
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetangaza majina ya walioteuliwa kushiriki kura za maoni kwa ajili ya kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Uteuzi huo, umefanyika kufuatia vikao vya juu vya chama hicho, ikiwemo Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), vilivyoketi hadi usiku wa manane, tarehe 28 Julai.
Orodha hiyo ilisomwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, CPA Amos Makalla, ambapo baadhi ya majina maarufu yaliyotarajiwa kurejea hayakuorodheshwa, jambo lililozua mijadala mikubwa miongoni mwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
Miongoni mwa waliokosa kurejea ni kigogo wa siasa na aliyewahi kuwa mgombea urais mwaka 2015, Januari Makamba, jina lake halikurudi katika Jimbo la Bumbuli.
Aliyekuwa mbunge wa Bukoba Mjini na Naibu Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Byabato, naye jina lake halikurudi.
Waziri wa zamani wa ardhi, Anjelina Mabula jimbo la Ilemela, Naibu Waziri wa zamani wa Michezo, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Pauline Gekul- Babati Mjini, na wabunge maarufu Christopher Ole Sendeka (Simanjiro), Seif Gulamali (Manonga), majina yao pia yameondolewa.
Katika Jimbo la Arusha Mjini, aliyekuwa mbunge, Mrisho Gambo naye ametemwa, huku Lengai ole Sabaya, aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, jina lake likiondolewa kwenye Jimbo la Arumeru Magharibi.
Waziri Mkuu wa sasa, Kassim Majaliwa, alitangaza mwenyewe kuwa hatawania tena ubunge katika jimbo la Ruangwa.
Rais wa klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, ambaye alikuwa akitazamiwa kugombea jimbo la Kigamboni, jina lake halikurudi na badala yake watu sita wamepitishwa kuwania nafasi hiyo.
Majina hayo, ni Ponela Mtei, Habib Mchange, Allan Sanga, Ally Mandai, Francis Elias na Henjelewe.
Aliyekuwa Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajina, naye hayupo katika orodha ya wagombea. Gwajima hakuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
Katika jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina, ameondolewa katika kinyang’anyiro hicho, huku majina saba yakipitishwa kugombea wadhifa huo.
Mpina aliwahi kutajwa na Rais Samia Suluhu Hassan kama “mbunge wa taifa” kutokana na namna alivyokuwa akieleza matatizo ya wananchi kwa ukosoaji wa aina yake hadharani.
Hatua ya kutomrejesha imeibua tafsiri tofauti kuhusu mwelekeo wa chama kuelekea uchaguzi mkuu huu.
Jerry Muro, mwanahabari, msemaji wa zamani wa Yanga na aliyewahi kuwa Mkuu wa wilaya, amepitishwa kugombea jimbo la Hai.
Mtangazaji maarufu wa michezo, Shaffih Dauda, jina lake limepita katika Jimbo la Temeke, na Jemedari Said ametajwa kugombea Jimbo la Mtama.
Hashim Ibwe atapeperusha bendera ya CCM katika Jimbo la Mwanga, Mtangazaji wa zamani wa BBC, Salim Kikeke, amepitishwa kugombea Jimbo la Moshi Vijijini. Katika Jimbo la Kigoma Mjini, Baruhani Muhuza na Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo, wamepitishwa kuwania nafasi hiyo.
Mkuwe Issale “Mamybaby, mtangazaji wa Clouds fm amepitishwa kuwania viti maalumu Tabora, kama ilivyo kwa Jesca Magufuli, mtoto wa rais wa awamu ya nne, John Pombe Magufuli aliyepitishwa kupitia Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa.
Mtoto wa Rais Samia, Wanu Hafidh Ameir amepitishwa jimbo la Makunduchi na Mkuu wa mkoa wa zamani mweye ‘vituko’, Agrey Mwanri amerejea tena kupitia Jimbo la Siha.
Familia ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete imeendelea kuwa na ushawishi ndani ya CCM. Mke wake, Salma Kikwete, amekuwa mgombea pekee katika Jimbo la Mchinga, Lindi, huku mtoto wao, Ridhiwani Kikwete, akipitishwa peke yake Jimbo la Chalinze.
Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko, naye hakuwa na mpinzani katika Jimbo la Bukombe. Katika visiwa vya Zanzibar, Hemed Abdulla ametajwa kama mgombea pekee Jimbo la Kiwani, huku Jimbo la Ole likiwa na majina mawili yaliyopitishwa – Ali Salim Ali na Amour Kassim.
Majina mengine yaliyovuta hisia ni la Daniel Chongolo, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, na Deo Sanga waliopitishwa kuchukua fomu Jimbo la Makambako, ambapo Sanga anatetea nafasi yake. Wilson Mahera, aliyekuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, amepitishwa kugombea Jimbo la Butiama.
William Lukuvi, mmoja wa wanasiasa wakongwe zaidi wa CCM, amerudishwa kugombea Jimbo la Isimani kwa mara ya saba mfululizo. Lukuvi ana rekodi ya kuwa bungeni kwa miaka 30 sasa. Job Ndugai, Spika wa zamani aliyejiuzulu baada ya kutofautiana na Rais Samia, amerejeshwa jimbo la Kongwa, dodoma.
Katika hali isiyo ya kawaida, baadhi ya waliokuwa wabunge wa CHADEMA na waliorejea CCM, nao wamepita katika mchujo wa chama hicho. Jesca Kiishoa, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia CHADEMA, ameteuliwa kugombea Jimbo la Iramba Mashariki.
Ester Bulaya, mmoja wa wanasiasa waliokuwa maarufu CHADEMA, ametajwa miongoni mwa majina matano yaliyopitishwa kugombea Jimbo la Bunda Mjini.
Wengine waliokuwa upinzani pamoja na Peter Msigwa, ambaye amepitishwa kugombea katika jimbo la Iringa Mjini, ni Ester Matiko, anayegombea Tarime Mjini.
ZINAZOFANANA
CCM ‘iwachinje’ wanaonunua ubunge
Kampeini uchaguzi mkuu kuanza 28 Agosti
CCM kufanya marekebisho madogo ya Katiba