
KUSHAMBULIWA kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC), Dk. Charles Kitima, kumemuibua James Mbatia, mmoja wa wanasiasa wa siku nyingi nchini. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Anasema, waliomshambuliwa Padre Kitima, ambaye ni ndugu yake na mlezi wake wa kiroho, “walitaka kuondoa uhai wake.”
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, leo tarehe 1 Mei 2025, Mbatia amesema: “Father Kitima ameumizwa sana. Na waliomuumiza walikuwa na dhumuni la kutoa uhai wake.”
Akiongea kwa uchungu, Mbatia amesema, ripoti ya Jeshi la Polisi, kuhusiana na tukio hilo, imejaa kejeli, jambo linalosababisha hasira kwa wananchi.
Anasema, “Tukiangalia mabishano yanayoendelea ndani ya mitandao ya jamii, tukiangalia ripoti ya polisi kuhusu tukio hilo na matukio mengine, unaona wazi wananchi wanatiwa hasira zaidi.”
Ameongeza, “Father Kitima ameumizwa kwenye eneo la TEC. Ameumizwa nyumbani kwake. Hajaumizwa nje; hata angeumizwa nje au maeneo ya wazi, huyu ni kiongozi. Kuna namna ya kulieleza taifa kuhusu jambo hili.
“Polisi ni walinzi wa raia na mali zao. Nawaombea hekima. Taarifa yao imeonesha Padre Kitima alikuwa kwenye kinywaji; wakati siyo kweli. Unapoanza kuhusishaji mambo ya namna hiyo, hujengi umoja wa taifa, bali unachochea vurugu,” amefafanua Mbatia ambaye ni mtaalamu wa majanga.
Ametoa pole kwa Rais wa TEC na kwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini. Hakufafanua.
Kwa mujibu wa Mbatia, ni muhimu kujenga tabia ya kustahamili wakosoaji wa serikali.
Kushambuliwa kwa Padre Kitima kumekuja katika kipindi ambacho yeye na kanisa lake, wamejitokeza kuwa wakosoaji wakubwa wa mifumo ya uchaguzi na wizi wa kura kwenye chaguzi nchini.
Kwa takribani mwaka mmoja sasa, Mbatia hajasikika kwenye vyombo vya habari kuzungumzia masuala mbalimbali ya kitaifa yanayoendelea nchini.
Baadhi ya wakosoaji wake, wanamlaumu kwa kukalia kimya kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani Tundu Lissu, wakihusisha kimya hicho na ukaribu wake na serikali.
Lakini Mbatia amekana madai hayo akisema, “kila jambo linazungumzwa kwa wakati wake.”
Wakati hayo yakiendelea, Baraza la Maaskofu limelaani na kueleza lilivyosikitishwa sana na tukio baya na uovu la kuvamiwa na kujeruhiwa Padre Kitima.
Taarifa ya baraza hilo kwa umma, iliyotolewa na Makamu wake wa Rais, Askofu Euseblus Nzigilwa, imeitaka “jeshi la polisi na vyombo vingine kuchukua hatua za haraka, kuwabaini na kuwakamata wote waliohusika katika kupanga na kutekeleza uhalifu huo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Imeongeza, “Uchunguzi wa tukio hilo, ufayike haraka na taarifa zitolewe kwa uwazi bila upotoshaji wowote ili kurudisha imani na matumaini kwa watu wetu.”
Haya yanajiri wakati Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muriro, ameeleza kuwa jeshi hilo, linachunguza tukio la kushambuliwa kwa Padre Kitima, aliyejeruhiwa kichwani usiku wa tarehe 30 Aprili.
Alisema, Padre Kitima alikuwa ametoka kuhudhuria kikao cha viongozi wa dini kilichodumu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa moja jioni.
Baada ya kikao hicho, aliendelea kubaki katika kantini ya baraza hilo, kwa ajili ya kupata kinywaji, ambapo baadaye alielekea maliwatoni na ndipo alipovamiwa na kushambuliwa na watu wawili waliotumia kitu butu.
Akaongeza, Jeshi la Polisi linamshikilia mtu mmoja, Rauli Mahabi (maarufu kama Haraja), mkazi wa Kurasini, kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tukio hilo, huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kuwabaini wote waliohusika na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa mara moja.
Kwa sasa, Padre Kitima anapatiwa matibabu katika hospitali ya Aga Khan na hali yake inaendelea vizuri.
ZINAZOFANANA
Serikali yawaongezea mshahara wafanyakazi
Luhemeja ataka Afrika yenye kukabili mabadiliko ya tabianchi
Mtu mmoja mbaroni kwa kushambuliwa Padri Kitima