July 16, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mohamed Abdulrahman: Gwiji la utangazaji DW laanguka

Mohamed Abdulrahman

 

ALIYEKUWA mhariri na naibu mkurugenzi wa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (Deutsche Welle), Mohamed Abdulrahman, amefariki dunia nyumbani kwake mjini Cologne. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mohamed amefariki dunia nyumbani kwake mjini Cologne, akiwa ameacha alama isiyofutika nyuma yake katika tasnia ya habari.

akiwacha nyuma yake alama isiyofutika kwenye tasnia ya uandishi wa habari.

Kwa mujibu wa DW Kiswahili, jina kamili la Mohamed, ni Mohamed Abdulrahman Mkufunzi. Ikasadifu kwamba jina la babu yake, Mkufunzi, ambalo linamaanisha fundi anayefundisha wengine, ikawa ndiyo khulka na mwenendo wake kitaaluma na kikazi.

Watangazaji wengi waliopo Idhaa ya Kiswahili ya DW na hata idhaa nyengine za kimataifa ni matokeo ya moja kwa moja ya ukufunzi wake na hawafichi jinsi walivyofundika chini ya ufundi wa ‘mkufunzi’ huyu.

Bruce Amani aliyejiunga na DW mwaka 2011, anamtaja kama mtu aliyempokea na kumfundisha kazi kwa ufanisi mkubwa.

“Nilikutana na Mohamed Abdulrahman, nilipotembelea Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani. Tulizungumza mengi. Baadaye tuliondoka wote studio na akanisindikiza hadi kituo cha treni, nikielekea Ubelgiji,” anaeleza Saed Kubenea, mwandishi wa habari na mkurugenzi wa magazeti ya MwanaHALISI.

Anasema, “baada ya kuondoka Ujerumani mwaka 2018, niliendelea kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na Mohemmed. Kuna wakati niliwahi kumuomba atuandikie makala kwenye magazeti yetu. Alikubali.”

Kubenea anasema, anamkumbuka Mohamed Abdulrahman, kama mwandishi wa habari mahiri, mnyenyekevu, jasiri na msanifu wa kweli wa lugha ya Kiswahili.

“Namuombea kwa Mungu, ndugu yetu, mwandishi wa habari mwenzetu mwandamizi na mtangazaji huyu mahiri wa kimataifa,” anaeleza Kubenea.

Kwa mujibu wa DW Kiswahili, Mohamed alijiunga na Deutsche Welle mwaka 1980 akitokea nchini Komoro, ambako alikuwa akifanya kazi kwenye shirika la utangazaji la visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi, chimbuko la wazee wake.

Hata hivyo, DW Kiswahili inasema, Mohamed mwenyewe, ni mzaliwa wa Tanganyika ya wakati huo (sasa Tanzania Bara) kwa wazazi wenye asili ya Kizanzibari na Kingazija na alikuja baadaye kuhamia kisiwani Unguja kwa masomo na maisha kabla ya kwenda London, Uingereza, kisha Moscow, Urusi, alikosomea uandishi wa habari.

“Mimi asili yangu ni Mngazija, ni Mtanganyika kwa kuzaliwa, Mzanzibari ikiwa ni chimbuko la mama yangu, na Mtanzania kutokana na Muungano wa mataifa mawili ya Tanganyika na Zanzibar 1964. Lakini zaidi najivunia kuwa Mwafrika,” anaeleza Mohamed kwenye kitabu alichokichapisha baada ya kustaafu alichokipa jina la “Maisha Yangu Ninavyoyakumbuka.”

Lakini leo hii tunapoadhimisha maisha yake baada ya kutangulia mbele ya haki, Mohamed hakumbukwi na wenzake wa DWkwa utambulisho wake huo, bali kwa utambulisho wa kuwa mwandishi bingwa, mahiri na mwenye kipaji cha hali ya juu.

“Kifo cha Mohamed kimenishituwa, kimenifadhaisha sana. Namkumbuka kwa umahiri wake na ukweli kuwa ni yeye aliyekuwa daraja ya mimi kutoka Afrika na kuja hapa kujiunga na DW,” anasema Zainab Aziz aliyefanya kazi na Mohamed kwa zaidi ya miongo miwili.

Miongoni mwa sifa kubwa ambazo Idhaa ya Kiswahili ya DW inajivunia ni msingi wake wa matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu, lakini kwa wengi wanafahamu kuwa mjenzi wa msingi huo alikuwa Mohamed.

Josephat Charo aliyekuwa mmoja wa wasaidizi wawili wa mkuu wa Idhaa hii anakumbuka jinsi Mohamed ‘alivyowanyooshea lugha’ kwenye chumba cha uhariri,

“Ukiwataja watetezi wakubwa wa Kiswahili duniani, Mohamed utamkuta naye yumo. Kwenye mikutano yetu ya uhariri, alikuwa akituelekeza na wakati mwengine hata kutukemea pale anapoona Kiswahili kinatumiwa vibaya. Hakutaka kuona Kiswahili kinachanganywa na lugha nyengine kama vile Kiingereza, kwa mfano,” anaeleza Josephat.

Mohamed alijiunga na DW kama mwanafunzi wa vitendo, akapanda daraja hadi kuwa mtangazaji kamili, akashika wadhifa wa uhariri na hatimaye naibu mkuu wa Idhaa – safari iliyoweka alama ya uandishi, umahiri na wito aliokuwa nao maishani.

Kwake uandishi ulikuwa si sauti tu nyuma ya kipaza sauti cha redio, bali maarifa na muakisiko wa kilimwengu. Ndio maana aliumiliki uandishi na uchambuzi wa masuala ya siasa, michezo na ya kijamii kama vile alivyomiliki hati kwenye maandiko yake.

About The Author

error: Content is protected !!