
CHAMA cha ACT Wazalendo kimetoa tamko rasmi kupinga uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wa kumuondoa mgombea wake wa urais, Luhaga Mpina, kwenye orodha ya wagombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 15 septemba 2025 na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu Ado, Tume ya Uchaguzi imekubaliana na pingamizi lililowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, huku ikitupilia mbali pingamizi lililowekwa na Mpina dhidi ya mgombea wa CCM, Samia Suluhu Hassan, pasipo kutoa maelezo ya kutosha.
ACT Wazalendo imeeleza kuwa haikubaliani na uamuzi huo, ikieleza kuwa umetolewa kwa kutegemea uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa ambao tayari chama hicho kimeupinga mahakamani kupitia Shauri Na. 23428/2025 katika Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma. Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa leo saa 8 mchana mbele ya Jaji Wilbert Chuma.
Chama kimeituhumu Serikali ya CCM kwa, kwa mujibu wa taarifa hiyo, kudhamiria kuvuruga mfumo wa vyama vingi nchini, kikieleza kuwa hatua ya kuenguliwa kwa Mpina ni sehemu ya mkakati huo.
Aidha, Kiongozi wa Chama Taifa, Dorothy Semu, ameagiza kufanyika kwa kikao cha dharura cha Kamati ya Uongozi ya Taifa, ili kujadili hatua hiyo na uwezekano wa kuitisha kikao cha Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi za kisiasa na kisheria.
Chama pia kimewataka wagombea wake wote wa ubunge na udiwani kuendelea kusimama imara na kuendelea na kampeni licha ya changamoto zilizopo.
ZINAZOFANANA
Mahakama yatupilia mbali pingamizi la Lissu, kesi kuendelea
Mpina aenguliwa tena mbio za kusaka Urais
Polisi wanaendelea kumshikiria kada wa Chadema kwa kusambaza taarifa za uzushi