September 29, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Polepole kumwaga mboga Jumanne

Humphrey Polepole

 

ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humprey Polepole, ameendelea kutisha watawala na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akiandika kupitia ukurasa wake wa instagram@hpolepole, leo tarehe 28 septemba, Polepole amasema, tarehe 30 Septemba 2025, atazungumza na umma.

Amesema, “Jumanne ya tarehe 30 Septemba, majira ya saa 10 jioni, nitazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara na kufichua mambo makubwa matatu.”

Ametaja mambo atakayoibua, ni kile alichoita, “historia ya ahadi hewa” za fedha za kuwainua vijana, ikiwemo madai ya Sh. 200 bilioni ndani ya siku 100, zinazotolewa na chama chake.

Jingine ambalo atalizungumzia, Polepole anasema, ni suala la bima ya afya kwa wote. Anasema, hadi sasa hakuna dhamira ya dhati ya utekelezaji wa jambo hili.

Anasema, “Siyo vizuri kudanganya wananchi… tusikubali kuchonganishwa na wananchi.”

Aidha, Polepole amataja jambo la tatu (3) atakalolizungumzia, ni kuhusu Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (4IR) na changamoto ya gharama kubwa za intaneti nchini.

Amesema, Tanzania bado inasuasua huku mataifa mengine ya Afrika yakiwa mbele.

“Tuko Mapinduzi ya 4 ya viwanda wakati hapa Tanzania mabando ya internet gharama ni juu kuliko nchi nyingi za Afrika kwa uzembe tu,” ameeleza.

Kwa mujibu wake, uamuzi wa kufanya mkutano na umma majira ya jioni, umetokana na tabia ya aliowaita, watendaji wa serikali, kufunga mitandao nyakati za usiku wakati anazungumza na umma.

“Nitazungumza mchana wakati watu wako kwenye kampeni, ili kuepukana na usumbufu wa wanaokata mitandao, nitapozungumza,” alifafanua.

About The Author

error: Content is protected !!