
Onesmo OleNgurumwa, Mratibu wa THRDC-Taifa
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umewakumbusha waandishi wa habari nchini wajibu wao kwa umma, ikiwa pamoja na kupanga ajenda zenye maslahi ya umma. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … ( endelea).
Leo tarehe 2 Mei 2025, THRDC ikishirikiana na Umoja wa Klabu za waandishi wa habari nchini (UPTC), Baraza la Vyombo vya Habari Tanzania (MCT), imekutana na waandishi wa habari zaidi ya 130 kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Onesmo OleNgurumwa, Mratibu wa THRDC-Taifa, amesema kuwa waandishi wa habari wanapaswa kujua nguvu yao ya kuchagiza mabadiliko kwenye jamii.
“Bahati mbaya waandishi wa habari hamjajua nguvu yenu, waandishi wa habari mna nguvu siku hizi mmekuwa watu wa kupewa ajenda hawezi kuwa na ajenda,” amesema Olengurumwa na kuongeza.
“Waandishi wa habari muwe na ajenda moja yenye maslahi ya taifa. Kwanini tusikamate ajenda ya muafaka wa kitaifa kuelekea kwenye uchaguzi ili twende kwenye uchaguzi tukiwa salama. Haya masuala ya kuvutana hatutasaidia taifa. Sisi waandishi wa habari lengo letu kuisaidia nchi.”
Kenneth Sibaya, Mwenyekiti wa UTPC, amewataka waandishi wa habari kujua wajibu wao ili kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria.
“Kila mtu atekeleze wajibu, sisi waandishi wa habari wajibu wetu kuhakikisha wadau wa uchaguzi wanahakikisha wajibu wao,” amesema Sibaya.
Amesema kuwa chombo cha habari kina nafasi ya kuwapa watu cha kufikiri, “tunaambiwa chombo cha habari hakifundishi watu kufikiri lakini chombo cha habari kinawapa watu cha kufikiria. Amewasihi waandishi wa habari kuzipa nafasi sauti za wengi badala ya sauti chache zenye mamlaka.
Paul Malimbo, mwakilishi wa MCT-Tanzania ametoa wito kwa waandishi kuepuka upendeleo katika kuandika au kutangaza habari.
ZINAZOFANANA
Padre Kitima amuibua Mbatia
Serikali yawaongezea mshahara wafanyakazi
Luhemeja ataka Afrika yenye kukabili mabadiliko ya tabianchi