May 19, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali kufikisha mashahidi 15 kumkabili Lissu kizimbani

Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema akiwa mahakamani Kisutu

 

UPANDE wa mashtaka katika kesi ya uchochezi na kutoa taarifa za uongo inayomkabili Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umepanga kupeleka mashahidi 15 na vielelezo tisa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Wakili wa Serikali Mkuu, Nasoro Katuga alieleza hayo leo tarehe 19 Mei 2025, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.

Katuga amedai kuwa idadi ya mashahidi aliyoitaja ni iliyopo kwa sasa lakini kuna uwezekano wakapata mashahidi wengine na kuwa wataifahamisha mahakama iwapo kutakuwa na mabadiliko.

Akisoma maelezo hayo ya awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawabu Issa alidai kuwa katika shtaka la kwanza tarehe 3 Aprili 2025, Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya Lissu alichapisha kupitia mtandao wa Youtube maneno yanayosema “uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 wagombea wa CHADEMA walienguliwa kwa maelekezo ya Rais” wakati akijua sio kweli.

Tawabu amedai kuwa tarehe 3 Aprili 2025, mkoani Dar es Salaam, Lissu kupitia mtandao wa Youtube alichapisha taarifa inayosema “Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi” wakati akijua sio kweli.

Vilevile katika shitaka la tatu Tawabu amedai kuwa tarehe 3 Aprili 2025, mkoani Dar es Salaam akiwa na nia ya kudanganya umma, Lissu alichapisha katika mtandao wa Youtube maneno yanayosema “Majaji ni ma-CCM hawawezi kutenda haki wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa mahakama ya rufaa” wakati akijua tarifa hiyo ni uongo na inapotosha umma.

Lissu amekana maelezo yote isipokuwa taarifa zake binafsi ambapo amedai kuwa maelezo yaliyotolewa si ya kweli lakini maneno yake aliyoyasema si ya uongo.

Aidha, Wakili wa utetezi ameomba mahakama iamuru upande wa mashtaka wawapatie maelezo ya mtu aliyepeleka maelezo kusababisha kesi hiyo kufunguliwa ambapo Hakimu Mkazi Mwandamizi Mhini aliuagiza upande wa mashtaka kutekeleza ombi hilo.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 2,2025 itakapoanza kusikilizwa mahakamani hapo.

About The Author

error: Content is protected !!