
Humphrey Polepole
HUMPHREY Polepole, aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) ya chama kilichoko Ikulu, amekosoa utaratibu uliompa Rais Samia Suluhu Hassan, tiketi ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Anasema, utaratibu uliotumika kumchagua Rais Samia na Dk. Emmanuel Nchimbi, kama wagombea wa urais na mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, umevunja Katiba.
Alisema, uchaguzi huo, ulikiuka desturi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), zinazokifanya chama hicho kuendelea kuwa imara.
“Mimi sikuwapongeza na sitawapongeza. Unapongezaje mchakato ambao haukuwa halali? Mimi nataka kwenda mbinguni. Huu mchakato wa kupata mgombea tumeukosea,” alieleza.
Alisema, “Naomba ni-conclude kwamba, kwa desturi ya CCM, mwaka huu 2025, tunapaswa kuwa na wagombea wengine wa urais na makamu wake.”
Pendekezo la CCM kumpitisha Samia kuwa mgombea wake mapema, liliridhiwa na wajumbe wa mkutano mkuu, baada ya Jakaya Kikwete, kueleza kuwa halima shida.
Lakini Polepole akahoji, “Huyu Kikwete alitumwa na nani?”
Ameongeza, “Na hapa nitawasema, wale wanaokuwaga wenyeviti wa kamati za maadili wanajua… Hili ni gumu kidogo.. unajua wakati mwingine unatakiwa ubomoe ili ujenge.
“Sasa, huu mchakato wa kupata wagombea kwa kweli tumeukosea, nimeongea na mzee mmoja, ndugu yangu, rafiki yangu nikamweleza, akasema pale bwana tulichemka.. Lakini sasa tunatokaje?
“Nikamwambia, kukiri tatizo ni sehemu ya suluhu. Nendeni mkarekebishe, ili mkipatie heshima chama chetu, alisema Polepole.
Akizungumza katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu aachie wadhifa huo wiki iliyopita,
Polepole anasema, “Watu wanataka uwabembeleze, uwaombe, uwabembeleze, uwaombe, lakini wao wakiwa na shida watakutafuta.”
Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, alijiuzuru Jumatatu iliyopita akidai hawezi kuwa sehemu ya serikali isiyojali misingi ya haki, sheria na katiba ya nchi.
Usiku wa kuamkia leo, Polepole alitoa taarifa katika mtandao wake wa Instagram kwamba dada yake alivamiwa na watu wasiojulikana walioingia nyumbani kwake kwa kuruka ukuta.
Katika hotuba yake aliyoitoa leo kupitia mtandao wa Facebook, Polepole amesema, anapinga masuala ya utekeaji na kuwa dada yake ametekwa na kuumizwa.
Hata hivyo, kamanda wa kanda maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema kuwa walifatilia tukio hilo, na kuwa uchunguzi unaendelea.
Kada huyo wa CCM alidai kitendo hicho kililenga kumtisha asizumgume alichopanga kuzungumza leo na kuapa kufanya hivyo hata ikiwa familia yake yote itatekwa.
Bali Polepole anafahamika kwa kutetea sera na utendaji wa CCM na serikali ya Rais John Magufuli, hata pale kulipokuwa na utata mkubwa wa masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu, utekaji na kuwaweka watuhumiwa mahabusu kwa muda mrefu.
Aidha, Polepole alikuwa mtetezo wa kufunguliwa kesi nzito za uhujumu uchumi kwa baadhi ya wananchi na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020.
Anajulikana pia kwa kauli tata au ahadi za CCM na serikali ambazo hazikuwa kutekelezwa, kama vile ujenzi wa barabara za juu (fly overs) katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, “Linalongojewa sasa ni kuona mustakabali wake kisiasa baada ya kujiuzulu ubalozi na nafasi nyingine za umma.”
ZINAZOFANANA
Polisi wafunguka sakata la kuchukuliwa dada yake Polepole
Rostam: Sekta binafsi iko tayari kuisadia ukuaji wa uchumi wa dola trilioni moja
Mohamed Abdulrahman: Gwiji la utangazaji DW laanguka