September 23, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kesi ya Lissu kuanza kutolewa ushahidi Oktoba 6, Samia atajwa

 

JUMLA ya mashahidi 30 wa upande wa Jamhuri wataanza kutoa ushahidi wao kwenye kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kuanzia tarehe 6 Oktoba 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Shauri hilo lilikuja leo tarehe 22 Septemba 2025, kwenye Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam, kwa ajili ya kutolewa uamuzi mdogo ambapo mahakama hiyo imetupilia mbali mapingamizi mawili yaliwekwa na Lissu.

Mapingamizi hayo yalikuwa yanahusiana na hati ya mashtaka pamoja na maelezo ya mashahidi kuchukuliwa kinyume cha Sheria.

Mara baada ya Jaji Dastan Ndungulu kusoma uamuzi huo kwa niaba ya jopo la Majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo, Lissu alisomewa maelezo ya awali (preliminary hearing) na kusaini nyaraka hiyo.

Aidha upande wa Jamhuri uliorodhesha jumla ya mashahidi 30 watakaotoa ushahidi katika kesi hiyo wakiwemo askari Polisi na raia wa kawaida.

Kwa upande wa Lissu yeye aliorodhesha jumla ya mashahidi 15, wakiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, IJP Camilius Wambura, Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Kamishna wa Polisi, Ramadhani Kingai.

Aidha Lissu ameileza mahakama hiyo kwamba anaweza kuita tena mashahidi wa ziada kama watahitajika.

Mara baada ya mawasilisho hayo upande waashtaka ukiongozwa na Wakili mkuu wa Serikali mwandamizi, Nassoro Katuga, uliomba Mahakama kuahirishwa shauri hilo kutojipanga kwa ajili ya ushahidi.

Kufuatia maombi hayo Mahakama imeahirisha shauri hilo hadi tarehe 6 Oktoba 2025, na litasikilizwa mfululizo.

About The Author

error: Content is protected !!