
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwezeshaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Serikali inahitaji vyombo vya habari imara (visivyoionea au kuipendelea) kwa ajili ya kuichagiza gurudumu la maendeleo na utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Anaripoti Salehe Mohamed, Dar es Salaam … (endelea).
Amesema kwa jamii iliyoelimika na kustaarabika mchango wa sekta ya habari ni muhimu kwa ajili ya maendeleo hivyo yoyote anayedharau wanahabari ni mpumbavu.
Prof Kitila, ametoa kauli hiyo leo, tarehe 8 Julai 2025, wakati akizungumza na wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kuhusu kukamilika kwa Dira ya Taifa 20250 (TanzaniaTuitakayo) itakayozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, tarehe 17 Julai, mwaka huu ambayo imebeba mchango wa makundi mbalimbali wakiwemo wanahabari.
Amebainisha kuwa Serikali inapotaka kujipima na kujitathimini kazi inazofanya kwenye jamii huangalia vyombo vya habari kwa kuwa ndiyo kioo chake.
Amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Ilani yake ya 2025-2030 imeainisha umuhimu wa vyombo vya habari katika ustawi wa nchi na kuna majadiliano watafanya ya namna ya kuviimarisha kiuchumi ili vifanye kazi kwa uhuru na ufanisi zaidi.
“Vyombo vya habari ni nyenzo muhimu kwa ajili ya maendeleo, mimi siamini kuwa waandishi si watu muhimu, anayesema au kuwaona hivyo huyo ni mpumbavu. Tunajua kuna shida kwenye vyombo vya habari na tunachotakiwa ni kuviimarisha ili vifanye kazi nzuri zaidi na si kuvibagaza”
“Bila vyombo vya habari imara Serikali haiwezi kupiga hatua, tukiwa na vyombo vya habari vya kupendelea na kunyamazia mambo yasiyofaa maana yake tunaharibu jamii, CCM tunataka huko tunakoelekea tuimarishe vyombo vya habari ikiwezekana kuvipatia fedha (ruzuku) kupitia kodi za wananchi kwa sababu vinafanya kazi nzuri yenye masilahi kwa taifa” amesema.
Naye Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amewataka wananchi kutowapa nafasi watu wanaotaka kuwagawa Watanzania na kushusha heshima ya tasnia ya habari.
“Tunajua kuna watu wanalipwa kutuchafua, wanafanya hivyo ili kututoa kwenye mstari wa maendeleo, ukweli hivi sasa nchi yetu imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali. Tusiwape nafasi” amesema.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa TEF, Absalom Kibanda amesema kuwafananisha waandishi wa habari na ‘toilet paper’ ni kuwakosea heshima na kutothamini mchango wao kwenye jamii.
ZINAZOFANANA
Matokeo ya kitado cha sita ufaulu kuongezeka
Wanaosifia dawa za kulevya kuchukuliwa hatua kali – DCEA
Karia mgombea pekee nafasi ya Urais TFF