
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) leo kinaketi mjini Dodoma kwa ajili ya kuchuja majina ya wanachama wake walioomba kukiwakilisha chama hicho katika nafasi za ubunge na uwakilishi, kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakaofanyika Oktoba 29. Anaripoti Mwandishi Wetu, Darbes Salaam … (endelea).
Jana Jumamosi, CCM kilifanyia marekebisho kile kifungu cha Katiba kilichokuwa kimeweka ukomo wa majina matatu tu yatakayorudishwa kwa wanachama katika kila jimbo ili kupigiwa kura za maoni, ambapo sasa imeainishwa kwamba Kamati Kuu inaweza kurudisha majina zaidi ya matatu kutegemea na mahitaji ya kila jimbo.
Wakati wa kuchuja majina ya watia nia, sifa za msingi zitakazozingatiwa ni Pamoja na kuwa mwanachama mwaminifu na mtiifu wa CCM, mchapa kazi, mwadilifu, na mtu anayekubalika kwenye jamii katika eneo la ubunge au uwakilishi analogombea.
Aidha, makosa yanayoweza kusababisha mwana CCM kutoteuliwa kugombea ubunge au uwakilishi pamoja na sababu zingine, kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kuwashawishi wajumbe kukuchagua ni kosa kubwa pengine kuliko makosa mengine yote.
Kwa miaka mingi CCM kimejipambanua kupiga vita aina zote za rushwa katika kutafuta uongozi, na kina uvumilivu sifuri kwa mwanachama wake yeyote anayebainika kutumia rushwa kutaka kuchaguliwa si katika ubunge na uwakilishi pekee, bali katika nafasi zote za uongozi ndani ya chama hicho.
Ni matumaini ya wana CCM wengi kwamba viongozi wa juu wa chama hicho watakuwa wakali kama upanga dhidi ya watia nia wote waliobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kununua wajumbe watakaopiga kura za maoni majimboni.
Hata hivyo, katika siku za karibuni tuhuma za kuwepo watia nia wanaonunua wajumbe zimesikika maeneo mengi ya nchi yetu, hali ambayo siyo njema kwa CCM, kwani inaweza kusababisha chama hicho kupata wagombea dhaifu na wasiokubalika kwa jamii.
Kwa mfano, mtia nia mmoja katika moja ya majimbo ya wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga amegawa pikipiki, baiskeli na fedha taslimu kwa wajumbe wenye sifa za kupiga kura za maoni, katika kipindi hiki cha kutafuta wagombea ubunge na uwakilishi, kinyume kabisa na kanuni za CCM.
Imeelezwa kwamba mtia nia huyo amefanya hivyo bila kuwahusisha viongozi wa chama wilayani humo, kitendo ambacho kimetafsiriwa na wana-CCM wenzake kuwa rushwa ya wazi wazi.
Katika mazingira yanayotia nguvu tuhuma ya rushwa dhidi ya mtia nia huyo, imedaiwa kuwa pikipiki hizo zimetolewa kwa kubagua viongozi, kwamba baadhi wamepewa na wengine kunyimwa bila kuwepo maelezo ya msingi huku kadi za pikipiki hizo zikisalia mikononi mwa mbunge huyo.
Imeelezwa zaidi kuwa hata umiliki wa pikipiki hizo siyo wa CCM bali ni wa mbunge huyo kwani zimesajiliwa kwa jina la kampuni yake na kwamba amezigawa kwa viongozi hao wa CCM kama kishawishi cha kupigiwa kura.
Utaratibu wa CCM wa kutoa misaada kwa chama unafahamika ambapo mtu anayetaka kukisaidia chama anatakiwa kupeleka msaada huo kwa katibu wa wilaya ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuamua viongozi wa kuwapa, sio kama alivyofanya mtia nia huyo.
Taarifa kutoka jimboni humo zimefichua zaidi kwamba mtia nia huyo amewanunulia baiskeli baadhi ya wenyeviti na makatibu wa matawi ya chama hicho kwa kutumia utaratibu ule ule wa kutopitisha msaada huo kwenye chama na kwa kuchagua watu anaowataka.
Vitendo hivyo vinakwenda kinyume na msimamo wa miaka mingi wa chama na viongozi wa juu wa CCM wa kukataza vitendo vya rushwa kwa wanaotafuta uongozi wa kuchaguliwa katika chama na katika serikali.
Imeelezwa kwamba malalamiko dhidi ya mtia nia huyu yamefikishwa kwenye ngazi zote za uongozi wa CCM, kuanzia wilaya, mkoa na taifa.
Bila shaka kikao cha NEC kitasimamia kwa nguvu zote msimamo wa wa miaka mingi wa CCM kwa kutorudisha jina la mtia nia huyu, na wengine wote waliobainika kufanya vitendo kama hivyo katika majimbo mbalimbali nchini ili kulinda heshima na taswira yake njema kwa umma wa watanzania.
ZINAZOFANANA
Kampeini uchaguzi mkuu kuanza 28 Agosti
CCM kufanya marekebisho madogo ya Katiba
Malecela atajwa kuwa mkombozi jimbo la Dodoma