
Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan
RAIS Samia Suluhu Hassan, amegoma kumpigia kampeni mgombea ubunge wa chama chake, katika jimbo la Kigoma Mjini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma … (endelea).
“Ninyi wote ni watoto wangu. Kwa sababu, hata yule mwingine (Zitto Kabwe), ametoa vibao vya kijani na njano vinasema mpe Mama Samia, ubunge nipe mimi. Sasa unajua kwamba kwenye nyumba watoto wakiwa wawili, watatu wanavutana? Lakini wote ni wanangu,” alieleza Samia huku akishangiliwa.
Mgombea urais huyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikuwa akijibu ombi la Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo, aliyemtaka kiongozi huyo, kutangaza maslahi yake katika jimbo hilo.
Samia alitoa kauli hiyo, leo tarehe 14 Septemba 2025, wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika jimbo la Kigoma Mjini.
Baba Levo aliyemuomba Samia kumtaja mgombea anayemuunga mkono kuelekea uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba, katika jimbo lake.
Alisema, “Sina utani. Nakuhakikishia nitampiga mtu saa tano asubuhi, kwasababu ninayeshindana naye ni mtu dhaifu sana. Ni maarufu kwenye mitandao, lakini ukimleta huku chini ni biskuti.”
Akiongea kwa kujiamini, Baba Levo alisema, “Ni kama ameshahamia CCM, maana leo alikuwa anasambaza vipeperushi vya Oktoba tunatiki, akiwa amemuweka Mama na yeye pale chini. Nakuomba Mama ni muda wa kutuambia ukweli unamsapoti nani hapa Kigoma Mjini?”
Hii ni mara ya kwanza kwa Samia kutomtangaza mgombea anayemuunga mkono katika uchaguzi huu.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, hatua ya Samia ya kutoegemea upande wowote, kuna unafuu mkubwa Zitto katika azma yake ya kurejea bungeni.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, hatua hiyo, inamuweka Zitto kwenye wakati mgumu ndani ya chama chake, kwa kudhanikiwa kuwa ni “Ndumi la kuwili.”
ZINAZOFANANA
Polisi wanaendelea kumshikiria kada wa Chadema kwa kusambaza taarifa za uzushi
Mpina awekewa pingamizi, ACT wajibu mapigo
OMO, Mwinyi jino kwa jino urais Zanzibar