
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amesema moja ya sababu zilizopelekea TTCL kuonesha hasara ni uhamishwaji wa Mkongo wa Taifa kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenda shirika la TTCL. Anaripoti Apaikunda Mosha, Dar es Salaam … (endelea).
Amezungumza hayo leo Jumatano, tarehe 2 Aprili 2025, amesema kuwa hasara ya Sh. 28 bilioni iliyosemwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) haina maana ya kuwa biashara imeshindwa kujiendesha, bali inahusiana na kanuni za kihasibu zinazotumika kwenye mashirika ya umma.
Ameeleza kuwa mkongo huo una thamani kubwa, hivyo unapouhamisha kutoka kwenye vitabu vya wizara kwenda kwenye vitabu vya shirika, moja kwa moja unakuwa umeongeza mali kwenye mizania ya shirika, hivyo moja ya gharama kubwa zinazotokea ni uchakavu wa mkongo huo (depreciation).
“Gharama ya uchakavu wa mkongo kwa mwaka mmoja wa fedha ni Sh. 36 bilioni, lakini kwa kipindi cha Novemba 2023 hadi Juni 2024, ilifikia Sh. 27 bilioni, ambayo kwenye vitabu vya hesabu inaingizwa kama matumizi (expenses) kwenye hesabu za TTCL. Kumbuka pia TTCL tayari ilikuwa na hasara iliyokuwa imebaki (carried forward) ya Shilingi bilioni 4 kutoka mwaka uliopita. Ukijumlisha zote mbili, unapata ile hasara ya karibu Sh. 28 bilioni iliyotajwa na CAG,” amefafanua Silaa.
Silaa amesema kwa Mtanzania wa kawaida, unapozungumzia faida na hasara, anazingatia tu hesabu rahisi za biashara ndogo ndogo. Mfano, ukinunua kuku wa Shilingi elfu 10 kutoka Singida, lazima uangalie nauli yako, gharama ya chakula huko na bei ya kuuza ili upate faida. Lakini kwa mashirika makubwa kama TTCL, hesabu ni tofauti.
Hivyo kwa mujibu wa Silaa kama hesabu za TTCL zingefanywa kwa njia rahisi kama biashara ya kuuza kuku, shirika hilo lingekuwa lina faida. Licha ya ripoti ya CAG kuonesha hasara.
Aidha, Silaa amesisitiza kuwa licha ya hasara hiyo TTCL bado inaendelea kujiendesha bila matatizo na inaendelea kutoa huduma kwa Watanzania kama kawaida.
Hivyo amewataka Watanzania kutoingiwa na hofu kuhusu ripoti hiyo na amewaarifu kuwa ripoti hiyo itajadiliwa bungeni kupitia kamati za kudumu za Bunge ili kutoa uelewa sahihi kwa Watanzania na kusaidia wabunge kuhoji kwa niaba ya wananchi.
ZINAZOFANANA
Exim yaboresha mikopo kwa Watumishi wa Umma kupitia ‘Utumishi Portal’
EWURA Yatangaza Bei za Mafuta kwa mwezi Aprili 2025
Wanawake wasiojistiri vyema ni wachafu