February 27, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mwana FA aivulia kofia Serikali ya Rais Samia

 

MBUNGE wa Jimbo la Muheza na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ameishukuru Serikali kwa  maendeleo katika sekta  mbalimbali  ndani ya wilaya yake pamoja na  mafanikio makubwa ya uboreshwaji wa huduma za kijamii ndani ya wilaya hiyo. Anaripoti Apaikunda Mosha. Tanga…(endelea). 

Amezungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika alhamisi, 27 Februari 2025. Mwinjuma kwa niaba ya wananchi wa Muheza amepongeza juhudi za serikali ya awamu ya sita kwa kuleta maendeleo wilayani hapo.

Amesema katika  kipindi cha miaka minne sekta ya Afya wilaya ya Muheza imenufaika na jumla ya Sh. 5.1 bilioni, ambapo bilioni 4.3 zimetumika kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, ikijumuisha ujenzi wa majengo, ununuzi wa vifaa tiba na rasilimali watu.

Aidha, amesema serikali ilitoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha kimkakati katika Tarafa ya Bwembera, kilichojengwa katika Kata ya Kwafungo na sasa kinafanya kazi.

Mbali na hayo, serikali imechangia kukamilika kwa ujenzi wa zahanati saba katika kata mbalimbali za jimbo hilo, huku akimuomba Rais kupitisha ombi la utoaji wa fedha katika ujenzi wa kituo kingine cha afya cha kimkakati cha Tarafa ya Amani ambacho kinatarajiwa kujengwa Kata ya Misalai, eneo la Mgambo.

Kwa upande wa Elimu, amesema Muheza  idadi ya kata 37 kata 13 zilikuwa hazina  shule za sekondari na sasa zimebaki kata 2 ambazo hazina shule za sekondari na wanatarajia kupata shule hizo kabla ya kufikia kipindi cha uchaguzi, hata hivyo ameipongeza serikali kwa kazi kubwa, kwani ndani ya kipindi cha miaka minne, vyumba vya madarasa 219 vimejengwa kwa shule za msingi na 106 kwa shule kwa za sekondari.

Mwinjuma amezungumza juu ya nishati ya umeme, amesema serikali imepeleka umema  vijiji 75 kati ya 126 vya Muheza, kati ya vitongoji 512  mpaka sasa vimebaki 65 huku vitongoji 22 vikiwa kwenye mpango wanafanyia kazi, hivyo vilivyobaki 43 meneja wa REA ameahidi 30 kati ya hivyo kuwekwa kwenye mpango wa Mei na amesesisitiza kuwa kufikia mwisho wa mwaka huu kote kutakuwa na umeme.

Katika suala la maji, Mwinjuma amesema kuwa, hali ya upatikanaji wa maji ilikuwa mbaya na hivi sasa imeongezeka kutoka asilimia 41 hadi 71 kwa mijini na kutoka asilimia 53 hadi 73  kwa vijijini hivyo hayo ni maendeleo makubwa na wanatarajia kufikia asilimia 100 ifikapo mwishoni mwa mwaka.

Aidha, Mwinjuma ameomba serikali kujenga soko la kitaifa la machungwa na mazao ya viungo Muheza ili kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri na mazao yao hayaharibiki baada ya kuvuna au kuuza kwa bei ya hasara.

About The Author

error: Content is protected !!