
Luhaga Mpina, Mgombea Urais wa ACT Wazalendo
MGOMBEA urais wa Tanzania, kupitia chama cha ACT- Wazalendo, Luhaga Mpina, amewekewa mapingamizi yanayoweza kumuondoa kwenye kinyang’anyiro hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Mapingamizi dhidi ya Mpina yamewewasilishwa Tume ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG); Kunje Ngombale Mwilu, mgombea urais wa Alliance for African Farmers Party (AAFP) na Hassan Almas, mgombea urais wa National Reconstruction Alliance (NRA).
Kwa mujibu wa taarifa ya ACT- Wazalendo, iliyotolewa leo Jumapili, tarehe 14 Septemba, mapingamizi hayo yaliwekwa usiku wa tarehe 12 Septemba, majira ya saa 2:36 za usiku.
Taarifa inasema, ofisi ya katibu mkuu wa chama hicho, tayari imepokea mapingamizi hayo.
“Mapingamizi hayo matatu yamewekwa na AG, mgombea urais wa AAFP na mgombea urais wa NRA,” imeeleza taarifa hiyo.
Imeongeza, “…sura za mapingamizi yote matatu, ni madai yasiyo na ukweli wala msingi wowote ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa, kwamba Ndugu Luhaga Mpina hakuteuliwa kwa mujibu wa taratibu za chama kuwa mgombea urais.”
ACT-Wazalendo, kimeyataja mapingamizi hayo kuwa ni pamoja na katika fomu ya uteuzi wa mgombea urais kwa msajili wa Vyama vya Siasa na tume ya uchaguzi, jina la Mpina halikuwamo.
Kikizungumzia hoja hiyo, chama hicho kinakiri kuwa majina yaliyowasilishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kwa tume ya uchaguzi, jina la Mpina halikuwekwa na ofisi hiyo.
Hata hivyo, ACT- Wazalendo kinasema, “hilo siyo mgombea. Ni kosa la Msajili mwenyewe.”
Pingamizi la pili linahusu uraia wa Mpina. Chama hicho kinasema, ushahidi wa vyeti na vielelezo vya kisheria vimewasilishwa kuthibitisha kuwa mgombea wake huyo, ni Mtanzania kwa kuzaliwa na uraia wake haujawahi kubatilishwa.
Pingamizi lingine limehusu mali na maslahi ya kifedha ya Mpina, ambapo chama hicho kimeeleza kuwa kuna ushahidi wa kutosha na vielelezo na sahihi kuonesha kuwa mgombea huyo, waliyempachika jina la “Rais Mteule” – Candidate for Presidency – amekidhi masharti yote ya kisheria yanayohusu kutangaza mali na madeni yake.
“Tunapenda kuujulisha umma kuwa majibu ya pingamizi yaliyowasilishwa na Chama cha Mapinduzi na Serikali yake, kupitia mwanasheria wake mkuu, yamejibiwa kwa ukamilifu na uthibitisho wa kisheria,” kimeeleza taarifa hiyo, iliyosainiwa na Shangwe Ayo, naibu katibu wa habari, uenezi na mahusiano na umma.
Wameongeza, “Tunaamini Tume ya Taifa ya Uchaguzi itafanya maamuzi ya haki kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi.”
Aidha, chama hicho kimesema, kwa kuwa walishajua mapema kwamba kuna njama za kumuondoa mgombea wao, tayari wamefungua kesi Mahakama Kuu, kupinga maamuzi ya Msajili wa Vyama dhidi ya mgombea wao.
Kinasema, “Kwa kuwa tulifahamu mapema kuwa CCM wana hofu kubwa na ACT- Wazalendo katika uchaguzi huu, na kwamba njama zao ni kuhakikisha mgombea wetu anaondolewa katika kinyang’anyiro cha urais, mara baada ya amri ya Mahakama Kuu, iliyotolewa tarehe 11 Septemba, tulichukua hatua nyingine mara moja.
“Tumefungua kesi ya kikatiba kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kutomtambua mgombea wetu wa urais, Ndugu Luhaga Mpina. Kesi hiyo tayari imesajiliwa kwa hati ya dharura na kupewa Na. 23438/2025.”
Mpina aliondolewa kwenye kinyang’anyiro cha urais na Msajili wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi, aliyedai kuwa kuteuliwa kwake, kulikwenda kinyume na kanuni na taratibu za chama chake.
Lakini Alhamisi iliyopita (tarehe 11 Septemba), majaji watatu wa Mahakama Kuu – Abdi Kagomba, Evaristo Longopa na John Kahyoza, waliagiza tume ya uchaguzi kupokea fomu zake za uteuzi na kuendelea na mchakato wa kumteuwa kuwa mgombea urais.
Katika hatua nyingine, ACT- Wazalendo, kimedai kuwa kimepanga kumuwekea pingamizi mgombea urais CCM, Samia Suluhu Hassan, kwa maelezo kuwa uteuzi wake, haukufuata Katiba na Kanuni za chama chake.
“Tofauti na Katiba na Kanuni zinavyotaka, Samia amepitishwa kinyume na maelekezo hayo. Ndugu Samia hakuwahi kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea, hakuwahi kudhaminiwa na wanachama, hakuwahi kupendekezwa na Kamati Kuu ya CCM, wala hakuwahi
kupendekezwa na Halmashauri Kuu ya CCM kwa Mkutano Mkuu,” wameeleza.
ACT- Wazalendo kinasema, “Vilevile, Samia hakuwahi kushindanishwa na mwanachama yeyote wa CCM kama Katiba na Kanuni zinavyoeleza na vikao vya chama chake vya kikatiba, havijawahi kupitisha ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea urais. Kwa mantiki hiyo, tumeamua kumuwekea pingamizi ili asiweze kuwa mgombea.”
Wanaongeza, “Hivyo, mgombea huyo alipataikana kwa utaratibu wa kinyemela usiofahamika kikatiba na kikanuni, na hivyo kuvunja Katiba ya nchi na Sheria ya Vyama vya Siasa.”
ZINAZOFANANA
Polisi wanaendelea kumshikiria kada wa Chadema kwa kusambaza taarifa za uzushi
Samia agoma kumuombea kura Baba Levo
OMO, Mwinyi jino kwa jino urais Zanzibar