
Siglada Mligo
MWENYEKITI wa Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA), Kanda ya Nyasa, Tabia Mwakikuti amesema, tukio la kushambuliwa kwa kiongozi wao, Siglada Mligo, limechochewa kisiasa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Njombe … (endelea).
“Nilikuwepo kwenye Kikao kilichofanyika ukumbi wa Milimani – Njombe Mjini, kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche, juzi tarehe 25 Machi 2025. Nimeona na kushuhudia upotoshaji mkubwa unaosambaa kuhusu kupigwa kwa Siglada Mligo na kutolewa ndani ya ukumbi.
“Nikiwa kama Mwenyekiti wa BAWACHA Kanda ya Nyasa, naomba kuelezea mambo machache, wakati tunasubiri hatua zingine ndani ya chama,” anaeleza Tabia.
Anaongeza: “Siglada Mligo, Mwenezi Bawacha Taifa, alipewa muda mrefu kuliko wajumbe wote wa kikao kile kujieleza na kujibu tuhuma mbalimbali. Hakuwa yeye pekee yake, aliyetwakiwa kutoa ufafanuzi.
“Lakini mara zote ilipofika zamu yake, Makamu wa chama, alijitahidi kumpa muda mrefu. Inapofika wakati wa kuzungumza watu wengine, ni lazima Siglada asimame na kuleta fujo kutoruhusu ili kuzuia maoni ya wengine.”
Amesema, “Makamu alikuwa na busara sana, hadi Dk. Willibroad Slaa alisema, ningekuwa naendesha kikao hiki enzi hizo, pengine nisingekuwa na busara uliyoonyesha hapa. Akampongeza kwa kweli.
“Wote tuliokuwepo ndani ya kikao na tuliokuwa na mapenzi mema na chama, tulikubaliana Mwenezi wa Bawacha ni mtovu wa nidhamu, kutokana na matendo yake ndani ya kikao.”
Anasema, hataki kueleza tuhuma zilizomkabili Siglada kwa kuwa suala hilo, linataratibu zake za kulishughulikia.
Lakini Tabia anasema: “Sisi Bawacha tusijifunike kwenye kivuli cha kuvunja sheria na taratibu, kisha tukatafuta huruma na kusambaza uongo na matukio ya kukivuruga chama. Kamwe hatutakubali.”
Anasema: “Nashauri wanawake wote tusiingie mkenge wa kushabikia tuhuma na matukio ambayo hatuna uhakika nazo. Haki itatendeka na tusitumie jinsia zetu kutetea mambo ambayo hayana nidhamu kwa chama.”
ZINAZOFANANA
Wassira ataja Chanzo cha Deni la Sh. 97 Trilioni.
Mwenezi Bawacha ashambuliwa mlinzi, Polisi wafunguka
Hatua za msajili analenga kuinyamazisha ajenda ya Chadema