bora.
“Wazee wana mchango mkubwa wa kuhakikisha vijana wao wanafanya maamuzi sahihi. Wanapaswa kutambua kuwa mwaka huu ni mwaka wa kuinusuru Zanzibar,” alisema Othman, akisisitiza kuwa busara za wazee ndizo zitakazowapa vijana ujasiri wa kuchagua mabadiliko.
Akigusia changamoto za maisha ya kila siku, Othman alisema: “Kila mzazi anapaswa kuangalia hali ngumu anayopitia. Mazingira haya yameandaliwa na watawala waliopo kwa lengo la kuwanyanyasa wananchi na kuwafanya watumwa wao.”
Aliongeza kuwa jukumu la wazee halipaswi kuishia kwenye nasaha pekee bali pia kushirikiana na vijana kuhakikisha kura zinapigwa kwa wingi.
“Ni jukumu lenu kusimama imara na kuwaambia vijana wenu kuwa mabadiliko yanakuja kupitia sanduku la kura 29Oktoba .”
Katika hotuba yake, Othman pia aliahidi mageuzi makubwa kwenye sekta ya ajira akisema iwapo atakua kuwa Rais, hatakuwa tayari kuona tena mzazi akibeba mzigo wa kijana asiye na ajira.
Aliahidi kuwa Serikali yake itatengeneza mazingira ya ajira na mitaji kwa vijana ili familia ziishi kwa heshima.
Akizungumzia sekta ya afya, alisema, alisema huduma ya afya ni haki, si biashara hivyo wazee hao wanapaswa kutibiwa ipasavyo kama wengine.
Aidha alisema Serikali ya ACT itapunguza gharama za matibabu na kuhakikisha kila Mzanzibari anapata matibabu kwa heshima bila ubaguzi.
Katika hatua nyengine Othman alisisitiza kwamba serikali yake itaboresha mfumo wa elimu unaoendana na mazingira ya Zanzibar.
Aliahidi kuboresha mfumo wa elimu kwa kuhakikisha vijana wanajifunza masomo ya vitendo na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri badala ya kubaki wakikariri vitabu bila tija.
Wakati hayo yakijiri wazee waliokuwepo katika mkutano huo walimpongeza Othman kwa kuona nafasi yao katika safari ya mabadiliko.
Mzee Ali Mohamed kutoka Chole Kengeja alisema: “Sisi wazee tumekuwa shahidi wa matatizo ya Zanzibar kwa muda mrefu. Sasa tupo tayari kuwaongoza vijana wetu kuhakikisha tunaleta mabadiliko kupitia kura.”
Kwa upande wake, Mzee Makame Juma aliongeza kuwa wazee ndiyo nguzo ya mshikamano wa jamii na iwapo watajitokeza kwa wingi kupiga kura, Zanzibar itaanza ukurasa mpya wa maendeleo na heshima.
ZINAZOFANANA
Vurugu zawang’oa vigogo DART/UDART
OMO: Nitairejeshea Zanzibar rasilimali zake, Wananchi wafaidike
Watatu wakamatwa vurugu mwendo kasi