May 14, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Suzan Kiwanga ang’oka Chadema na wengine 50

 

JUMLA ya wanachama 50 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka wilaya mbalimbali mkoani Morogoro wamejiondoa rasmi ndani ya chama hicho, wakilalamikia kupotea kwa mwelekeo wa kisiasa na sintofahamu juu ya ushiriki wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Anaripoti Yusuph Kayanda, Morogoro … (endelea).

Wanachama hao, waliokuwa wakihudumu katika nafasi mbalimbali, wameeleza kuwa hawaridhishwi na msimamo wa baadhi ya viongozi wa chama wanaosisitiza kuwa “Hakuna Marekebisho ya Katiba, Hakuna Uchaguzi” (No Reform, No Election), hali wanayodai inahatarisha mustakabali wa kisiasa na maendeleo ya wananchi.

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mlimba na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Suzan Kiwanga, amethibitisha kujivua nafasi zake zote za chama akieleza kuwa haoni tena dira ya kweli ya kisiasa ndani ya CHADEMA.

Naye David Chiduo, Mwenyekiti mstaafu wa Chadema Jimbo la Kilosa aliyedumu ndani ya chama tangu 2012, amesema: “Nilijiunga kwa lengo la kutatua changamoto za wananchi kupitia siasa. Kama chama hakiendi uchaguzi, ndoto hizo haziwezi kutimia.”

Kwa upande wake, Magreth Raphael, aliyewahi kuwa Diwani wa Viti Maalum na hadi sasa akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Wilaya ya Kilombero, amesema amevunjika moyo na namna wanachama waandamizi wanavyopuuzwa licha ya kujitolea kwa miaka mingi.

Wanachama hao wameeleza pia kuwa wamekuwa wakikejeliwa, kudharauliwa na kuitwa majina ya kubeza wanapotoa maoni ya kukosoa uongozi wa juu wa chama, hali iliyochochea maamuzi yao ya kujiondoa.

About The Author

error: Content is protected !!