July 17, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Julai 11 Mahakama kuamua mapingamizi ya Serikali kesi Lissu

Tundu Lissu akiwa mahakamani

 

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es salaam, tarehe 11 Julai 2025, inatarajia kutoa uamuzi juu ya pingamizi zilizowasilishwa na upande wa Jamhuri katika maombi ya marejeo yenye shauri namba 14496/2025 juu ya mwenendo wa kesi ya uchochezi iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Maombi hayo yalifunguliwa na Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), dhidi ya upande wa Jamhuri ambayo yametokana na shauri namba 8606/2025 ambalo lipo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geoffrey Mhini.

Msingi wa maombi ya mshitakiwa ni kuiomba mahakama hiyo kuitisha rekodi za mwenendo wa shauri hilo tajwa ili liweze kuangalia na kutoa uamuzi kama uendeshwaji wa shauri hilo unafaa au haufai wakihusisha ahirisho la tarehe 2 Juni, mwaka huu ambalo lilikuwa na maombi ya kuficha uhalisia wa mashahidi katika shauri hilo.

Shauri hilo linalosikilizwa na Jaji Elizabeth Mkwizu wakati pande zote mbili zilipofika mahakamani hapo kwa ajili ya maombi hayo kuanza kusikilizwa.

Awali Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga alidai pamoja na maombi hayo kuwepo mahakamani hapo kwa upande wa Jamhuri ulikuwa na pingamizi na aliomba yasikilizwe kwanza kabla ya maombi kuanza kusikilizwa.

Baada ya kudai hayo Wakili wa Lissu, Peter Kibatala aliiomba mahakama iamuru kwamba kwa kuwa vyote vipo pamoja visikilizwe kwa utaratibu mahakama ambao utaelekeza, kwani mazingira ya shauri hilo yanaridhisha shauri la msingi na pingamizi vyote kusikilizwa kwa pamoja.

Wakiwasilisha pingamizi zao upande wa Jamhuri ulidai amri ya kuahirishwa kwa kesi iliyotolewa tarehe 2 Juni, mwaka huu ilikuwa halimalizi kesi kwani wakili wa Serikali aliweka wazi shauri lilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa lakini walikuwa na maombi ambayo yangeweza kuathiri mwenendo wa uendeshwaji shauri tajwa.

Katuga ameleza wazi kuwa shauri lilipangwa kwa ajili ya kuskilizwa lakini kulikuwa na maombi namba 13298/2025 na aliweka mahakama wazi kwamba ombi hilo lingeweza kuathiri mwenendo wa uendeshwaji wa shauri hilo.

Amedai mahakama ilitoa uamuzi kwa sababu haikujua shauri lipo kwa nani na wala hakujua maombi yanahusu nini na kwa kuwa lilikuwa halijatolewa uamuzi ndipo wakili aliiomba mahakama iahirishe shauri hadi maombi hayo yatakayotolewa uamuzi.

Akitoa hoja ya pili Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema alidai maombi hayo yaliyowasilishwa ni ya mchanganyiko yaani wamewasilisha maombi zaidi ya moja ambayo wanahitaji yasikilizwe kwa pamoja maombi ya pamoja.

Mrema amedai maombi yaliyowasilishwa katika mahakama hiyo yanakinzana na kiapo kilichowasilishwa ambacho pia kina mchanganyiko, hivyo mahakama hiyo haiwezi kwenda kwa mchanganyiko kwa sababu ni mahakama ya sheria na sheria hizo ziliwekwa ili zifuatwe.

Walidai Mahakama hiyo haina mamlaka ya kufanya ukatiba wa kifungu cha sheria kama walivyoeleza katika maombi yao, hivyo waliiomba mahakama itupilie mbali maombi ya mahitakiwa kwani hayakuwa na mashiko.

Wakijibu pinzamizi hizo mawakili wa maombaji (Lissu), Paul Kisabo, Peter Kibatala, Jeremiah Mkondesya na Hekima Mwasipu walidai maombi yao hayajaeleza kuhusu mahakama kufanya ukatiba wa kifungu cha sheria namba 188 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) bali wanataka kuangaliwa uhalali wa uendeshwaji wa shauri hilo.

Akisisitiza hilo Mwasipu alidai walichokiomba kwenye ombi la tatu ni kwamba mahakama iweze kutathmini kilichofanyika katika mahakama ya chini kwamba ilikuwa ni halali kwa hakumi kuamua kuahirisha shauri, hivyo ni maombi ambayo yanaendana moja kwa moja na hakukuwa na suala la ukatiba katika maombi hayo.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili Jaji Mkwizu aliahirisha shauri hilo hadi tarehe 11 Julai 2025, kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

About The Author

error: Content is protected !!