August 10, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Samia achukua fomu ya urais, asindikizwa na wajumbe wa Kamati Kuu

 

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza, Balozi Emmanuel Nchimbi, wamechukua fomu za uteuzi katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), mjini Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Katika hafla hiyo, iliyofanyika tarehe 9 Agosti, maelfu ya watu wamejitokeza kuwaunga mkono wagombea hao.

Chama tawala nchini Tanzania, kilipitisha azimio la kumteua Rais Samia na Balozi Nchimbi, katika Mkutano Mkuu Maalum wa Januari mwaka huu – chombo cha mwisho cha maamuzi.

Naye Dk. Hussein Mwinyi, rais wa sasa wa Zanzibar, alipitishwa kugombea urais Visiwani.

Uamuzi huo ulifanyika mapema kuliko kawaida, na katika mkutano ambao awali haukupangwa kufanya maamuzi hayo katika ajenda zake.

Wote wawili – Samia na Mwinyi – wanamaliza muhura wao wa kwanza wa uongozi mwaka huu; kwa utamaduni wa chama hicho, marais walioko madarakani hawapatiwi ushindani katika kutetea nafasi zao.

Mkutano uliofanya maamuzi ya kupitisha mgombea wake wa urais, ulikuwa na ajenda kuu moja ya kupitisha jina la Makamu wa Mwenyekiti (Bara), ambapo Stephen Wassira, alipitishwa kushika wadhifa huo.

Kampeni za uchaguzi mkuu ujao wa rais, wabunge na madiwani, zinatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

About The Author

error: Content is protected !!