June 21, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

CCM yalaumiwa kwa kutochukua hatua kikokotoo cha wastaafu

Waziri Kivuli wa Uchukuzi, Halima Nabalang’anya

 

CHAMA cha ACT Wazalendo kimelaumu Serikali kwa kushindwa kusikiliza kilio cha wastaafu kuhusu marekebisho ya kikokotoo cha mafao ya pensheni kwa watumishi wa umma na sekta binafsi. Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri Kivuli wa Uchukuzi, Halima Nabalang’anya, katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya chama hicho Magomeni, Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa Nabalang’anya, mfumo wa sasa wa kikokotoo unaotumika kwa wastaafu wanaochangia mifuko ya PSSSF na NSSF unawapunja kwa kiwango kikubwa, huku akibainisha vipengele vinne kandamizi vinavyochangia hali hiyo.

“Mfumo huu unapunguza mafao kwa wastani wa asilimia 60 kutokana na asilimia ya malipo, kutumia kipimo cha 1/580 badala ya 1/540 kunapunguza mafao kwa zaidi ya asilimia 7, na pia kutumia wastani wa mishahara mitatu ya mwisho badala ya mshahara wa mwisho kunapunguza mafao kwa asilimia 7.2. Aidha, kupunguza muda wa kuhudumu kwa pensheni kutoka miaka 15-5 hadi 12.5 kunazidi kuwanyima haki wastaafu wetu,” alisema.

ACT Wazalendo imesema hatua hii siyo tu inawapunja wastaafu, bali pia inaendeleza ubaguzi kati ya wafanyakazi wa sekta binafsi na wale wa serikali, hasa wanaohudumiwa na mifuko tofauti ya hifadhi ya jamii.

Chama hicho kimetaka kurejeshwa kwa mfumo wa zamani wa kabla ya mwaka 2018, uliokuwa unatoa mafao ya mkupuo kwa asilimia 50 na kutumia kikokotoo cha 1/540, huku mstaafu akipewa mafao kulingana na umri wake wa kuishi badala ya muda uliodhibitiwa.

Pia ACT Wazalendo imekosoa Serikali kwa kushindwa kumaliza deni la wafanyakazi waliostaafu kabla ya mwaka 1999. Nabalang’anya amesema kuwa katika deni la trilioni 4.46 ambalo PSSSF inadai, Serikali imelipa trilioni 2.18 pekee, hali inayosababisha mfuko huo kushindwa kulipa wastaafu kwa wakati na kushindwa kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo.

“Haiwezekani Serikali inapanga kulipa bilioni 630 tu. ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kulipa deni lote kupitia mfumo wa hati fungani, ili kuimarisha PSSSF na kuhakikisha wastaafu wanapata haki yao kwa wakati,” alisisitiza Nabalang’anya.

Kauli hii inakuja wakati kukiwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wastaafu na vyama vya wafanyakazi kuhusu hali ngumu ya maisha baada ya kustaafu na ukosefu wa mfumo wa hifadhi ya jamii unaolinda utu wa wazee.

About The Author

error: Content is protected !!