
JESHI la Polisi nchini Tanzania, limeanza uchunguzi kuhusu madai ya mwanamke mmoja, kumnywesha pombe mtoto mdogo. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa ya makao ya Polisi, iliyotolewa kwa umma na David Misime, Naibu Kamishena wake na Msemaji wa jeshi hilo, video hivyo, ni kinyume na sheria.
Amesema, tukio hilo ni ukatili dhidi ya mtoto na kinyume na sheria za nchi.
Kwa mujibu wa Misime, kitendo hicho kinauka Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 (Marekebisho ya 2023), katika vifungu vya 9(3) na 13, pamoja na kifungu cha 169A cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (CPA), Sura ya 16 ya mwaka 2023.
Amesema, “Kwenye mitandao ya kijamii, kunaonekana video, inayomuonyesha binti anayesemekana ametokea Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam, akidhalilishwa na kufanyiwa ukatili ambao ni kinyume cha sheria, maadili na haki za binadamu.
“Tunapenda kutoa taarifa kwamba Jeshi la Polisi, limeshaanza kulifanyia kazi tukio hilo ovu na kulaaniwa,” anaeleza Misime.
Anaongeza: “Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote, kuacha kuendelea kusambaza video hiyo, kwani kwa kufanya hivyo, ni kosa kisheria. Lakini pia ni kitendo cha kuendelea kudhalilisha utu wa mwanadamu mwezetu.”
Aidha, Misime ametoa wito kwa kila mwananchi wenye taarifa sahihi za kuwapata wahusika, kuzifikisha kwa jeshi lake, ili kuhakikisha mkono wa sheria unawafikia wote waliohusika na ukatili huo.
Anasema, wenye taarifa hizo, wanaombwa kuziwasilisha kupitia viongozi wanaoamini watazifikisha kunakohusika au kupitia namba ya simu ya Jeshi la Polisi: 0699 998899.
Vilevile, jeshi la Polisi limemtaka mwanamke huyo, kujisalimisha mara moja, katika kituo chochote cha Polisi.
ZINAZOFANANA
Bosi wa JamiiForum ajiuzulu ujumbe wa Tume ya Ulinzi ya Taarifa Binafsi
Chadema yalaani tukio la kushambuliwa mwandishi EATV
Rais Samia kuinua sekta ya viwanda na biashara