
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa taarifa ya tukio la kupatwa kwa Mwezi linalotarajiwa kutokea tarehe 7 Septemba 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hali ya kupatwa kwa Mwezi ni tukio linalotokea wakati Dunia inapita kati ya Jua na Mwezi na kusababisha kivuli cha Dunia kuwa katika uso wa Mwezi. Aidha, hali hii hutokea wakati Dunia, Mwezi na Jua vinapokaa kwenye mstari mnyoofu. Tukio la kupatwa kwa mwezi limegawanyika katika aina kuu mbili.
Aina ya kwanza ni kupatwa kwa Mwezi Kikamilifu (Umbra), hali ambayo Dunia inakuwa imefunika mwanga wote wa Jua na kupelekea kivuli kizito (giza) katika uso wa Mwezi. Aina ya pili ni kupatwa kwa Mwezi Sehemu (Penumbra) ambapo Dunia husababisha kivuli hafifu katika uso wa Mwezi.
Tukio la kupatwa kwa Mwezi kwa tarehe 7 Septemba 2025 ni la kupatwa kwa Mwezi Sehemu na Kikamilifu. Tukio hili linatarajiwa kuonekana katika maeneo ya bara la Ulaya, Asia, Australia na Afrika. Kwa hapa nchini, hali ya kupatwa kwa Mwezi inatarajiwa kuanza kwa kupatwa kwa Mwezi Sehemu kuanzia pale Jua linapozama hadi saa 2:29 usiku na kufuatiwa na kupatwa kwa Mwezi Kikamilifu kuanzia saa 2:30 hadi saa 3:52 usiku.
Aidha, tukio hili linatarajiwa kuhitimishwa kwa kupatwa kwa Mwezi Sehemu kuanzia saa 3:53 hadi 5:55 usiku. Kwa ujumla hali hii inatarajiwa kudumu kwa muda wa takriban masaa sita.
Kwa kawaida, mzunguko wa mwezi una uhusiano mkumbwa na Kupwa na Kujaa kwa maji baharini. Hali hii inatarajiwa kuongezeka kwa kina cha maji katika Bahari wakati wa tukio hilo.
Hata hivyo, hali hiyo haitarajiwi kupekelea athari kubwa. Hali ya anga inatarajiwa kuwa yenye mawingu kiasi na kutoa fursa nzuri ya kuonekana kwa tukio hilo kwa macho.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kufuatilia tukio hili la kupatwa kwa Mwezi na itatoa mrejesho kila inapobidi.
ZINAZOFANANA
Askofu Mwanamapinduzi akimbia nchini akidai kusakwa kuuwawa
Bosi wa JamiiForum ajiuzulu ujumbe wa Tume ya Ulinzi ya Taarifa Binafsi
Chadema yalaani tukio la kushambuliwa mwandishi EATV