
MGOMBEA wa Ubunge wa jimbo la Msalala, wilayani Kahama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), (jina linahifadhiwa) anadaiwa kugawa pikipiki kwa baadhi ya viongozi wa kata wa chama hicho ikiwa ni kishawishi cha kumpigia kura kwenye kura za maoni za kuwania ubunge. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kahama, Shinyanga … (endelea).
Kitendo hicho kimelalamikiwa vikali na watia nia wenzake katika jimbo hilo wakidai kuwa hiyo ni rushwa ya dhahiri kwani pikipiki hizo zimetolewa wakati huu ambao chama hicho kinaendelea na taratibu za uchaguzi wa ndani kusaka wagombea wake kwenye nafasi za ubunge, Uwakilishi na udiwani.
Katika kuthibitisha tuhuma zao dhidi ya mgombea huyo, baadhi ya watia nia waliozungumza na gazeti hili wameeleza kuwa pikipiki hizo hazitambuliwi na CCM kwani zimesajiliwa kwa jina la kampuni ya mgombea huyo huku kadi za pikipiki hizo zikisalia mikononi mwake.
Wameeleza zaidi kuwa mgombea huyo amegawa pikipiki hizo kwa kuchagua viongozi wa CCM anaoona wapo upande wake na kuwanyima wengine ambao hana uhakika ya uungaji mkono wao kwenye harakati zake za kugombea tena jimbo hilo.
“Huu siyo msaada bali ni rushwa ya wazi kabisa kwa sababu taratibu za kutoa msaada kwenye chama zinajulikana, kwamba mtu anayetaka kusaidia chama chetu anatakiwa kupeleka huo msaada kwa katibu wa chama wa wilaya ili huo usajiliwe kwenye chama na kisha katibu na wasaidizi wake wataamua maeneo na viongozi wa kupewa, siyo mtoaji achague watu wake wa kuwapa,” alifafanua mtia nia huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
“Halafu hao viongozi wa CCM wa kata aliowapa pikipiki hajawapa kama viongozi wa chama bali kawapa wao kama wao, yaani kama watu binafsi kwa sababu kadi za pikipiki hizo hazijaandikwa CCM bali zimesajiliwa kwa jina la kampuni yake inayoitwa Iddcon, kwa maana hata wakiacha madaraka yao wataondoka na pikipiki hizo”, alifafanua mtia nia huyo.
Aidha, habari zaidi zimefichua kuwa mgombea huyo amewanunulia baiskeli baadhi ya wenyeviti na makatibu wa matawi ya chama hicho tawala katika jimbo lake kwa utaratibu ule ule aliotumia kugawa pikipiki na katika kipindi hiki cha uchaguzi wa ndani ya CCM.
Katika hatua nyingine katibu wa mbunge huyo, ameonekana akiwagawia fedha taslimu mabalozi kadhaa wa CCM aliowakusanya kutoka kata mbalimbali za jimbo hilo, huku akiwalisha kiapo cha kutomsaliti mbunge huyo anayetetea kiti chake.
Hayo yamo kwenye video iliyosamabaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ambayo inamuonesha katibu huyo wa mbunge akizungumza na mabalozi hao kwa kirefu kuhusu masuala ya uchaguzi wa ndani ya chama hicho na baadaye kuwalisha kiapo cha kutomsaliti mgombea huyo, huku akiwasindikiza kwa minoti bwerere.
Alipohojiwa kuhusu video hiyo pamoja na tuhuma za rushwa za pikipiki na baiskeli zinazomkabili mgombea huyo, katibu wa mbunge huyo alithibitisha kuwa ni kweli anayeonekana kwenye video hiyo ni yeye mwenyewe huku akijitetea kuwa hiyo haikuwa rushwa bali ni ahadi ya mbunge kwa wananchi wake.
“Mimi nilitumwa kwenda kukabidhi msada wa fedha ambazo mabalozi hao walimuomba mheshimiwa mbunge kwa ajili ya mradi wao wa kiuchumi, hizo fedha unazoziona ni ahadi ya mbunge kwa viongozi hao wa chama, siyo rushwa kama wanavyosema watu, kwani kwa sasa mbunge haruhusiwi kutekeleza ahadi zake kwa wananchi wa jimbo lake? alihoji katibu huyo.
“Hata hizo pikipiki na baiskeli ni kweli ametoa lakini zilikuwa ni ahadi za mbunge kwa viongozi wa chama chetu, siyo rushwa”, alifafanua katibu huyo.
ZINAZOFANANA
NBC yakutana na wateja wake wakubwa Arusha, yajadili fursa, ufanisi wake
Zanzibar yatajwa kughairishwa Kamati Kuu CCM
Polepole avunja mwiko, azungumza