Afisa Takukuru mkoani Iringa, Ditram Muhoma
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), mkoani Iringa, imeweka msimamo mkali dhidi ya wagombea wanaojihusisha na kutoa ahadi za uongo wakati huu wa kampeni. Anaripoti Zakia Nanga, Iringa … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa, Afisa Takukuru mkoani Iringa, Ditram Muhoma amesema, wagombea wote wa ubunge na udiwani, wanatakiwa kuzingatia kikamilifu ahadi zilizoainishwa kwenye Ilani rasmi za vyama vyao, badala ya kutumia maneno matamu au matarajio yasiyotekelezeka kama chombo cha kuwashawishi wapiga kura.
Amesema, tabia hiyo si tu ya kupotosha umma, bali ni aina ya rushwa ya kisiasa inayodhoofisha misingi ya demokrasia na uwajibikaji.
Kwa mujibu wa afisa huyo, Takukuru inafuatilia kauli za wagombea wote wa ubunge na udiwani mkoani Iringa. Amesema, wale ambao hawatazingatia Ilani zao na hivyo, kutoa ahadi kinyume na maelezo hayo, watachukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, afisa huyo, hakutaja wagombea ambao tayari wameanza kukiuka taratibu hizo.
ZINAZOFANANA
TMA yatangaza mvua kubwa zitakuja, mikoa 14 kuathirika
TRC yaomba radhi na kuongeza safari za SGR
Mwigulu akagua uzalishaji na usambazaji maji Ruvu chini