June 24, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Bosi Kituo cha Afya Salaaman ashinda kesi mbili za jinai dhidi yake

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachiliwa huru Dk. Abdi Hirsi, Mkurugenzi na mmiliki wa kampuni ya Salaaman Health Services Ltd inayomiliki Kituo cha Afya cha Salaaman (Salaaman Health Centre), baada ya kushinda kesi mbili za jinai alizokuwa amefunguliwa mahakamani hapo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Katika kesi zote mbili Dk Hirsi alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kughushi kinyume na vifungu vya 333(a), 335(a) na 337 na kuwasilisha nyaraka za uwongo kinyume na vifungu 342 na 337 vyote vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, marejeo ya mwaka 2019.

Alikuwa anatuhumiwa kughushi fomu za bima za matibabu za kampuni mbili tofauti kuonyesha kuwa wagonjwa walitibiwa katika kituoni hicho cha afya eneo la Mtaa wa Misheni, Wilayani Nyamagana, jijini Mwanza na, kuwasilisha fomu hizo katika ofisi za kampuni hizo za bima kwa malipo.

Mahakama katika hukumu zake zilizotolewai tarehe 17 Juni, 2025, ambazo gazeti hili imepata nakala ya huku hiyo mapema wiki hii.

Dk. Hirsi ambaye aliwakilishwa na wakili Juma Nassoro amepangua kesi zote, baada ya Mahakama kuridhika kuwa upande wa mashtaka hakuweza kuthibitisha mashtaka dhidi yake.

Katika hukumu ya kesi namba 000019187 ya mwaka 2024 Hakimu Mkazi Mkuu Gwantwa Mwankuga amesema kuwa kulingana na utetezi wa mshtakiwa, inaonekana kulikuwa na nia ovu dhidi ya mshtakiwa katika kufunguliwa kesi hiyo.

Katika kesi hiyo Dk. Hirsi alikuwa akikabiliwa na mashtaka sita, matatu ya kughushi na matatu ya kuwasilisha nyaraka za uwongo, akidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Novemba 2016 na Januari 2017, akiwa mkurugenzi na mmiliki wa kituo hicho.

Alidaiwa kuwa aliandaa fomu za bima ya afya ya kampuni ya AAR Insurance (T) Limited, za wagonjwa watatu tofauti kwa kusudi la kuonesha kuwa walipata matibabu katika kituo hicho.

Pia alidaiwa kuwa aliwasilisha fomu hizo katika ofisi za kampuni ya AAR Insurance, Mlimani City, wilayani Kinondoni-Dar es Salaam, mashtaka ambayo aliyakana.

Upande wa mashtaka uliita mashahidi tisa lakini Hakimu Mwankuga amesema kuwa ushahidi pekee unaomhusisha Dk. Hirsi na makosa hayo ni maelezo kwamba ndiye mkurugenzi na mmiliki wa kituo hicho.

Amesema kuwa hakuna hata shahidi mmoja aliyesema kuwa mshatakiwa ndiye aliyesaini nyaraka hizo na kwamba hata mtaalamu wa maandishi alisema kuwa hakufanya uchunguzi wa maandishi au saini katika fomu hizo.

Hakimu Mwankuga amesisitiza kuwa mpelelezi wa kesi na mtaalamu wa maandishi walieleza kuwa mshatakiwa hakusaini nyaraka hizo na hivyo haikuweza kuthibitishwa kuwa mwandiko unaoonekana katika fomu hizo ni wa mshtakiwa.

Amefafanua kuwa madai tu ya mpelelezi kuwa alielezwa na afisa wa AAR kuwa mshtakiwa ndiye aliyewasilisha nyaraka hizo ofisini kwao hayaungwi mkono kutokana na kwamba afisa huyo wa AAR hajatajwa wala kuitwa mahakamani kutoa ushahidi.

“Hakuna dispatch (kitabu cha kupokelea nyaraka) kilichowasilishwa mahakamani kuunga madai kuwa mshatakiwa aliwasilisha fomu hizo katika ofisi za AAR kwa ajili ya malipo”, amaesema Hakimu Mwankuga.

Amesema kuwa Dk. Hirsi katika ushahidi wake na kilelelezo cha ushahidi alichokiwasilisha mahakamani, alidai malipo kutoka AAR katika kesi ya kibiashara namba 91 ya mwaka 2016 ambayo baadaye yalisuluhishwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (Tira) Bhgaoyo Saqware ambaye baadae ndiye amekuwa mlalkamikaji katika kesi hii ya jinai.

“Maelezo hayo ambayo hayakupingwa huleta hitimisho kuwa kulikuwa na nia ovu dhidi ya mshtakiwa”, amesema Hakimu Mwankuga na kusisitiza kuwa mshtakiwa ameweza kuibua mashaka dhidi ya ushahidi wa upande wa mnashtaka.

Hakimu Mwankuga amesema kuwa kwa sababu zilizotangulia mshtakiwa hana hatia.

“Hivyo ninamwachilia huru mshtakiwa,” amesema Hakimu Mwankuga.

Katika kesi nyingine, kesi ya jinai Na.2496/2024, Dk. Hirsi na kampuni yake hiyo, alikuwa akikabiliwa na mashtaka mawili, moja la kughushi na lingine la kuwasilisha nyaraka za uwongo, akidaiwa kutenda makosa hayo tarehe 1 na 19 Mei 2018..

Alidaiwa kuwa kwa nia ya kufanya ulaghai aliandaa nyaraka za uwongo zilizoitwa Fomu ya Madai, za kampuni ya Strategis Insurance (TZ) Ltd, kuonesha kuwa wagonjwa wawili walipata huduma ya matibabu na kulazwa katika kituo hicho, kwa siku sita.

Katika shtaka la pili alidaiwa kuwa aliwasilisha fomu hizo katika ofisi za kampuni hiyo, Masaki, Wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Upande wa mashtaka uliwaita mashahidi 13 na mshtakiwa, Dk Hirsi alijitetea mwenyewe.

Katika utetezi wake, Dk. Hirsi alikana kuwa na daktari ambaye majina yake yalionekana katika fomu zinazodaiwa kughushiwa na hata hivyo pia hazikuwa na mhuri wa kituo hicho cha afya.

Alidai kuwa baada ya kampuni ya Strategis kukatisha mkataba wa huduma hiyo, walimkamata mtu mmoja aitwaye Musa Eliasi aliyempa kaka yake kadi yake ya bima aliyoiktumia kupata matibabu kituoni hapo.

Pia alieleza kuwa mtu huyo alishtakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, na aliwasilisha mahakamani hati ya mashtaka, mwenendo na hukumu ya kesi hiyo zilizopokewa kama vielelezo vya utetezi wake katika kesi hii.

Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi, aliyesikiliza kesi hiyo katika hukumu yake amesema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa, kwani hakuna ushahidi wowote kuonesha kuwa ndiye aliyeziandaa na alisaini fomu hizo wala hati za malipo zilizowasilishwa Strategies.

Amesema kuwa hata waajiriwa wa kampuni ya Strategis walikana kumuona Dk. Hirsi akipeleka ofisini kwao fomu za madai ya malipo.

Pia Hakimu Mushi amesema kuwa licha ya fomu hizo kutokuwa na mhuri wa hospitali hiyo hata baada ya kumaliza ushahidi wake upande wa mashtaka bado jina la mtu aliyesaini fomu hizo halikuweza kufahamika.

“Hivyo ninaawaachilia huru mara moja”, ameasema Hakimu Mushi.

About The Author

error: Content is protected !!