May 4, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali itachukua hatua kwa waliomshambulia Padri Kitima

Makamu wa Tanzania, Dk. Philip Mpango

 

MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango amesema kuwa, serikali kupitia vyombo vya dola tayari imeshatoa maelekezo ya wale wote waliohusika kwenye shambulizi dhidi ya Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk. Charles Kitima wakamatwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria ili kukomesha vitendo hivyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea)

Dk. Mpango ameyasema hayo hii leo tarehe 04 Mei 2025, wakati wa adhimisho la Misa ya kusimikwa Askofu Stephano Musomba, kwenye jimbo jipya katoliki la Bagamoyo.

Katika Salamu zake, Dk. Mpango alianza kutoa pole kwa Padri Kitima, Baraza la Maaskofu na Kanisa kwa ujumla kwa niaba ya Serikali, na kusema serikali inalaani vikali tukio hilo pamoja na matukio mengine.

“Serikali inalaani vikali na kukemea tukio hilo, pamoja na matukio mengine kama hayo ya uvunjifu wa sheria na Serikali imepokea kwa unyenyekevu rai iliyotolewa na kanisa kupitia makamu wa Rais wa TEC.

“Napenda kuwahakikisha watanzania kuwa, tayari serikali imechukua hatua kupitia wizara ya mambo ya ndani imeviagiza vyombo vya dola kuwatafuta, kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria waliohusika na tukio hilo,” slisema Dk. Mpango.

Ikumbukwe Padri Kitima alishambuliwa usiku wa tarehe 30 Aprili 2025, kwenye makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Kurasini jijini Dar es Salaam, na tayari jeshi la Polisi kupitia taarifa yao wamesema wanamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kuhusika na shambulio hilo.

About The Author

error: Content is protected !!