
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi,amezindua rasmi kituo kipya cha Mabasi na Soko la Wafanyabiashara katika eneo la Chuini, Wilaya ya Magharibi A, mkoani Unguja. Anaripoti Zakia Nanga, Zanzibar … (endelea).
Uzinduzi huo umeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya biashara ya usafiri,sambamba na kuinua uchumi wa wananchi katika ngazi ya jamii.
Kituo hicho kipya kinajumuisha soko la kisasa lenye miundombinu bora kwa ajili ya wauzaji wa bidhaa mbalimbali hususani mbogamboga, matunda, nafaka na biidhaa nyingine za kila siku.
Aidha kituo cha mabasi kilichojengwa pembeni ya soko hilo kinatarajiwa kurahisisha safari za wananchi kutoka na kuingia Chuini pamoja na maeneo mengine ya Wilaya ya Magharibi A na jirani.
Kwa mujibu wa viongozi wa serikali za mitaa, kukamilika kwa mradi huu kutasaidia kupunguza msongamano katika meneo ya mjini kuongeza tija kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati. Viongozi hao walimshukuru Rais Mwinyi kwa kuendelea kusikiliza na kutekeleza mahitaji ya wananchi kwa vitendo.
Mradi huu umefadhiliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mpango wa kuimarisha huduma za kijamii na unatarajiwa kutoa ajira mpya, kuongeza mapato ya wafanyabiashara na kuchochea ukuaji wa uchumi katika Mkoa wa Mjini Magharibi.
Uzinduzi huu unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali kuendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi kwa njia ya vitendo na maendeleo jumuishi.
ZINAZOFANANA
Msako wa magari yenye namba za usajili SSH 2030 wasaka 10 Dar
Matibabu bure ya Moyo, Figo na Sukari kwa wasiojiweza sio kila mtu – Samia
Askari afariki kwa kushambuliwa na chui