
BARUA wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Hesron Polepole, ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi yake ya kidiplomasia na uongozi wa umma, akitaja kukosekana kwa uelekeo sahihi katika uongozi wa kitaifa, kufifia kwa maadili na dhamira ya kuhudumia wananchi kama sababu kuu za hatua hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kupitia barua yake aliyomwandikia Rais Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 13 Julai 2025, Polepole amesema amefikia hatua hiyo kwa tafakari ya kina na kwa utulivu wa dhamira, baada ya kushuhudia kwa muda mrefu hali ya mambo ambayo kwa maoni yake “inateteresha maslahi mapana ya Taifa.”
Polepole amehudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Malawi kuanzia Machi 2022 hadi Aprili 2023, na baadaye kuhamishiwa Cuba, akihudumu pia kwa nchi rafiki za Karibe, Amerika ya Kati na baadhi ya mataifa ya Amerika ya Kusini hadi alipojiuzulu Julai 2025. Awali, alikuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 2020 hadi 2022.
Katika barua yake, Polepole amesema: “kwa muda wote wa kuhudumu ndani na nje ya nchi, nimefuatilia kwa karibu na kushuhudia kwa masikitiko makubwa mwelekeo wa uongozi usiojielekeza ipasavyo katika kusimamia haki za watu, amani na kuheshimu watu, kufifia kwa dhamira ya kweli na uwajibikaji wa dhati wa kushughulikia kero na changamoto zao, na kudidimia kwa maadili ya uongozi katika ngazi mbalimbali”.
Akiwa mwanachama wa muda mrefu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Polepole amekosoa mchakato wa uteuzi ndani ya chama hicho kwa mwaka huu, akisema umevuruga misingi ya CCM ya “chama kwanza, mtu baadaye.” Kwa mujibu wake, mwenendo wa sasa wa uteuzi wa wagombea unakiuka utamaduni uliojenga chama hicho katika nyakati mbalimbali.
“Mwanzoni mwa mwaka huu, nilipoona kauli hii (chama kwanza, mtu baadaye) inafanyika vinginevyo, nimejiuliza mara kadhaa ni maslahi ya nani yanapiganiwa wakati huu, mtu, kikundi au Chama Taasisi?” ameandika Polepole.
Licha ya kujiuzulu nafasi zote za kiserikali, Polepole amesema ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida wa CCM, akisisitiza kuwa bado ni mzalendo na raia mwaminifu kwa Tanzania.
Amemshukuru Rais Samia kwa fursa aliyompa na kuhitimisha barua yake kwa imani kuwa siku moja Tanzania itaongozwa kwa misingi ya haki, siasa safi na hofu ya Mungu.
ZINAZOFANANA
Maofisa wa Chadema wazuiliwa kisafiri, Polisi wasema
Maadhimisho ya Nne ya Lugha ya Kiswahili yapokewa kwa bashasha Harare, Zimbabwe
Tundu Lissu akwama Mahakamani