September 5, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Aliyemuua mkewe kwa kisu, ahukumiwa kunyongwa

 

MAHAKAMA Kuu, Masijala Ndogo ya Mtwara, imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Issa Kaunda baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe, Elimina Severine. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).

Jaji Martha Mpaze, ameeleza katika uamuzi wake, Kaunda, aliyetenda kosa hilo, tareh 2 Januari 2024, katika kijiji cha Llukula, wilayani Nanyumbu,mkoa wa Mtwara, anastahili adhabu hiyo, kutokana na ushahidi usio na shaka, uliyowasilishwa mbele yake.

Amesema, mshtakiwa alikiri kumuua mkewe akidai amemsema vibaya mitaani.

Anasema, kwa mujibu wa mashahidi sita na vielelezo vinne vilivyowasilishwa mbele yake, ikiwemo ushahidi wa daktari, marehemu alipatikana na jumla ya majeraha saba ya kuchomwa shingoni, kifuani na tumboni, yakionesha kifo hakikuwa cha asili.

Hata hivyo, akiwa mahakamani, Jaji Mpaze, ameeleza kuwa mshitakiwa alijitetea kwa madai tofauti akisema alimkuta mke wake huyo, akifanya mapenzi na mwanaume mwingine.

Amesema, Kaunda alibainisha kuwa utetezi huo ulikuwa wa kubuni, kwani mshtakiwa mwenyewe alikiri kuchukua kisu na kumchoma mkewe kutokana na hasira.

Aidha, ushahidi ulionyesha kwamba kabla ya tukio hilo, mshtakiwa aliandika wosia na kuchukua kisu kutoka nyumbani kwake hatua iliyoonesha nia ya makusudi ya kuua.

“Kutokana na ushahidi uliotolewa, ni dhahiri kwamba mshtakiwa alihusika moja kwa moja na mauaji haya,” alisema Jaji Mpaze, kabla ya kutoa hukumu hiyo, tarehe 2 Septemba 2025.

Alisema, ungamo la mshtakiwa mwenyewe lilitosha kuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.

About The Author

error: Content is protected !!