April 13, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Othman: Tutairudisha mamlaka yenu

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman

 

MWENYEKITI wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema serikali atakayoiongoza baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 itawarudishia Wazanzibari mamlaka ya nchi yao iliyo huru na inayostahili kuongozwa kidemokrasia. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Amesema Zanzibar ina historia ya karne na karne ya kuwa nchi mashuhuri iliyovutia watu wa mataifa mbalimbali ya nje kuja kufanya biashara na kujifunza mambo tofauti.

Ameyasema hayo katika mkutano wake na viongozi wa ngazi mbalimbali kwenye ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Kisongo Makunduchi, Wilaya ya Kusini.

Mwenyekiti Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema ataongoza nchi yenye heshima na haiba inayotambuliwa kuwahi kuipatia maendeleo ya kiwango cha juu na kuwa kituo muhimu kwa ajili ya biashara ya kimataifa.

Amesema kwa saaa haiba na heshma ya Zanzibar imetoweka kutokana na viongozi waliopo kushindwa kutumikia watu badala yake wakijinufaisha binafsi.

“Tuna nchi leo imevurugwa kwelikweli. Kama ni ujanadume basi imebaki mwanamme suruali. Kila serikali inachotaka kukifanya inaambiwa hapana ni jambo la Muungano.

“Tumefikishwa mahali pagumu sana mpaka sasa. Watu hawapewi haki zao kwa sababu huku chini kwenye serikali za mitaa waliopewa dhamana ni wageni. Unaye Sheha lakini yupo Naibu Sheha ndio amepewa mamlaka ya kutambua huyu ni mwenyeji huyu siye. Hii haikubaliki kwa sababu si hulka ya nchi hii,” alisema.

Othman amesema mfumo wa Muungano unaofanya kazi umesababisha maisha ya kinyonge kwa Wazanzibari tofauti na upande mwengine wa Muungano ambako wanachopigania ni mtu gani makini aongoze nchi yao.

Amesema wao wanayo nchi tatizo haijaongozwa kwa kutumikia watu kama yalivyo matumaini yao. Watu wanataka kuongozwa kwa imani na utu huku akihakikishiwa haki zake zote za kiraia na viongozi wakitumikia watu sio watu wakakandamizwa na serikali yao.

Ni msimamo wa ACT Wazalendo kwamba Muungano wenye tija ni ule ambao watu wenyewe wameuchagua kama inavyoonekana kwenye nchi nyengine duniani zilizoungana; akiitolea mfano Uskochi na Uingereza zilizoungana mwaka 1707.

Alisema nchi hizo mbili zina historia inayorudi mwaka 1502 walipoacha kupigana na kuingia mkataba wa kushirikiana. Nchi hizo tangu hapo zimekuwa na muungano wenye tija na kuheshimiana.

Alisema anatarajia wananchi wapewe nafasi ya kuchagua chama wanachokitaka ili ridhaa yao itumiwe kuundwa serikali makini itakayoongoza kwa uadilifu na imani ya kujenga watu na matumaini yao.

“Hakuna nafasi ya kuwatumia wananchi kujitwalia madaraka kishetani. Hakuna nafasi ya kuhujumu uchaguzi, mwisho wao umefika,” alisema.

Othman ambaye alijiunga na ACT Wazalendo mwaka 2021 akirithi wadhifa alouacha Maalim Seif Shariff Hamad, aliyefariki dunia Februari 17 mwaka huo, anatarajiwa kesho kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kuteuliwa kuwania urais wa Zanzibar, kwa mara ya kwanza maishani mwake.

Kiutumishi, Othman amekuwa mtumishi aliyepanda ngazi hadi kufikia ofisa mwandamizi serikalini mpaka alipofukuzwa kazi mwaka 2014 baada ya kutoa msimamo wa kukataa Katiba iliyopendekezwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Bunge Maalum la Katiba.

Wakati ule alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar chini ya urais wa Dk. Ali Mohamed Shein. Msimamo aloutoa Othman ulionekana kutotii matakwa ya Chama Cha Mapinduzi [CCM], kinachoendelea kushika dola kwa mbinde kila ufikapo uchaguzi mkuu.

About The Author

error: Content is protected !!