
Naibu Katibu Mkuu CHADEMA, Amani Golugwa
OFOSI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeelezwa kutengua uteuzi wa viongozi wanane wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), waliothibitishwa na Baraza Kuu la chama hicho mnamo Januari 22, 2025, kutokana na kutokuwepo kwa akidi halali ya kikao hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa na Lembrus Mchome, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, akipinga uhalali wa kikao hicho kwa madai kuwa akidi ya wajumbe haikufikiwa.
Viongozi waliotenguliwa ni pamoja na John Mnyika, Katibu Mkuu, Amani Golugwa, Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Ally Ibrahim Juma, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar).
Wengine ni Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh, na Dk. Rugemeleza Nshala (Mwanasheria Mkuu wa chama) ambao ni Wajumbe wa Kamati Kuu Msajili ametoa maelekezo kwa CHADEMA kuitisha Baraza Kuu jipya lenye akidi stahiki, ili kufanikisha uteuzi upya wa viongozi hao kwa mujibu wa Katiba ya chama, Sheria ya Vyama vya Siasa, na kanuni zinazohusika.
Katika mafunzo ya viongozi wa BAWACHA na BAVICHA Kanda ya Kusini mnamo Machi 25, 2025, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alieleza kuwa akidi ya kikao hicho ilikuwa sahihi, kwa kuwa kilihusiana na uteuzi wa kawaida si mabadiliko ya katiba wala uchaguzi.

Mnyika alisema kikao hicho kilikuwa na zaidi ya asilimia 50 ya wajumbe, akisisitiza kuwa hiyo ilikuwa akidi ya kutosha kwa mujibu wa taratibu za ndani. Hata hivyo, Ofisi ya Msajili, baada ya kupitia malalamiko ya Mchome na majibu ya CHADEMA, imeafiki kwamba akidi haikufikiwa na hivyo uamuzi wa kikao hicho si halali.
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani ya CHADEMA kilichozungumza na tovuti hiyo, uamuzi wa msajili ni “taarifa mbaya sana kwa chama” na unaweka chama katika hatari ya kisheria iwapo hakitatekeleza maelekezo hayo. Chanzo hicho kimesema kuwa viongozi wengi kwa sasa wako mikoani wakitekeleza operesheni ya “No Reforms, No Election.”
Aidha, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CHADEMA, Brenda Rupia, ameeleza kusikia taarifa hizo, akisema bado anazifuatilia na chama kitatoa taarifa rasmi pindi zitakapothibitishwa.
Kwa upande wake, Mchome amesema siku ya Jumatano, tarehe 14 Mei 2025, atazungumza na wanahabari kuhusu uamuzi wa Msajili juu ya malalamiko yake kwani hakukataa wala kukubali juu ya taarifa hiyo. Viongozi mbalimbali wa ofisi ya msajili akiwemo Msajili mwenyewe, Jaji Francis Mutungi na au Naibu Msajili, Sisty Nyahoza wametafutwa kuzungumzia suala hilo bila mafanikio. Jitihada za kuwatafuta bado zinaendelea.
ZINAZOFANANA
Kadinali Robert Prevost atangazwa kuwa Papa mpya
Bunge la Ulaya laitaka Tanzania kumuachia huru Lissu
Chatanda ashuhudia utiaji saini wa Bil 13.3 kuboresha miundombinu Rufiji