September 30, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Busara za Maalim Seif nguzo ya kuinusuru Zanzibar – Othman Masoud.

 

OTHMAN Masoud Othman ‘OMO’ , mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, amesema kuwa busara, uadilifu na uthubutu wa kisiasa wa Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ndiyo nguzo pekee iliyoiokoa Zanzibar kutokana na kuingia katika maafa makubwa yaliyokuwa yakitishia mustakabali wa nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pemba … (endelea).

Akizungumza leo tarehe 30 Septemba 2025, mara baada ya kutembelea kaburi la kiongozi huyo wa kihistoria lililopo Mtambwe Nyali, Pemba, Othman alisema kuwa mchango wa Maalim Seif hauwezi kufutika, kwani alisimama kama ngao ya amani na maridhiano kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

“Maalim Seif aliamua kuilinda Zanzibar kwa hekima kubwa, alipokuwa na nafasi ya kupeleka nchi kwenye njia mbaya lakini akachagua maridhiano na mshikamano wa kitaifa,”amesema Othman.

Busara zake ndizo zilizotufanya tuendelee kuwa na matumaini ya kesho bora,” alisema Othman kwa msisitizo.

Akigusia uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Othman alionya kuwa Zanzibar inakabiliana tena na changamoto zinazofanana na zile za mwaka 2020, akibainisha kuwa baadhi ya wanasiasa waliokuwa karibu na Maalim Seif wamepuuzia makubaliano ya kihistoria yaliyokuwa dira ya amani na maridhiano.

“Kama taifa tusipoheshimu busara na misingi ya maridhiano aliyotuachia Maalim, basi tunaelekea kurudia makosa yale yale ya uchaguzi wa 2020.

Hii ni hatari kubwa kwa Zanzibar na kwa mustakabali wa vizazi vyetu,” aliongeza.

Othman alisisitiza kuwa ACT Wazalendo imedhamiria kuendeleza urithi wa kisiasa na kimaadili wa Maalim Seif kwa kusimamia haki, demokrasia na maendeleo ya wananchi wote bila ubaguzi.

Alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi, akisema kura zao ndiyo silaha ya kulinda heshima ya nchi na urithi wa maridhiano.

“Leo tunapoinamisha vichwa vyetu mbele ya kaburi la Maalim, tunapaswa kukumbuka siyo tu historia yake, bali pia wajibu wetu wa kuipeleka Zanzibar mbele kwa misingi ya amani, haki na mshikamano,” alisema Othman.

About The Author

error: Content is protected !!