
David Kafulila
MKURUGENZI Mkuu wa kituo cha Ubia kati ya Sekta Binafsi na Umma (PPP), David Kafulila ameeleza kuwa kuna nafasi muhimu ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi katika kufanikisha maendeleo ya taifa, akisema miradi mikubwa kama bandari, barabara na majengo imefanikiwa kupitia ushirikiano huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).
Kafulila ameyasema hayo wakati wa kongamano la uchumi jumuishi lililofanyika leo mkoani Mbeya likiratibiwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kituo cha PPP huku akisisitiza umuhimu wa kujenga uchumi jumuishi unaozigusa moja kwa moja jamii.
“Sekta binafsi ni nguzo kuu ya kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Pia ili uchumi uwe wa watu wengi lazima ufuate sekta ambazo zimebeba watu wengi. Ripoti ya siku nyingi kidogo kutoka miaka ya 2008 inasema kwamba ukikuza uchumi kati ya asilimia nane mpaka 10 kwa miaka mitatu mfululizo, utapunguza umasikini kwa asilimia 50,” amesema Kafulila.
Pia, washiriki wengine walihimiza kila Mtanzania kushiriki na kunufaika na dira hiyo kwa kutumia fursa ya ubia kati ya sekta binafsi na umma, teknolojia, mabadiliko ya mitazamo na mshikamano wa karibu kati ya sekta zote.
Aidha, wadau wa maendeleo wamesema Tanzania imepiga hatua kupitia dira 2025 licha ya changamoto za kiuchumi za kimataifa huku wakitaja kuwa kilimo bado ni sekta dhaifu kutokana na utegemezi wa mvua na ukosefu wa viwanda vya zana za kilimo, wakishauri kuongezwa uwekezaji katika umwagiliaji, na miundombinu.
Mmoja wa wachangiaji katika kongamano hilo Jordani Matonya ameeleza kuwa dira ya maendeleo imejengwa juu ya misingi ya utawala bora, usalama, amani na utulivu. Kadhalika amesisitiza kuwa nguzo kuu tatu za dira ni uchumi jumuishi na imara, maendeleo ya watu, na uhifadhi wa mazingira, huku akitaja sekta za mageuzi zitakazowezesha utekelezaji wake kuwa ni kilimo cha umwagiliaji, utalii, viwanda na huduma za kifedha.
ZINAZOFANANA
Julai yaja na neema kwa wacheza Win&Go
Uhamiaji yawang’ang’ania wageni wa Lissu
Kitabu cha Lissu chazua gumzo mahakamani