August 7, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Huyu ndiye Job Ndugai

 

ALIYEKUWA Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amefariki dunia jana Jumatano, jijini Dodoma. Ndivyo Tulia Ackson Mwansasu, spika wa sasa wa Bunge, alivyoueleza ulimwengu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tulia hakutaja sababu ya kifo cha mtangulizi wake. Hakutaja ugonjwa uliokuwa unamsumbua. Wala hakutaja hospitali ambayo Ndugai alikuwa akitibiwa.

Aliishia kusema, “…kwa masikitiko makubwa, naomba kutoa taarifa ya kifo cha kiongozi wetu, mwanasiasa mkongwe na Spika mstaafu wa Bunge, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, kilichotokea leo jijini Dodoma.

“Natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa jimbo la Kongwa, Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”

Alisema, mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.

Kabla ya kifo chake, Ndugai aliibuka mshindi katika kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwania ubunge katika jimbo la Kongwa, mkoani Dodoma.

Pamoja na kwamba katika barua yake ya kujiuzulu, Ndugai alitaja sababu ya kufanya hivyo, kuwa ni “uamuzi wake binafsi, uliozingatia maslahi mapana ya Bunge, Serikali na chama chake,” lakini ukweli ni kwamba kilichomuondoa ofisini, ni kuzorota kwa uhusiano wake na Rais Samia Suluhu Hassan.

Alituhumu utawala wa Rais Samia kuingiza nchi kwenye mikopo isiyokuwa na tija na kwamba kuna siku nchi itapigwa mnada kwa madeni.

Kauli yake hiyo, ilitafsiriwa kama ni ukosoaji wa hatua ya serikali ya Rais Samia kuchukua mkopo wa Sh. 1.3 trilioni, kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Rais Samia, haraka alijibu maelezo ya Ndgai, lakini bila kutaja jina na kusema, serikali itaendelea kukopa kwa ajili ya kuleta maendeleo hata kama kuna watu wanatoa kauli za kukatisha tamaa.

Alisema, nchi imekuwa ikikopa tangu utawala wa Mwalimu Nyerere na kushangaa inakuwaje watu wanahoji wakati huu.

Ndugai aliyewahi kuwa naibu spika kati ya Novemba 2010 na Novemba 2015, alihudumu katika nafasi hiyo, kuanzia Novemba 2015 hadi Januari 2022.

Ameondoka ulimwenguni akiwa ameweka historia ya kuwa Spika wa kwanza wa Bunge la Tanzania kujiuzulu wadhifa wake.

Majigambo yake kwamba “Chezea wengine, lakini usimchezee Ndugai,” yaligeuka “Chezea wengine, usimchezee Rais Samia.”

About The Author

error: Content is protected !!