
TUME ya Uchaguzi, imemuengua katika kinyang’anyiro cha urais, mgombea wa chama cha ACT- Wazalendo, Luhaga Mpina. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Mpina ameondolewa katika orodha ya wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 oktoba mwaka huu, baada ya tume kukubaliana na pingamizi dhidi yake.
Taarifa ya tume iliyotolewa leo Jumatatu, tarehe 15 Septemba 2025, imeeleza kuwa imekubaliana na pingamizi lililowasilishwa kwake na Hamza Johari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), dhidi ya uteuzi wa Mpina.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na INEC leo Jumatatu, tarehe 15 Septemba 2025 imeeleza kuwa tume iliketi leo na kufanya uamuzi juu ya jumla ya mapingamizi manne yaliyowasilishwa.
“Katika maamuzi hayo, mapingamizi matatu yaliyowasilishwa na wagombea wengine wa urais akiwamo Almas Hassan Kisabya wa NRA, Kunje Ngombale Mwiru wa AAFP na Mpina mwenyewe dhidi ya Samia Suluhu Hassan wa CCM, yamekataliwa,” imeeleza taarifa ya tume.
Imeongeza, “Lakini tume imekubali pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Mpina na hivyo, jina lake limefutwa kwenye orodha ya wagombea wa urais.”
Mapingamizi dhidi ya Mpina yamewewasilishwa Tume ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kunje Ngombale Mwilu na Hassan Almas.
Kunje anagombea urais kupitia chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP) na Almas amepitishwa kugombea urais kupitia chama cha National Reconstruction Alliance (NRA).
Jana Jumapili, ACT- Wazalendo, kilieleza kuwa kuna njama za kumuondoa mgombea wao, na kwamba mapingamizi hayo matatu yamesheheni madai yasiyo na ukweli wala msingi wowote ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa na AG.
“Kwamba, Ndugu Luhaga Mpina hakuteuliwa kwa mujibu wa taratibu za chama kuwa mgombea urais,” taarifa imeeleza.
ACT-Wazalendo, kimeyataja mapingamizi hayo kuwa ni pamoja na katika fomu ya uteuzi wa mgombea urais kwa msajili wa Vyama vya Siasa na tume ya uchaguzi, jina la Mpina halikuwamo.
Chama hicho kinakiri kuwa majina yaliyowasilishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kwa tume ya uchaguzi, jina la Mpina halikuwekwa na ofisi hiyo, lakini kinasisitiza kuwa hilo siyo kosa la mgombea wao.
ZINAZOFANANA
Polisi wanaendelea kumshikiria kada wa Chadema kwa kusambaza taarifa za uzushi
Mpina awekewa pingamizi, ACT wajibu mapigo