September 16, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Lissu agoma kuendelea na kesi hadi wafuasi wake waingie mahakamani

Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema akiwa mahakamani

 

TUNDU Lissu, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendele (Chadema), amegoma kuendelea na kesi yake ya uhaini inayomkabili, kufuatia madai kuwa wafuasi wake, wamezuiwa kufuatilia shauri hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mara baada ya Majaji kuingia kwenye chumba cha Mahakama Kuu, Masjala ya Dar es Salaam, kwa ajili ya kuanza usikilizaji wa kesi hiyo, Lissu aliiambia Mahakama kuwa wafuasi wake wamezuiliwa kuingia mahakamani na askari polisi, wanaotekeleza amri ya bosi wao.

Kwa mujibu wa ratiba, leo Jumanne, tarehe 16 Septemba 2025, Lissu alitakiwa kuendelea kujenga hoja yake, kuhusiana na pingamizi aliloliwasilisha jana kupinga hati ya mashitaka.

Lissu aliiambia Mahakama kuwa amepata taarifa kwamba wafuasi wake, wanachama na baadhi ya viongozi wa chama chake, wamezuiwa kuingia mahakamani. Alisema, kutokana na kuzuiliwa huko, baadhi ya wanachama wameshindwa kuhudhuria shauri hilo.

Kutokana na hoja hiyo, Lissu ameomba Mahakama kutoa muongozo wake wa haraka na kuhoji “inawezekanaje ZCO anaawafukuze watu mahakamani na Mahakama iko kimya?

Akiongea kwa hisia kali, Lissu alisema, “Ni majaji pekee wenye mamlaka ya kutoa amri yoyote mahakamani. Sasa inawezekanaje mtu mwingine anatoa amri ndani ya viunga vya mahakama, amri ambazo pia zinakinzana na sheria na taratibu?”

Alisema, hawezi kuendelea na kesi hadi suala hilo litolewe muongozo na Mahakama na hadi wafuasi wake waruhusiwe kuingia mahakamani.

Lissu amesema, kesi hiyo ni ya wazi na kwamba kinachofanyika sasa hakina uhalisia wa uwazi wa Mahakama.

Hata hivyo, baada ya kuwasilishwa kwa hoja hiyo, Nassor Katuga, Wakili wa Serikali Mkuu, aliiomba Mahakama kuendelea ratiba ya usikilizwaji wa kesi. Alisema, suala alilowasilisha Lissu halina uhalisia.

Alisema, “lakini wafuasi hao, walikuwapo kwenye chumba cha Mahakama na walitoka muda mfupi kabla ya kesi kuanza.”

Aidha, Katuga alisema, baadhi ya watu wako Mahakamani na wanasikiliza kesi bila kikwazo. Lakini watu hao, Chadema kinasema, si wanachama wao, bali ni askari kanzu waliomwagwa mahakamani.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, majaji wameahirisha kesi hiyo hadi saa tano watakaporejea kutoa uamuzi wa suala hilo.

Hayo yamejiri wakati mahakama hiyo, ilipanga kutoa uamuzi wake leo, kuhusiana na maombi ya Lissu ya kuendeshwa kwa kesi hiyo live.

About The Author

error: Content is protected !!